Part 13
53. NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu,
isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika Mola wangu Mlezi
ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
54. Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe khasa.
Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na
umeaminika.
55. Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi
ni mlinzi mjuzi.
56. Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo
popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo
ya wafanyao mema.
57. Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio amini na
wakawa wachamngu.
58. Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia kwake. Yeye akawajua na
wao hawakumjua.
59. Na alipo watengenezea tayari haja
60. Na msipo niletea basi hampati kipimo chochote kwangu, wala
msinikurubie.
61. Wakasema: Sisi tutamrairai baba yake; na bila ya shaka tutafanya
hayo.
62. Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao katika mizigo
yao, ili wazione watakapo rudi kwa watu wao wapate kurejea tena.
63. Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu!
Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate kupimiwa; na
yakini sisi tutamlinda.
64. Je, nikuaminini kwa huyu ila
65. Na walipo fungua mizigo
66. Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu
kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipo mpa ahadi
67. Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni
kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu
yake Yeye wategemee wanao tegemea.
68. Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao, haikuwafaa kitu
kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi ya Yaa'qub
aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu tulimfundisha; lakini
watu wengi hawajui.
69. Na walipo ingia kwa Yusuf alimchukua nduguye akasema: Mimi
hakika ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyo kuwa wakiyafanya .
70. Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha
kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri!
Hapana shaka nyinyi ni wezi!
71. Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini?
72. Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta atapewa
shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo.
73. Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya
uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi.
74. Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa nyinyi ni
waongo?
75. Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo yeye huyo
ndiye malipo yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
76. Basi akaanza kwenye mizigo
77. Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba
zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha.
Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi
hayo mnayo singizia.
78. Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee
79. Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote yule isipo
kuwa tuliye mkuta naye kitu chetu. Hivyo basi tutakuwa wenye kudhulumu.
80. Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao
akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu kutokana na
Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi
mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu
anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu.
81. Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba.
Na sisi hatutoi ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye
kuhifadhi mambo ya ghaibu.
82. Na waulize watu wa mji tulio kuwako, na msafara tulio kuja nao.
Na hakika sisi tunasema kweli.
83. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani.
Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni
Mjuzi Mwenye hikima.
84. Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Masikini Yusuf! Na macho
yake yakawa meupe kwa huzuni aliyo kuwa akiizuia.
85. Wakasema: Wallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au
uwe katika walio hiliki.
86. Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu
na huzuni yangu. Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
87. Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate
tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi
Mungu isipo kuwa watu makafiri.
88. Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata
shida, sisi na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya
kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka.
89. Akasema: Je! Mmejua mliyo mfanyia Yusuf na nduguye mlipo kuwa
wajinga?
90. Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na
huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu
na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema.
91. Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko
sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa.
92. Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu
atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu.
93. Nendeni na kanzu yangu hii na mumwekee usoni baba yangu, atakuwa
mwenye kuona. Na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.
94. Na ulipo ondoka tu msafara baba yao alisema: Hakika mimi nasikia
harufu ya Yusuf, lau kuwa hamtanituhumu.
95. Wakasema: Wallahi! Hakika bado ungali katika upotovu wako wa
zamani.
96. Basi alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni pake alirejea
kuona. Akasema: Je! Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi Mungu msiyo yajua
nyinyi?
97. Wakasema: Ee baba yetu! Tuombee msamaha kwa dhambi zetu. Hapana
shaka sisi tulikuwa na makosa.
98. Akasema: Nitakuja kuombeeni msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika
Yeye ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kusamehe.
99. Na walipo ingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema:
Ingieni Misri, Inshallah, mmo katika amani.
100. Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote
wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile
ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi
Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya
Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole
kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
101. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na umenifunza
tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika
dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe na watendao
mema.
102. Hizi ni katika khabari za ghaibu tulizo kufunulia. Na hukuwa
pamoja nao walipo azimia shauri yao, walipo fanya njama zao wakizua
vitimbi.
103. Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi..
104. Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Hayakuwa haya ila ni mawaidha
kwa walimwengu wote.
105. Na ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazo zipitia, na hali
ya kuwa wanazipuuza.
106. Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni
washirikina.
107. Je! Wanaaminisha kuwa haitowajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya
kuwagubika, au haitawafikia Saa ya Kiyama kwa ghafla, na hali hawatambui?
108. Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa
kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si
katika washirikina.
109. Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa wanaume tulio
wafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika ardhi
wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya
Akhera ni bora kwa wamchao Mungu. Basi hamfahamu?
110. Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa wamekadhibishwa,
hapo ikawajia nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu yetu haitowawacha
kaumu ya wakosefu.
111. Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si
maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa
kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.
13 - AR-RAA'D
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Alif Lam Mym Ra. (A.L.M.R.) Hizi ni Ishara za Kitabu. Na uliyo teremshiwa
kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki. Lakini wengi wa watu hawaamini.
2. Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo mnazo ziona,
ametawala kwenye Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii, kila kimoja
kinakwenda kwa kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua Ishara ili
mpate kuwa na yakini kukutana na Mola wenu Mlezi.
3. Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima na mito. Na
katika kila matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana.
Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.
4. Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani
za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na
isio chipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya
baadhi yao bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa
watu wanao tia mambo akilini.
5. Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Ati
tukisha kuwa mchanga kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio walio mkufuru
Mola wao Mlezi. Na hao ndio watao kuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio
watu wa Motoni. Humo watadumu.
6. Na wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa
zimekwisha pita kabla yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi
ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni
Mkali wa kuadhibu.
7. Na wale walio kufuru husema: Mbona hakuteremshiwa muujiza kutoka
kwa Mola wake Mlezi? Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa
kuwaongoa.
8. Mwenyezi Mungu anajua mimba abebayo kila mwanamke, na kinacho
punguka na kuzidi matumboni. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.
9. Yeye ndiye Mwenye kujua yanayo onekana na yasio onekana; Mkuu
Aliye tukuka.
10. Ni sawa anaye ficha kauli yake kati yenu na anaye idhihirisha,
na anaye jibanza usiku na anaye tembea jahara mchana.
11. Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake
linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko
kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao. Na Mwenyezi Mungu anapo
watakia watu adhabu hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala
yake.
12. Yeye ndiye anaye kuonyesheni umeme kwa khofu na tamaa, na
huyaleta mawingu mazito.
13. Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia,
kwa kumkhofu. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana
juu ya Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Mwenye adhabu kali!
14. Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba badala yake
hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji
ili yafike kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila
katika upotovu.
15. Na viliomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyezi Mungu
tu vikitaka visitake. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni.
16. Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi
Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao
hawajifai wenyewe kwa jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona huwa
sawa? Au hebu huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu
washirika walio umba kama alivyo umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia?
Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye
kushinda!
17. Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji
kwa kadiri yake. Na mafuriko yakachukua mapovu yaliyo kusanyika juu yake. Na
kutokana na wanavyo yayusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea
povu vile vile. Namna hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo anavyo piga mifano ya Haki na
baat'ili. Basi lile povu linapita kama takataka tu basi. Ama kinacho wafaa watu
hubakia kwenye ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga mifano.
18. Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia,
hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya
shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao
yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahala pabaya mno!
19. Je! Anaye jua ya kwamba yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola
wako Mlezi ni Haki ni sawa na aliye kipofu? Wenye akili ndio wanao
zingatia,
20. Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wala hawavunji
maagano.
21. Na wale ambao huyaunga aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na
wanaikhofu hisabu mbaya.
22. Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi, na
wakashika Sala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo wapa; na
wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya
Akhera.
23. Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio wema
miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia
katika kila mlango.
24. (Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu
ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.
25. Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga,
na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika
nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.
26. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa
kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na
Akhera si kitu ila ni starehe ndogo.
27. Na wanasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka
kwa Mola wake Mlezi. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humwacha kupotea amtakaye, na
humwongoa anaye elekea kwake,
28. Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi
Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!
29. Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo
mazuri.
30. Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao wamekwsiha pita kabla
yao umati nyengine, ili uwasomee tunayo kufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani,
Mwingi wa Rehema! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hapana mungu isipo kuwa
Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndio marejeo yangu!
31. Na kama ingeli kuwako Qur'ani ndiyo inayo endeshewa milima, na
kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (basi ingeli kuwa Qur'ani hii). Bali
mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua walio amini kwamba lau kuwa
Mwenyezi Mungu ange penda bila ya shaka angeli waongoa watu wote? Wala walio
kufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyo yatenda, au ikawateremkia karibu
na nyumbani kwao, mpaka ifike ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
havunji miadi yake.
32. Na hakika walifanyiwa kejeli Mitume walio kuwa kabla yako. Na
nikawapururia wale walio kufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu
yangu!
33. Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo yachuma...? Na
wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au ndio mnampa
khabari ya yale asiyo yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali walio
kufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi Mungu
amemwacha apotee basi hana wa kumwongoa.
34. Wanayo adhabu katika maisha ya dunia, na adhabu ya Akhera hapana
shaka ina mashaka zaidi. Na wala hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi
Mungu.
35. Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake inapita
mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale
walio walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
36. Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa. Na katika
makundi mengine wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa nimuabudu
Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo ninaita, na
kwake Yeye ndio marejeo yangu.
37. Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni hukumu kwa lugha
ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na
rafiki wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
38. Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na
tukajaalia wawe na wake na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo
kuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake.
39. Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo. Na asili ya hukumu
zote iko kwake.
40. Na ikiwa tukikuonyesha baadhi ya tuliyo waahidi au tukakufisha
kabla yake, juu yako wewe ni kufikisha ujumbe na juu yetu ni hisabu.
41. Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza nchani mwake?
Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake, naye ni Mwepesi
wa kuhisabu.
42. Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye mipango yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na makafiri watajua ni
ya nani nyumba ya mwisho Akhera!
43. Na walio kufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu
anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye ilimu ya
Kitabu.
14 - IBRAHIM
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Alif Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako
ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao
Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa,
2. Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote viliomo katika
mbingu na ardhi. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali!
3. Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na
wanawazuilia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao
wamepotelea mbali.
4. Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate
kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa
amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
5. Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe
watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za
Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri
akashukuru.
6. Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu
aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio kupeni
adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha hai wanawake.
Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu Mlezi.
7. Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni;
na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
8. Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani,
hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.
9. Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu,
na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi
Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao
kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa, na
hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
10. Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba
mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni
muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu
kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi
tuleteeni hoja ilio wazi.
11. Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni wanaadamu
kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika waja wake.
Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu
ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini.
12. Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye
ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo maudhi mnayo
tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
13. Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi
yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika
tutawaangamiza walio dhulumu!
14. Na tutakuwekeni katika ardhi baada
15. Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari mkaidi,
16. Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanywishwa maji ya
usaha.
17. Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe yanamjia
kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine kali
vile vile.
18. Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni kama
jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi
kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali!
19. Huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki?
Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya!
20. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu.
21. Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge
watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei
kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu
angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu
tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.
22. Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu
alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na
sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi
msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala
nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani
kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu
chungu.
23. Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani
yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio yao
humo yatakuwa: Salaam!
24. Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano wa neno zuri?
Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni.
25. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na
Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
26. Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya
ardhi. Hauna imara.
27. Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara
katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao
wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
28. Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa
kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo?
29. Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo!
30. Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze watu kwenye
Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni!
31. Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na watoe katika
tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa na
biashara wala urafiki.
32. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na
akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki
yenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na
akaifanya mito ikutumikieni.
33. Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu, na
akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu.
34. Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema za Mwenyezi
Mungu hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye
kuzikufuru neema.
35. Na Ibrahim alipo sema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ujaalie mji huu uwe
wa amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.
36. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi
aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.
37. Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu
katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola wetu
Mlezi, ili washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku
matunda, ili wapata kushukuru.
38. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo yaficha na tunayo
yatangaza. Na hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi
wala katika mbingu.
39. Alhamdulillahi! Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu aliye nipa juu
ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusikia
maombi.
40. Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika
dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu.
41. Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na
Waumini, siku ya kusimama hisabu.
42. Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayo yafanya
madhaalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka macho
yao.
43. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao
tupu.
44. Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu waseme:
Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate
Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?
45. Na mkakaa katika maskani zile zile za walio zidhulumu nafsi zao.
Na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo watendea. Nasi tukakupigieni mifano
mingi.
46. Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao anavijua
Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.
47. Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi
yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, na ni Mwenye
kulipiza.
48. Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu pia. Nao
watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu.
49. Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo;
50. 50 Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso zao.
51. Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyo yachuma.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
52. Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa
hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.