Part 10
41. NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi khums (sehemu moja
katika tano) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na mayatima, na
masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo
yateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuo, siku yalipo kutana majeshi mawili.
Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
42. Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya
bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na
ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili
Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie
wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili
zilizo dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
43. Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache
- na lau angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli
zozana katika jambo
44. Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni
wachache, na akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu
atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu.
45. Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na
mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.
46. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane
mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu
pamoja na wanao subiri.
47. Wala msiwe kama wale walio toka majumbani mwao kwa fakhari na
kujionyesha kwa watu, na wakawazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu ameyazunguka yote wanayo yafanya.
48. Na pale Shet'ani alipo wapambia vitendo vyao, na akawaambia:
Hapana watu wa kukushindeni hii leo, na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipo onana
majeshi mawili, akarudi nyuma, na akasema: Mimi si pamoja nanyi. Mimi naona
msiyo yaona. Mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkali wa
kuadhibu.
49. Na walipo sema wanaafiki, na wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao:
Watu hawa dini yao imewadanganya. Na Mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu basi
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Ametukuka, na Mwenye hikima.
50. Na laiti ungeli ona Malaika wanapo wafisha wale walio kufuru
wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, na kuwaambia: Ionjeni adhabu ya Moto!
51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyo kwisha tangulizwa na mikono
yenu, na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.
52. Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa kabla yao - walizikataa
Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa sababu ya madhambi
yao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mkali wa kuadhibu.
53. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo
waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika
Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
54. Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao -
walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao. Na
tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu.
55. Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni
wale wanao kufuru, basi hao hawaamini;
56. Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi, kisha wanavunja
ahadi yao kila mara, wala hawamchi Mungu.
57. Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma yao ili wapate
kukumbuka.
58. Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie ahadi
59. Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao wametangulia mbele.
La, wao hawatashinda.
60. Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio
fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu,
na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa chochote
katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa.
61. Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu.
Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
62. Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu atakutosheleza. Kwani
Yeye ndiye aliye kuunga mkono kwa nusura yake na kwa Waumini.
63. Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo
duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye
waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
64. Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na Waumini walio
kufuata.
65. Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani. Wakiwapo kati yenu
ishirini wanao subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo kati yenu mia
watawashinda elfu moja katika walio kufuru. Kwa sababu wao ni watu wasio
fahamu.
66. Sasa Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua kuwa upo udhaifu
kwenu. Kwa hivyo wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye kusubiri
watawashinda mia mbili. Na wakiwapo elfu moja watawashinda elfu mbili, kwa
idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
67. Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda
baraabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka
Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
68. Lau isingeli kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa
Mwenyezi Mungu ingeli kupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyo chukua.
69. Basi kuleni katika mlivyo teka, ni halali na vizuri, na mcheni
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye
kurehemu.
70. Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi
akiona kheri yoyote nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko vilivyo chukuliwa
kwenu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu.
71. Ikiwa wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha mfanyia khiana
Mwenyezi Mungu kabla yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
72. Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya
Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na
wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini
hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame.
Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo
kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu
anayaona mnayo yatenda.
73. Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipo
fanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa.
74. Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya
Mwenyezi Mungu, na walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa
kweli. Watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema.
75. Na watakao amini baadaye na wakahajiri, na wakapigana Jihadi
pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa nasaba wanastahikiana
wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
9 - AT-TAWBA
1. Huku ni kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwenye jukumu la
maagano na mlio ahidiana nao katika washirikina.
2. Basi tembeeni katika nchi miezi mine, na jueni kwamba nyinyi
hamwezi kumshinda Mwenyezi Mung, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anaye wahizi
makafiri.
3. Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote
siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa
washirikina. Basi mkitubu itakuwa kheri kwenu, na mkigeuka basi jueni kuwa
nyinyi hamumshindi Mwenyezi Mungu. Na wabashirie makafiri kuwa watapata adhabu
chungu.
4. Isipo kuwa washirikina ambao mliahidiana nao kisha
wasikupunguzieni chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi hao
watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda
wacha-Mungu.
5. Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote
mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia. Lakini
wakitubu, wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi waachilieni. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
6. Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi
mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa
amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.
7. Itakuwaje iwepo ahadi na washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na
mbele ya Mtume wake, ila wale mlio ahidiana nao kwenye Msikiti Mtakatifu? Basi
maadamu wanakwenda nanyi sawa, nanyi pia nendeni sawa nao. Hakika Mwenyezi
Mungu huwapenda wachamngu
8. Itakuwaje! Nao wakikushindeni hawatazami kwenu udugu wala ahadi.
Wanakufurahisheni kwa midomo yao tu, na nyoyo zao zinakataa hayo. Na wengi wao
ni wapotovu.
9. Wamenunua thamani ndogo kwa Ishara za Mwenyezi Mungu, na
wakazuilia watu na Njia yake. Hakika hao ni maovu waliyo kuwa wakiyatenda.
10. Hawatazami kwa Muumini udugu wala ahadi; basi hao ndio warukao
mipaka.
11. Basi wakitubu na wakashika Sala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu
zenu katika Dini. Na tunazichambua Aya kwa watu wajuao.
12. Na wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao, na wakatukana
Dini yenu, basi piganeni na waongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo vya
kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha.
13. Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo vyao na wakawa na hamu
ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara ya kwanza? Je, mnawaogopa?
Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope, ikiwa nyinyi ni Waumini.
14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na
awahizi na akunusuruni muwashinde, na avipoze vifua vya kaumu ya Waumini,
15. Na aondoe hasira ya nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba
ya amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
16. Je, mlidhani kuwa mtaachwa tu, bila ya Mwenyezi Mungu kuwajuulisha
wale walio pigana Jihadi kati yenu, na wala hawakumfanya mwendani wao isipo
kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wenziwe? Na Mwenyezi Mungu anazo
khabari za yote mnayo yatenda.
17. Haiwi kuwa makafiri ndio waamirishe misikiti ya Mwenyezi Mungu,
hali wanajishuhudishia wenyewe ukafiri. Hao ndio ambao vitendo vyao
vimeharibika, na katika Moto watadumu.
18. Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao
muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka,
na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika
waongofu.
19. Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na kuamirisha Msikiti
Mtakatifu ni sawa na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na
akapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
20. Wale walio amini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia
ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele
ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu.
21. Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo kwake, na radhi, na
Bustani ambazo humo watapata neema za kudumu.
22. Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo
makubwa.
23. Enyi mlio amini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa vipenzi
vyenu ikiwa wanastahabu ukafiri kuliko Imani. Na katika nyinyi atakaye wafanya
hao ndio vipenzi vyake, basi hao ndio madhaalimu.
24. Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu,
na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na
majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume
wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri
yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
25. Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika mapigano mengi, na
siku ya Hunayni ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni
kitu. Na ardhi ikawa dhiki kwenu juu ya upana wake. Kisha mkageuka mkarudi
nyuma.
26. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake
na juu ya Waumini. Na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu
wale walio kufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
27. Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu atawasamehe awatakao. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
28. Enyi mlio amini! Hakika washirikina ni najsi, kwa hivyo
wasiukaribie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka wao huu. Na ikiwa mnakhofia
umasikini, basi Mwenyezi Mungu atakutajirisheni kwa fadhila yake akipenda.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
29. Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho,
wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala hawashiki Dini
ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa khiari yao, hali
wamet'ii.
30. Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu. Na Wakristo
wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao.
Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize!
Wanageuzwa namna gani hawa!
31. Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala
ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipo kuwa
wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo
wanayo mshirikisha nayo.
32. Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na
Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru yake ijapo kuwa makafiri
watachukia.
33. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki
ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
34. Enyi mlio amini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki
wanakula mali za watu kwa baat'ili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanao
kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.
35. Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo
vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya
ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.
36. Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili
katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo
iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu
humo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wnavyo pigana nanyi nyote. Na
jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
37. Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi katika kukufuru; kwa
hayo hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka
mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi
Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa
ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
38. Enyi mlio amini! Mna nini mnapo ambiwa: Nendeni katika Njia ya
Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia
kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na ya Akhera
ni chache.
39. Kama hamwendi atakuadhibuni adhabu chungu, na atawaleta watu
wengine, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila
kitu.
40. Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha
mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa
katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu
yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono
kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno
la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye
hikima.
41. Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na piganeni Jihadi kwa
mali yenu na nafsi zenu katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Haya ni kheri kwenu
mkiwa mnajua.
42. Na lau ingeli kuwa ipo faida ya papo kwa papo, na safari yenyewe
ni fupi, wangeli kufuata. Lakini wameona ni mbali na kuna mashaka. Nao wataapa
kwa Mwenyezi Mungu: Tungeli weza bila ya shaka tungeli toka pamoja nanyi.
Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni
waongo.
43. Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa ruhusa kabla ya
kubainikia kwako wanao sema kweli, na ukawajua waongo?
44. Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuwajua wachamngu.
45. Wasio muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na nyoyo zao
zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa. Basi hao wanataradadi katika
shaka zao.
46. Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangeli
jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo
akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!
47. Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na
wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao
wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
48. Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na wakakupindulia mambo
juu chini, mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya Mwenyezi Mungu, na wao
wamechukia.
49. Na miongoni mwao wapo wanao sema: Niruhusu wala usinitie katika
fitina. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika
Jahannamu imewazunguka.
50. Ukikupata wema unawachukiza, na ukikusibu msiba, wao husema:
Sisi tuliangalia mambo yetu vizuri tangu kwanza. Na hugeuka kwenda zao nao
wamefurahi.
51. Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye
Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu!
52. Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipo kuwa moja katika
mema mawili? Na sisi tunakutazamieni kuwa Mwenyezi Mungu akufikishieni adhabu
itokayo kwake, au kutokana na mikono yetu. Basi ngojeni, nasi tunangoja pamoja
nanyi.
53. Sema: Toeni mkipenda msipende. Hakitopokelewa kitu kwenu, kwani
nyinyi ni watu wapotovu.
54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa kuwa walimkataa
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala ila kwa uvivu, wala
hawatoi michango ila nao wamechukia.
55. Yasikufurahishe mali yao wala wana wao. Hakika Mwenyezi Mungu
anataka kuwaadhibu kwayo hapa duniani, na zitoke roho zao na hali wao ni
makafiri.
56. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, wala
wao si katika nyinyi. Lakini ni watu wanao ogopa.
57. Lau kama wangeli pata pa kukimbilia au mapango au pahala pa
kuingia basi wangeli fyatuka mbio kuelekea huko.
58. Na miongoni mwao wapo wanao kusengenya katika kugawa sadaka.
Wanapo pewa wao huridhika. Na wakito pewa hukasirika.
59. Na laiti wao wangeli ridhia kile alicho wapa Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa
katika fadhila yake - na pia Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi
Mungu!
60. Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia,
na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
61. Na miongoni mwao wapo wanao muudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni
sikio tu. Sema: Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamuamini Mwenyezi Mungu, na ana
imani na Waumini, naye ni rehema kwa wanao amini miongoni mwenu. Na wanao
muudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu watapata adhabu chungu.
62. Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni nyinyi, hali ya
kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lau kama
wao ni Waumini.
63. Je, hawajui ya kwamba anaye shindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
basi huyo atapata Moto wa Jahannamu adumu humo? Hiyo ndiyo hizaya kubwa.
64. Wanaafiki wanaogopa isije teremshwa Sura itakayo watajia
yaliyomo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni mzaha! Hakika Mwenyezi Mungu atayatoa
nje hayo mnayo yaogopa.
65. Na ukiwauliza, wanasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na
kucheza tu. Sema: Mlikuwa mkimfanyia maskhara Mwenyezi Mungu na Ishara zake na
Mtume wake?
66. Msitoe udhuru; mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu!
Tukilisamehe kundi moja kati yenu, tutaliadhibu kundi jingine kwa kuwa wao ni
wakosefu.
67. Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali moja.
Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi
Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanaafiki ndio wapotofu.
68. Mwenyezi Mungu amewaahidi wanaafiki wanaume na wanaafiki
wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu kudumu humo. Hayo yanawatosha, na
Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu milele.
69. Ni kama wale walio kuwa kabla yenu. Walikuwa wana nguvu na mali
na watoto zaidi kuliko nyinyi. Basi walistarehea fungu lao, na nyinyi
mnastarehea fungu lenu, kama walivyo starehe kwa fungu lao wale walio kuwa
kabla yenu. Na nyinyi mkazama katika maovu kama wao walivyo zama. Hao ndio
ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na Akhera; na hao ndio walio
khasiri.
70. Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla yao - kaumu ya
Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na miji
iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi. Basi
Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini wao walikuwa wakijidhulumu
wenyewe.
71. Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki
walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na
humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
72. Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake
Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi mema katika Bustani za
kudumu, na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu
kukubwa.
73. Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na wakazanie. Na
makaazi yao ni Jahannamu, na huo ndio mwisho mbaya.
74. Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema
neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya
ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume
wake amewatajirisha kutokana na fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na
wakigeuka Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala
hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru.
75. Na miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema:
Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika
watendao mema.
76. Alipo wapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na
wakageuka, na huku wakipuuza.
77. Basi akawalipa unaafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo
kutana naye, kwa sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyo
muahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.
78. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong'ono
yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua sana ya ghaibu?
79. Wale wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka nyingi na wasio
nacho cha kutoa ila kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli. Mwenyezi Mungu
atawakejeli wao! Nao watapata adhabu chungu!
80. Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara
sabiini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotofu.
81. Walifurahi walio achwa nyuma kwa kule kubakia kwao nyuma na
kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walichukia kupigana Jihadi kwa mali zao na
nafsi zao, na wakasema: Msitoke nje katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una
joto zaidi, laiti wangeli fahamu!
82. Basi nawacheke kidogo; watalia sana. Hayo ni malipo ya yale
waliyo kuwa wakiyachuma.
83. Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni
mwao - na wakakutaka idhini ya kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami
kabisa, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Nyinyi mliridhia kukaa nyuma mara
ya kwanza, basi kaeni pamoja na hao watakao bakia nyuma.
84. Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame
kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakafa
na hali ni wapotofu.
85. Wala zisikushitue mali zao na watoto wao. Mwenyezi Mungu anataka
kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke roho zao na hali wao ni makafiri.
86. Na inapo teremshwa Sura isemayo: Muaminini Mwenyezi Mungu na
piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu miongoni mwao hukutaka
ruhusa na husema: Tuache tuwe pamoja na wanao kaa nyuma!
87. Wameridhia kuwa pamoja na wabakiao nyuma, na nyoyo zao zikapigwa
muhuri; kwa hivyo hawafahamu.
88. Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi
kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio
wenye kufanikiwa.
89. Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake,
wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
90. Na walikuja wenye kutoa udhuru katika Mabedui ili wapewe ruhusa,
na wakakaa wale walio mwambia Mwenyezi Mungu na Mtume wake uwongo. Itawafika walio
kufuru katika wao adhabu chungu.
91. Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio pata cha kutumia,
maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu
wanao fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
92. Wala wale walio kujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha
kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya
kukosa cha kutoa.