Part 17
21 - AL - ANBIYAA
KWA JINA
LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza.
2. Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa
Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo.
3. Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu
4. Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika
ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
5. Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua
tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza
6. Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je,
wataamini hawa?
7. Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi
(ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui.
8. Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye
kuishi milele.
9. Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na
tukawateketeza walio pita mipaka.
10. Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo
makumbusho yenu. Je! Hamzingatii?
11. Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na
tukawasimamisha baada yao watu wengine.
12. Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia.
13. Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani
zenu, mpate kusailiwa!
14. Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu.
15. Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio
fyekwa, wamezimika.
16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa
mchezo.
17. Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe,
lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo.
18. Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka.
Na ole wenu kwa mnayo yazua.
19. Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika
ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.
20. Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei.
21. Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua?
22. Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu
basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika
Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.
23. Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa
wayatendayo.
24. Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi
wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu.
Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza.
25. Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya
kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
26. Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu,
Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa.
27. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake.
28. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei
yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa
wananyenyekea.
29. Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake,
basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye
kudhulumu.
30. Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa
zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho
hai? Basi je, hawaamini?
31. Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe,
na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka.
32. Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini
wanazipuuza Ishara zake.
33. Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote
katika anga vinaogelea.
34. Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha
ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele?
35. Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari
na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.
36. Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha
maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao
wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema!
37. Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu.
Basi msinihimize.
38. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema
kweli?
39. Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto
kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa!
40. Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza
kuurudisha, wala hawatapewa muhula!
41. Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale
walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka.
42. Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi
wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi.
43. Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi
kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi!
44. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu
kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi
je! Hao ni wenye kushinda?
45. Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo
onywa.
46. Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola
wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye
kudhulumu.
47. Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi
haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali
tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.
48. Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza,
na makumbusho kwa wachamngu,
49. Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya
Kiyama.
50. Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi
je! Mnayakataa?
51. Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na
tulikuwa tunamjua.
52. Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu
mnayo yashughulikia kuyaabudu?
53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
54. Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika
upotofu ulio dhaahiri.
55. Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika
wachezao tu?
56. Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi
ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
57. Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya
mkisha geuka kwenda zenu.
58. Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao
walirudie.
59. Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni
katika walio dhulumu.
60. Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa
Ibrahim.
61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate
kumshuhudia!
62. Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe
Ibrahim?
63. Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni
ikiwa wanaweza kutamka.
64. Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa
madhaalimu!
65. Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua
kwamba hawa hawesemi.
66. Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio
kufaini kitu wala kukudhuruni?
67. Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi
Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?
68. Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi
ni watendao jambo!
69. Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
70. Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio
khasiri.
71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio
ibariki kwa ajili ya walimwengu wote.
72. Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote
tukawajaalia wawe watu wema.
73. Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na
tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa
wanatuabudu Sisi tu.
74. Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio
kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu.
75. Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa
watenda mema.
76. Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye
na watu wake kutokana na shida kubwa.
77. Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao
walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote.
78. Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde
walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu
yao hiyo.
79. Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na
ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na
imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo.
80. Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili
yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru?
81. Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri
yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu.
82. Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo.
Na Sisi tulikuwa walinzi wao.
83. Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata
madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu.
84. Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na
tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na
ukumbusho kwa wafanyao ibada.
85. Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa
wanao subiri.
86. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika
watu wema.
87. Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya
kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu
isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa
wenye kudhulumu.
88. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo
ndivyo tunavyo waokoa Waumini.
89. Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi!
Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi.
90. Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe.
Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu.
Nao walikuwa wakitunyenyekea.
91. Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho
yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu.
92. Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu
Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.
93. Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote
watarudi kwetu.
94. Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake.
Na hakika Sisi tunamwandikia.
95. Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba
hawatarejea,
96. Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka
kila mlima;
97. Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya
walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na
haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
98. Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni
kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu.
99. Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu
humo.
100. Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia
(jenginelo).
101. Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na
hayo.
102. Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo
yatamani nafsi zao.
103. Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea
(kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa!
104. Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu.
Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu.
Hakika Sisi ni watendao.
105. Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu,
ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.
106. Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.
107. Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.
108. Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni
Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu?
109. Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala
sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa.
110. Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo.
111. Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda
kidogo.
112. Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni
Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua.
22 - AL -HAJJ
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko la Saa (ya
Kiyama) ni jambo kuu.
2. Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau
amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu
wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
3. Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu
bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet'ani aliye asi.
4. Ameandikiwa kwamba anaye mfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika
atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali.
5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika
Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana
na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo
na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya
uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto
mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo
katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui
kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo
yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea
mizuri.
6. Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba
hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila
kitu.
7. Na kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba
hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.
8. Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya
ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
9. Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya
Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu
ya kuungua.
10. (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako.
Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja.
11. Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni.
Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake.
Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.
12. Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho mdhuru wala
kumnufaisha. Huko ndiko kupotolea mbali!
13. Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi
kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu.
14. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema
katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda
atakayo.
15. Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika
dunia na Akhera na afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila yake
itaondoa hayo yaliyo mkasirisha?
16. Na namna hivi tumeiteremsha (Qur'ani) kuwa ni Aya zilizo wazi,
na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye.
17. Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo
na Majusi na wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao
Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
18. Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na
viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na
wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye
fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda
apendayo.
19. Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi.
Basi walio kufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao
maji yanayo chemka.
20. Kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao
pia.
21. Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma.
22. Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa
humo humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuungua!
23. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema
katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya
mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri.
24. Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa kwenye Njia
ya Msifiwa.
25. Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu na
Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao
humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi
tutamwonjesha adhabu chungu.
26. Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia:
Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanao
izunguka kwa kut'ufu, na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanao
sujudu.
27. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila
ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.
28. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu
katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na
mlisheni mwenye shida aliye fakiri.
29. Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao, na
waizunguke Nyumba ya Kale.
30. Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya Mwenyezi Mungu
basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na mmehalalishiwa nyama
hoa ila wale mlio somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni
na usemi wa uwongo.
31. Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha. Na
anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni,
kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali.
32. Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni
katika unyenyekevu wa nyoyo.
33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha pahala
pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale.
34. Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili
walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika wanyama wa
mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake tu, na
wabashirie wanyenyekevu,
35. Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanao
vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa katika tulivyo
waruzuku.
36. Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo
kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi
Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na
walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi tumewafanya hawa
wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
37. Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini
unamfikia uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze
Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema.
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika Mwenyezi
Mungu hampendi kila khaini mwingi wa kukanya mema.
39. Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu
wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia -
40. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa
wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu
hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na
makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu
linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye
msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.
41. Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na
wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu
ndio marejeo ya mambo yote.
42. Na wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao watu wa Nuhu,
na kina A'ad na kina Thamud,
43. Na watu wa Ibrahim na watu wa Lut'i
44. Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa. Nikawapa muda
makafiri, kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu!
45. Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu, ikawa imebaki
magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti?
46. Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za
kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka,
lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.
47. Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda
kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama
miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi.
48. Na miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, na
kisha nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndio marudio yote.
49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu niliye
dhaahiri.
50. Basi walio amini na wakatenda mema watapata maghfira na riziki
za ukarimu.
51. Na wanao jitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa
Motoni.
52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anapo soma,
Shet'ani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayo yatia
Shet'ani; kisha Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye hikima.
53. Hayo ni ili alifanye lile analo litia Shet'ani liwe ni fitna kwa
wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni ngumu. Na
hakika madhaalimu wamo katika mfarakano wa mbali.
54. Na ili walio pewa ilimu wajue kuwa hayo ni Haki itokayo kwa Mola
wako Mlezi na waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu
ndiye anaye waongoa wenye kuamini kwenye Njia Iliyo Nyooka.
55. Na walio kufuru hawatoacha kuwa katika wasiwasi kwa hilo mpaka
Saa iwafikie ghafla, au iwafikie adhabu ya Siku Tasa.
56. Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina
57. Na walio kufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi hao watapata
adhabu ya kufedhehesha.
58. Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au
wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao ruzuku.
59. BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapo paridhia. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
60. Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo adhibiwa, kisha
akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Msamehevu Mwenye maghfira.
61. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na
huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia
Mwenye kuona.
62. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale
wanao waomba badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye Juu
na ndiye Mkubwa.
63. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni,
na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole na Mwenye
kujua.
64. Ni vyake viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Mwenye kusifiwa.
65. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo
katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu
zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
huruma kwa watu, Mwenye kurehemu.
66. Na Yeye ndiye aliye kuhuisheni kisha akakufisheni, na kisha
atakufufueni. Hakika mwanaadamu hana fadhila.
67. Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika. Basi
wasizozane nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi.
Hakika wewe uko kwenye Uwongofu Ulio Nyooka.
68. Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayo
yatenda.
69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama katika hayo
mnayo khitalifiana.
70. Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na
katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni
mepesi.
71. Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia
ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhaalimu hawatakuwa na wa
kuwasaidia.
72. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso
za walio kufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya zetu. Sema:
Je! Nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi Mungu
amewaahidi walio kufuru, na ni marudio mabaya hayo.
73. Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao
waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa
74. Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kuadhimishwa.
Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda.
75. Mwenyezi Mungu huteuwa Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni
mwa watu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
76. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Na kwa Mwenyezi
Mungu yatarejeshwa mambo yote.
77. Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu
Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.
78. Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo
stahiki jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito
katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu)
alikuiteni Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume
shahidi juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni
Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora
kabisa, na Msaidizi bora kabisa.