Part 18
23 - AL - MUUMINUN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. HAKIKA wamefanikiwa Waumini,
2. Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,
3. Na ambao hujiepusha na mambo ya
upuuzi,
4. Na ambao wanatoa Zaka,
5. Na ambao wanazilinda tupu zao,
6. Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo
wamiliki mikono
7. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao
mipaka.
8. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
9. Na ambao Sala zao wanazihifadhi -
10. Hao ndio warithi,
11. Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo.
12. Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.
13. Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio
madhubuti.
14. Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa
pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa
tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi
Mungu Mbora wa waumbaji.
15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa.
16. Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa.
17. Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye
kughafilika na viumbe.
18. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza
katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa.
19. Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu,
mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula;
20. Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa
kitoweo kwa walao.
21. Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa -
tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika
hao manufaa mengi, na pia mnawala.
22. Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa.
23. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu
wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye. Basi je!
Hamwogopi?
24. Walisema wale wakuu walio kufuru katika watu wake: Huyu si
chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya
kwa baba zetu wa zamani.
25. Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa
muda.
26. Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa
wamenikanusha.
27. Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu!
Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila
namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake
imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya
shaka watazamishwa.
28. Basi utakapo tulia wewe na walio pamoja nawe humo marikebuni,
sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliye tuokoa na watu
madhaalimu!
29. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na
Wewe ni Mbora wa wateremshaji.
30. Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini Sisi ni wenye
kuwafanyia mtihani.
31. Kisha baada yao tukaanzisha kizazi kingine.
32. Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi
Mungu! Hamna mungu asiye kuwa Yeye. Jee, hamwogopi?
33. Na wakubwa katika watu wake walio kufuru na wakakanusha mkutano
wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu
si chochote ila ni binaadamu kama nyinyi; anakula mlacho, na anakunywa
mnywacho.
34. Na nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa
khasarani.
35. Hivyo anakuahidini ati ya kwamba mtakapo kufa na mkawa udongo na
mifupa kuwa mtatolewa?
36. Hayawi! Hayawi hayo mnayo ahidiwa.
37. Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na kuishi basi.
Wala sisi hatutafufuliwa.
38. Huyu si lolote ila ni mtu anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo,
wala sisi sio wa kumuamini.
39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa sababu
wananikanusha.
40. (Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache watakuwa wenye
kujuta.
41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kama takataka
zinazo elea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu!
42. Kisha tukaleta baada
43. Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
44. Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja. Kila umma
alipo wafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya hawa, na
tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Wakapotelea mbali watu wasio amini.
45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na ishara zetu
na hoja zilizo wazi.
46. Kumwendea Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna, nao walikuwa
watu majeuri.
47. Wakasema: Je, tuwaamini wanaadamu wawili hawa kama sisi, na
ambao watu wao ni watumwa wetu?
48. Basi wakawakanusha, na wakawa miongoni mwa walio angamizwa.
49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
50. Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni Ishara, na
tukawapa makimbilio kwenda mahali palipo inuka penye utulivu na chemchem za maji.
51. Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi
ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
52. Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu
Mlezi, basi nicheni Mimi.
53. Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali. Kila kundi
likifurahia kwa waliyo nayo.
54. Basi waache katika ghafla yao kwa muda.
55. Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyo wapa mali na watoto
56. Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe hawatambui.
57. Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi
wananyenyekea,
58. Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini,
59. Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi,
60. Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa
kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi,
61. Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio
watakao tangulia kuyafikia.
62. Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na tunacho
kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa.
63. Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo
vinginevyo wanavyo vifanya.
64. Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio dekezwa kwa starehe
kati yao, hapo ndipo watapo yayatika.
65. Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
66. Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi nyuma juu ya
visigino vyenu,
67. Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa
dharau.
68. Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo wafikia baba zao wa
zamani?
69. Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?
70. Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na wengi wao
wanaichukia Haki.
71. Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli
haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao
wanajitenga mbali na ukumbusho wao.
72. Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na
Yeye ndiye Mbora wa wanao ruzuku.
73. Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka.
74. Na hakika wale wasio iamini Akhera wanajitenga na Njia
hiyo.
75. Na lau tungeli warehemu na tukawaondolea shida waliyo nayo bila
ya shaka wangeli endelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga.
76. Na hakika tuliwatia adhabu kali; lakini hawakuelekea kwa Mola
wao Mlezi wala hawakunyenyekea.
77. Mpaka tulipo wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa
wenye kukata tamaa.
78. Na Yeye ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na nyoyo za
kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu.
79. Na Yeye ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye
mtakusanywa.
80. Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko
ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?
81. Bali wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza.
82. Walisema: Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa ndio
tutafufuliwa?
83. Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni
visa vya uwongo vya watu wa zamani.
84. Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama nyinyi
mnajua?
85. Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je,
hamkumbuki?
86. Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi
Kuu?
87. Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, hamwogopi?
88. Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye
anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua?
89. Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi vipi
mnadanganyika?
90. Bali tumewaletea Haki, na kwa yakini hao ni waongo.
91. Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hanaye mungu mwengine.
Inge kuwa hivyo basi kila mungu angeli chukua alivyo umba, na baadhi yao
wangeli washinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazo msifu.
92. Mjuzi wa siri na dhaahiri, na ametukuka juu ya hayo wanayo
mshirikisha nayo.
93. Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha adhabu waliyo ahidiwa,
94. Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu madhaalimu hao.
95. Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyeshsa tuliyo waahidi.
96. Kinga maovu kwa kutenda yaliyo mema zaidi. Sisi tunajua
wayasemayo.
97. Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi wa
mashet'ani.
98. Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie.
99. Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi!
Nirudishe.
100. Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni
kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo
fufuliwa.
101. Basi litapo pulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao
siku hiyo, wala hawataulizana.
102. Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye
kufanikiwa.
103. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia
khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu.
104. Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizo
kunjana.
105. Je! Hazikuwa Aya zangu mkisomewa, na nyinyi mkizikanusha?
106. Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio
potea.
107. Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli
sisi ni wenye kudhulumu.
108. Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeze.
109. Bila ya shaka lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola
wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanao
rehemu.
110. Lakini nyinyi mliwakejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka,
na mlikuwa mkiwacheka.
111. Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyo subiri. Bila ya
shaka hao ndio wenye kufuzu.
112. Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka?
113. Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize
wanao weka hisabu.
114. Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli
kuwa mnajua.
115. Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi
kwetu hamtarudishwa?
116. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye,
Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu.
117. Na anaye muomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe
hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi.
Kwa hakika makafiri hawafanikiwi.
118. Nawe sema: Mola wangu Mlezi! Samehe na urehemu nawe ni Mbora wa
wanao rehemu.
24 - AN - NUR
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. HII NI SURA Tuliyo iteremsha na tukailazimisha; tukateremsha
ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.
2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja
katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya
Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na
lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.
3. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke
mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina.
Na hayo yameharimishwa kwa Waumini.
4. Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi
wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na
hao ndio wapotovu.
5. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani
bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
6. Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi
zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha
Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
7. Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake
ikiwa ni miongoni mwa waongo.
8. Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo
cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo.
9. Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu
yake kama mumewe yu miongoni mwa wanao sema kweli.
10. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema
yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba....
11. Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri
ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo
yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao,
atapata adhabu kubwa.
12. Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake
Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
13. Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta
mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
14. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake
katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu
ya yale mliyo jiingiza.
15. Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo
yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa.
16. Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya.
Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!
17. Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya
kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!
18. Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye hikima.
19. Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini,
watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na
nyinyi hamjui.
20. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema
yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu....
21. Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata
nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila
ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu
kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
22. Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa
jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na
waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
23. Hakika wanao wasingizia wanawake, wanao jihishimu, walio
ghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu kubwa.
24. Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao
kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
25. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki,
na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi.
26. Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa
wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa
wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na
riziki ya ukarimu.
27. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe
ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka.
28. Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na
mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu
anajua mnayo yatenda.
29. Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisio kaliwa ambazo ndani yake
yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yadhihirisha na mnayo
yaficha.
30. Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu
zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayo
yafanya.
31. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde
tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe
shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au
baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka
zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo
wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto
ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili
yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi
Waumini, ili mpate kufanikiwa.
32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na
wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.
33. Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka
Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru
katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama
mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala
msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la
maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi
Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
34. Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na mifano
kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu.
35. Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni
kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile
ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti
ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta
yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu
humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
36. Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na
humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni
37. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru
Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na
macho yatageuka.
38. Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo yatenda, na
awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya
hisabu.
39. Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani.
Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta
Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwepesi wa kuhisabu.
40. Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu
ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake
anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na
nuru.
41. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika
mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala
yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua
wayatendayo.
42. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi
Mungu ndio marejeo ya wote.
43. Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha
huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na
huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo
amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua
macho.
44. Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo
yapo mazingatio kwa wenye kuona.
45. Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine
katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na
wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu.
46. Kwa yakini tumeteremsha Ishara zinazo bainisha. Na Mwenyezi Mungu
hummwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
47. Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tumet'ii.
Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini.
48. Na wanapo itwa kumuendea Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili
ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa.
49. Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kut'ii.
50. Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au
wanaogopa ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali hao ndio
madhaalimu.
51. Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume
wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio
wenye kufanikiwa.
52. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa
Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.
53. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba
ukiwaamrisha kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
54. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka,
basi yaliyo juu yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa
nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe
wazi wazi.
55. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na
wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya
makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo
wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi,
wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio
wapotovu.
56. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate
kurehemewa.
57. Msiwadhanie walio kufuru kwamba watashinda katika nchi. Na
makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo yao.
58. Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu
ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya
alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha.
Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya
nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu
anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
59. Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake
ruhusa, kama walivyo taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo
kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye
hikima.
60. Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza
nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
61. Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya
kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba
zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu,
au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu,
au nyumba za dada wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu.
Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba,
toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka
na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate
kuelewa.
62. Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume
wake; na wanapo kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka
wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu
umtakaye miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu.
63. Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa
nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho.
Basi nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata
adhabu chungu.
64. Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na
ardhini. Hakika Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza
waliyo yafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
25 - AL - FURQAN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji
kwa walimwengu wote.
2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana,
wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa
kipimo.
3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali
hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki
mauti, wala uhai, wala kufufuka.
4. Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio
uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na
uwongo.
5. Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha,
anavyo somewa asubuhi na jioni.
6. Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi.
Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea
masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?
8. Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika
hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa.
9. Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala
hawataiweza Njia.
10. Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo,
nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya
fakhari.
11. Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto
mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa..
12. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake
na mngurumo wake.
13. Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba
wafe.
14. Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!
15. Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa
wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?
16. Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya
Mola wako Mlezi, inayo ombwa.
17. Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema:
Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea
njia?
18. Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi
kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao
hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia.
19. Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi
kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha
adhabu kubwa.
20. Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na
yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi
yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye
kuona.