Part 21
46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri
kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo
teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni
Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.
47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale
tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa
(washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa
makafiri.
48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala
hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka
wavunjifu.
49.
50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake
Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji
mwenye kubainisha tu.
51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki
wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao
amini.
52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi.
Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na
wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri.
53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana
wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa
ghafla, na hali wao hawana khabari.
54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa
hakika imewazunguka makafiri!
55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu
yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda!
56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa.
Basi niabuduni Mimi peke yangu.
57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu.
58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka
katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni
mwema ulioje huo ujira wa watendao,
59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi
Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye
kujua.
61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua
na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi
wanako geuzwa?
62. Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye
katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
63. Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na
akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi
Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi
katika wao hawafahamu.
64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na
nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua!
65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa
kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara
wanamshirikisha.
66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja
jua!
67. Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na
hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu,
na neema za Mwenyezi Mungu wanazikataa?
68. Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi
Mungu au anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa
makaazi ya makafiri?
69. Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye
njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.
30 - AR-RUM
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Alif Lam Mim (A.L.M.)
2. Warumi wameshindwa,
3. Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao
watashinda
4. Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na
baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi.
5. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye
Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
6. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.
Lakini watu wengi hawajui.
7. Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na
Akhera.
8. Je! Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na
ardhi na viliomo ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu
wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.
9. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio
kuwa kabla
10. Kisha ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara
za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara.
11. Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili,
na kisha mtarejeshwa kwake.
12. Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa.
13. Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa
wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa
wao.
14. Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika.
15. Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika
Bustani.
16. Na ama walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa
Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu.
17. Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na
asubuhi,
18. Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na
adhuhuri.
19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho
kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama
hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa.
20. Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha
mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote.
21. Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na
nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu.
Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
22. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana
ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi.
23. Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na
kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa
watu wanao sikia.
24. Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na
tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi
baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
zingatia.
25. Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa
amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye
ardhi.
26. Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii
Yeye.
27. Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara
nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora
katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
28. Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo
wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni,
mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo ogopana wenyewe
kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili.
29. Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua.
Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao
hawatakuwa na wa kuwanusuru.
30. Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la
Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi
Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.
31. Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na
wala msiwe katika washirikina.
32. Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa
makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho.
33. Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao wametubu
kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao
humshirikisha Mola wao Mlezi,
34. Kwa kuyakataa tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua!
35. Au tumewateremshia hoja ambayo kwayo ndio wanafanya
ushirikina?
36. Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na ukiwasibu uovu
kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.
37. Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye
na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
amini.
38. Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni kheri
kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa.
39. Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu,
basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa
kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa.
40. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha akakuruzukuni, kisha
anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote katika hao mnao
washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika, na
ametukuka na hayo mnayo mshirikisha naye.
41. Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya
watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea
kwa kutubu.
42. Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa walio
tangulia. Wengi wao walikuwa washirikina.
43. Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika
Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu
watatengana.
44. Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na
anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao.
45. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na fadhila
yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri.
46. Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema,
na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa amri
yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru.
47. Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na wakawajia
kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya ukosefu. Na ilikuwa ni haki
juu yetu kuwanusuru Waumini.
48. Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua mawingu,
kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi
ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika waja wake,
mara hao huwa na furaha.
49. Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata
tamaa.
50. Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyo
ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya shaka Mwenye
kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
51. Na tunge utuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu
ya hayo wange endelea kukufuru.
52. Kwani wewe hakika huwafanyi maiti wakasikia, wala viziwi
wakasikia wito wakisha geuka kukupa mgongo.
53. Wala wewe huwaongoi vipofu na upotovu wao. Huwasikilizishi ila
wanao ziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walio nyenyekea.
54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha
akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena
na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.
55. Na siku itapo simama Saa wakosefu wataapa kwamba hawakukaa
duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyo kuwa wakipotozwa.
56. Na walio pewa ilimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwisha
kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo
Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamuijui.
57. Basi Siku hiyo hautawafaa walio dhulumu udhuru wao, wala
haitotakiwa toba yao.
58. Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur'ani.
Na ukiwaletea Ishara yoyote hapana shaka walio kufuru watasema: Nyinyi si
chochote ila ni waongo.
59. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga muhuri kwenye nyoyo za
wasio jua.
60. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala
wasikupaparishe hao wasio kuwa na yakini.
31 - LUQMAN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Alif Lam Mim (A.L.M.)
2. Hizi ni Aya za Kitabu chenye hikima.
3. Kuwa ni Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema,
4. Wanao shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na
Akhera.
5. Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao
ndio wenye kufanikiwa.
6. Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili
wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni
maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha.
7. Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna,
kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie
kuwa atapata adhabu chungu.
8. Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa nazo Bustani za
neema.
9. Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye
ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
10. Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika
ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya
wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea
mizuri ya kila namna.
11. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini
hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri.
12. Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye
kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.
13. Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe
mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka
ni dhulma iliyo kubwa.
14. Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua
mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka
miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo
marudio.
15. Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu
nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya
anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni
mliyo kuwa mkiyatenda.
16. Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali
kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi
Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye
khabari za yote.
17. Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na
subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa..
18. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo.
Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha.
19. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika
katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda.
20. Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni
viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na
za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo
ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
21. Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu,
husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani
anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao?
22. Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa
anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na
mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu.
23. Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio
yao, na hapo tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa
yaliyomo vifuani.
24. Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma kwenye adhabu
ngumu.
25. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka
watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za
Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
26. Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi.
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
27. Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari
(ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi
Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
28. Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi
moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
29. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana,
na huuingiza mchana katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi? Vyote hivyo
vinakwenda mpaka wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo
yatenda.
30. Hivi ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na
hakika wanacho kiomba ni cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye
Mtukufu na ndiye Mkubwa.
31. Kwani huoni kwamba marikebu hupita baharini zikichukua neema za
Mwenyezi Mungu, ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya
zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.
32. Na wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba Mwenyezi Mungu
kwa kumsafia dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao
huenda mwendo wa sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri
mkubwa.
33. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi
hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi
Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni
na Mwenyezi Mungu mdanganyifu.
34. Hakika kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye
ndiye anaye iteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na
haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi
gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.
32 - ASSAJDAH
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Alif Lam Mim (A.L.M.)
2. Huu ni mteremsho wa Kitabu kisicho kuwa na shaka yoyote kinacho
toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
3. Au wanasema: Amekizua? Bali hichi ni Kweli iliyo toka kwa Mola wako
Mlezi ili uwaonye watu wasio fikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda
wakaongoka.
4. Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba mbingu na ardhi na viliomo baina
yao kwa siku sita, na akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala
mwombezi isipo kuwa Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki?
5. Anapitisha mambo yote yalio baina mbingu na ardhi, kisha
yanapanda kwake kwa siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyo hisabu
nyinyi.
6. Huyu ndiye Mwenye kuyajua yasiyo onekana na yanayo onekana.
Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
7. Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha
kumuumba mtu kwa udongo.
8. Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji
madhaifu.
9. Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni
kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru.
10. Nao husema: Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli
tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola
wao Mlezi.
11. Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu;
kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi.
12. Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya
Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia.
Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini
sasa.
13. Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini
imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu : Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa
wote hawa, majini na watu.
14. Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na
Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa
mkiyatenda.
15. Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa
hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi,
nao hawajivuni.
16. Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa
khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku.
17. Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha
macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.
18. Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi
sawa.
19. Ama walio amini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za
makaazi mazuri. Ndio pa kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
20. Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni Motoni. Kila
wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya
Moto ambayo mliyo kuwa mkiikanusha.
21. Na tutawaonjesha adhabu khafifu kabla ya adhabu kubwa, huenda
labda watarejea.
22. Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa kwa
Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi tutajilipiza kwa
wakosefu.
23. Hakika Sisi tulikwisha mpa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka kuwa
kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili.
24. Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri
yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu.
25. Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye fafanua baina
26. Je! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao,
nao wanapita katika maskani zao hizo? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je,
hawasikii?
27. Je! Hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha
kwayo tunaitoa mimea wanayo kula wanyama wao na wao wenyewe? Je! Hawaoni?
28. Wanasema: Ushindi huu ni lini, kama mnasema kweli?
29. Sema: Siku ya Ushindi, wale walio kufuru imani yao haitawafaa
kitu, wala wao hawatapewa muhula.
30. Basi wapuuze, nawe ngonja; hakika wao wanangoja.
33 - AL-AH'ZAB
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat'ii makafiri na
wanaafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
2. Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi.
Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.
3. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni
wa kutegemewa.
4. Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani
ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao
na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa
kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi
Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia.
5. Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya
Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na
rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika
yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
6. Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake
ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu
kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu.
Haya yamekwisha andikwa Kitabuni.
7. Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na
Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu,
8.
9. Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu
yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi
msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
10. Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho
yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana
mbali mbali.
11. Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa mtikiso
mkali.
12. Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao:
Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu.
13. Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa
Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba
ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu;
hawakutaka ila kukimbia tu.
14. Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa
kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu.
15. Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba
hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.
16. Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au
kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu.
17. Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi
akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi
isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao
waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.
19. Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na
macho yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na
khofu ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la
kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao. Na
hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
20. Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo
makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza
khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu.
21. Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa
anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu
sana.
22. Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo
tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema
kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu.
23. Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na
Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala
hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.
24. Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na
awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
25. Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu
yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika
vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza.
26. Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa
Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao
mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka.
27. Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi
msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
28. Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na
pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano
mzuri.
29. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya
Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo
makubwa.
30. Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni
mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni
mepesi.