Part 22
31. NA MIONGONI mwenu atakeye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara
mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu.
32. Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si
33. Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya
kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa
Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara.
34. Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi
Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na Mwenye
khabari.
35. Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume
na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli
wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu
wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga
wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao
mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu
amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.
36. Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari
katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao.
Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu
ulio wazi.
37. Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe
ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini
mwako aliyo taka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja
naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa
kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya
Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.
38. Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia Mwenyezi Mungu.
Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na amri ya Mwenyezi
Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa.
39. (Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha risala za Mwenyezi Mungu
na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu.
40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa
Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila
kitu.
41. Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa
kumdhukuru. .
42. Na mtakaseni asubuhi na jioni.
43. Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani
mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.
44. Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Salama! Na
amewaandalia malipo ya ukarimu.
45. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na
mwonyaji,
46. Na mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa
yenye kutoa nuru.
47. Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayo toka
kwa Mwenyezi Mungu.
48. Wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe
mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.
49. Enyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa
t'alaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi wapeni
cha kuwaliwaza, na muwawache kwa kuwachana kwa wema.
50. Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na
ulio wamiliki kwa mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na
mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na
mabinti wa dada za mama yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini
akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumwoa. Ni halali
kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyo wafaridhia wao
katika wake zao na wanawake ilio wamiliki mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki
kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
51. Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze umtakaye.
Na kama ukimtaka yule uliye mtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya hivi
kutapelekea yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile
unacho wapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu, na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
52. Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala
kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipo kuwa yule
uliye mmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila
kitu.
53. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa
kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha
kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye
anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza
wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu
na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa
wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi
Mungu.
54. Mkidhihirisha chochote kile, au mkikificha, basi hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
55. Hapana ubaya kwao (wake za Mtume) kuonana na baba zao, wala
watoto wao, wala ndugu zao, wala watoto wa ndugu zao wanaume, wala watoto wa
ndugu zao wanawake, wala wanawake wenzao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao
ya kulia. Na enyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kushuhudia kila kitu.
56. Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio
amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu.
57. Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu
amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehi.
58. Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao
kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio
dhaahiri.
59. Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini
wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
60. Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao
fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha
hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.
61. Wamelaanika! Popote watakapo onekana watakamatwa na watauliwa
kabisa.
62. Hii ni ada ya Mwenyezi Mungu iliyo kuwa kwa wale walio pita
zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Mwenyezi Mungu.
63. Watu wanakuuliza khabari ya Saa (ya Kiyama). Sema: Ujuzi wake
uko kwa Mwenyezi Mungu. Na nini kitakujuvya? Pengine hiyo Saa iko karibu.
64. Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto
unao waka kwa nguvu.
65. Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru.
66. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto.
Watasema: Laiti tungeli mt'ii Mwenyezi Mungu, na tungeli mt'ii Mtume!
67. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwat'ii bwana zetu
na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia.
68. Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana
kubwa.
69. Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio mtaabisha Musa, lakini
Mwenyezi Mungu akamtakasa na waliyo yasema, naye alikuwa mwenye hishima mbele
ya Mwenyezi Mungu.
70. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya
sawasawa.
71. Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi
yenu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa
mafanikio makubwa.
72. Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na
milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu
akaichukua. Hakika yeye amekuwa dhaalimu mjinga.
73. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu anawaadhibu wanaafiki wanaume, na
wanaafiki wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na
anawapokelea toba Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
34 - SABAA
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye ni vyake vyote
viliomo mbnguni na katika ardhi. Na sifa ni zake Yeye katika Akhera. Naye ni
Mwenye hikima, Mwenye khabari.
2. Anajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo
teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda huko. Na Yeye ni Mwenye kurehemu,
Mwenye kusamehe.
3. Na walisema walio kufuru: Haitatufikia Saa (ya Kiyama). Sema:
Kwani? Hapana shaka itakufikieni, naapa kwa haki ya Mola wangu Mlezi, Mwenye
kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichikana kwake hata chenye uzito wa chembe tu,
si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko hivyo, wala
kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu chake chenye kubainisha.
4. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema. Hao watapata msamaha
na riziki ya ukarimu.
5. Na wale walio jitahidi kuzipinga Ishara zetu wakaona watashinda,
hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
6. Na walio pewa ilimu wanaona ya kuwa ulio teremshiwa kutoka kwa
Mola wako Mlezi ni haki, nayo huongoa kwendea njia ya Mwenye nguvu, Mwenye
kusifiwa.
7. Na walio kufuru walisema: Je! Tukujuulisheni mtu anaye kuambieni
kwamba mtakapo chambuliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya?
8. Ama amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au ana wazimu. Bali wasio
amini Akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali kabisa.
9. Kwani hawaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbingu na
ardhi? Tungeli penda tungeli wadidimiza ndani ya ardhi, au tungeli wateremshia
juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mja aliye
tubia.
10. Na tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu, (tukasema): Enyi milima!
Karirini kumtakasa Mwenyezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na tukamlainishia
chuma.
11. (Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na kadiria sawa
katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema mnayo
yatenda.
12. Na Suleiman tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya asubuhi
ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na
tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio kuwa
wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anaye jitenga
na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unao waka.
13. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na masanamu, na
madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa mahala pake.
Enyi watu wa Daudi! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu
wanao shukuru.
14. Na tulipo mhukumia kufa, hapana aliye wajuulisha kufa kwake ila
mnyama wa ardhi aliye kula fimbo yake. Na alipo anguka majini walitambua lau
kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli kaa katika adhabu hiyo ya
kufedhehesha.
15. Hakika ilikuwapo Ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika
maskani yao - bustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Mwenyezi
Mungu, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu.
16. Lakini wakaacha. Tukawapelekea mafuriko makubwa, na
tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda
makali machungu, na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi.
17. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi kwani
tunamuadhibu isipo kuwa anaye kufuru?
18. Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki tuliweka miji iliyo
dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni humo usiku na
mchana kwa amani.
19. Lakini wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu baina ya
safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni masimulizi tu, na
tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo Ishara kwa kila
mwenye kusubiri sana na akashukuru.
20. Na bila ya shaka Iblisi alihakikisha ile dhana yake juu yao. Nao
walimfuata, isipo kuwa kundi la Waumini.
21. Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa sababu ya
kuwajaribu tujue nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia shaka. Na Mola
wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.
22. Sema: Waite mnao wadaia kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu.
Hawamiliki hata uzito wa chembe hichi katika mbingu wala ardhi. Wala hawana
ushirika wowote humo. Wala Yeye hana msaidizi miongoni mwao.
23. Wala uombezi mbele yake hautafaa kitu, isipo kuwa kwa aliye mpa
idhini. Hata itapo ondolewa khofu kwenye nyoyo zao watasema: Mola wenu Mlezi
kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu, Mkubwa.
24. Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi?
Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko kwenye
uwongofu au upotofu ulio wazi.
25. Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyo yafanya, wala sisi
hatutaulizwa kwa mnayo yatenda nyinyi.
26. Sema: Mola wetu Mlezi atatukusanya, kisha atatuhukumu kwa haki;
na Yeye ndiye Hakimu Mwenye kujua.
27. Sema: Nionyesheni mlio waunganisha naye kuwa washirika. Hasha!
Bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
28. Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji.
Lakini watu wengi hawajui.
29. Na wanasema: Ahadi hii itakuwa lini, ikiwa nyinyi mnasema
kweli?
30. Sema: Nyinyi mnayo miadi ya Siku ambayo hamtaakhirika nayo kwa
saa moja, wala hamtaitangulia.
31. Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii, wala yaliyo
kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele ya Mola wao
Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia walio takabari:
Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi.
32. Walio takabari watawaambia wanyonge: Kwani sisi ndio tulio
kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ni wakosefu.
33. Na wanyonge wakawaambia walio takabari: Bali ni vitimbi vyenu
vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu, na
tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na tutaweka
makongwa shingoni mwao walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo kuwa
wakiyatenda?
34. Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji, ila walisema walio
jidekeza kwa starehe zao wa mji huo: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyo tumwa
nayo.
35. Na wakasema: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto, wala sisi
hatutaadhibiwa.
36. Sema: Hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha
amtakaye. Lakini watu wengi hawajui.
37. Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni kwetu
muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo
mardufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.
38. Na wanao jitahidi kuzipinga Ishara zetu, wakaona watashinda, hao
watahudhurishwa kwenye adhabu.
39. Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na
humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakacho kitoa Yeye
atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.
40. Na siku atakayo wakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je!
Hawa walikuwa wakikuabuduni?
41. Waseme: Subhanak, Umetakasika. Wewe ndiye kipenzi chetu si hao.
Bali wao walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.
42. Hii leo hataweza yeyote kumletea nafuu wala madhara mwenzie. Na
tutawaambia walio dhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mlio kuwa mkiukanusha.
43. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote
ila ni mtu anaye taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu. Na
wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru
waliiambia Haki ilipo wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri.
44. Wala hatukuwapa Vitabu wavisome, wala hatukuwatumia Mwonyaji
kabla yako wewe.
45. Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na hawakufikilia hata
sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao waliwakadhibisha Mitume wangu.
Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani!
46. Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa
ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu
huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu
kali.
47. Sema: Ujira nilio kuombeni ni wenu nyinyi. Sina ujira ila kwa
Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu.
48. Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anaondoa upotovu kwa Haki. Yeye
ndiye Mwenye kujua vyema yaliyo ghaibu.
49. Sema: Kweli imefika, na uwongo haujitokezi, wala haurudi.
50. Sema: Ikiwa mimi nimepotea, basi nimepotea kwa kudhuru nafsi
yangu mwenyewe. Na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ya kunifunulia Mola
wangu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu.
51. Na lau ungeli ona watapo babaika, basi hapana pa kukimbilia! Na
watakamatwa mahala pa karibu.
52. Na watasema: Tunaiamini! Lakini wataipata wapi kutoka huko
mahala mbali?
53. Na hapo kabla yake waliikataa, na wakiyatupilia mbali maneno ya
ghaibu kutoka mahali mbali.
54. Na watatiliwa kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani, kama
walivyo fanyiwa wenzao zamani. Hakika hao walikuwa na shaka ya kutia
wasiwasi.
35 - FAAT'IR
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi,
aliye wafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu- tatu, na
nne-nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu
ya kila kitu.
2. Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia.
Na anayo izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu,
Mwenye hikima.
3. Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo
muumba mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni
na kwenye ardhi? Hapana mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?
4. Na wakikukanusha, basi walikwisha kanushwa Mitume kabla yako. Na
mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
5. Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni
maisha ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu.
6. Hakika Shet'ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani
yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni.
7. Walio kufuru watakuwa na adhabu kali; na walio amini na
wakatenda mema watapata msamaha na ujira mkubwa.
8. Je! Yule aliye pambiwa a'mali zake mbaya na akaziona ni njema -
basi hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye.
Basi nafsi yako isijihiliki kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anajua
wanayo yafanya.
9. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma Pepo ziyatimue mawingu,
nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyo kufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa
kwake. Ndivyo kama hivyo kutakavyo kuwa kufufuliwa.
10. Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu.
Kwake Yeye hupanda neno zuri, na a'mali njema Yeye huitukuza. Na wanao panga
vitimbi vya maovu watapata adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea
patupu.
11. Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha kwa tone
la manii. Kisha akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui
mimba, wala hazai, ila kwa ilimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu,
wala hapunguziwi katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni
mepesi kwa Mwenyezi Mungu.
12. Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri
kunywa. Na haya ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula
nyama mpya (isiyo chacha). Na mnatoa mapambo mnayo yavaa. Na unaona ndani yake
marikebu zinakata maji ili mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
13. Anauingiza usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika
usiku. Na amelifanya jua na mwezi kutumikia. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda
maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnao
waomba badala yake hawamiliki hata ugozi wa kokwa ya tende.
14. Mkiwaomba hawasikii maombi yenu; na hata wakisikia hawakujibuni.
Na Siku ya Kiyama watakataa ushirikina wenu. Na hapana atakaye kupa khabari
vilivyo kama Yeye Mwenye khabari.
15. Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa.
16. Akitaka atakuondoeni na alete viumbe vipya.
17. Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.
18. Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Na aliye topewa na mzigo
wake akiomba uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo, na angamwomba jamaa yake.
Hakika wewe unawaonya wale wanao mcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na wanashika
Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo
ni kwa Mwenyezi Mungu.
19. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani.
20. Wala giza na mwangaza.
21. Wala kivuli na joto.
22. Wala hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi Mungu
humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini.
23. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.
24. Hakika Sisi tumekutuma wewe kwa Haki, kuwa ni mbashiri na
mwonyaji. Na hapana umma wowote ila ulipata mwonyaji kati
25. Na wakikukanusha basi walikwisha wakanusha walio kuwa kabla
26. Kisha nikawakamata walio kufuru. Basi kuchukia kwangu
kulikuwaje?
27. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka
mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima
imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana.
28. Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao
zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake
ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
29. Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika
Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao hutaraji
biashara isiyo bwaga.
30. Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie
kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani.
31. Na hayo tuliyo kufunulia kutoka Kitabuni ni Kweli yenye
kusadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni
Mwenye khabari na Mwenye kuona.
32. Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa
waja wetu. Kati yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na
yupo aliye tangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo
ndiyo fadhila kuu.
33. Mabustani ya milele watayaingia. Huko watavikwa vikuku vya
dhahabu, na lulu, na nguo zao humo ni za hariri.
34. Na watasema: Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi
Mungu aliye tuondolea huzuni zote. Hakika Mola wetu Mlezi bila ya shaka ni
Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani.
35. Ambaye kwa fadhila yake ametuweka makao ya kukaa daima; humu
haitugusi taabu wala humu hakutugusi kuchoka.
36. Na walio kufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu, hawahukumiwi
wakafa, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila
mwenye kuzidi ukafiri.
37. Na humo watapiga makelele: Mola wetu Mlezi! Tutoe tufanye mema
sio yale tuliyo kuwa tukiyafanya. Kwani hatukukupeni umri wa kutosha kukumbuka
mwenye kukumbuka? Na akakujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani walio dhulumu
hawana wa kuwanusuru.
38. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbinguni na ardhi.
Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliomo vifuani.
39. Yeye ndiye aliye kufanyeni manaibu katika ardhi. Na anaye
kufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa
Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila
khasara.
40. Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waomba
badala ya Mwenyezi Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi? Au
wana ushirika wowote katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na
hoja zilizo wazi? Lakini madhaalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu
tu.
41. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke.
Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipo kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole
Mwenye kusamehe.
42. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba
akiwajia mwonyaji bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine
lolote. Lakini alipo wajia mwonyaji hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo
Haki,
43. Kwa kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na
vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio
wasibu watu wa kale? Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu.
Wala hutapata mageuko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.
44. Je! Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa
walio kuwa kabla
45. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa waliyo
yachuma, basi asingeli muacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye
anawachukulia mpaka ufike muda maalumu. Basi ukifika muda wao basi hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake baraabara.
36 - YA-SIN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Ya-Sin (Y.S.).
2. Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima!
3. Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,
4. Juu ya Njia Iliyo Nyooka.
5. Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa
wenye kughafilika.
7. Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao,
kwa hivyo hawaamini.
8. Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo
vichwa vyao viko juu tu.
9. Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na
tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.
10. Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
11. Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha
Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira
mwema.
12. Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo
yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari
asli lenye kubainisha.
13. Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio
tumwa.
14. Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu
kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
15. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa
Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
16. Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa
kwenu.
17. Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.
18. Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha
basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.
19. Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa?
Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.
20. Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema:
Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.
21. Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe
wameongoka.
22. NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake
mtarejeshwa?
23. Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa
Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala
hawataniokoa.
24. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio
dhaahiri.
25. Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!
26. Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli
jua
27. Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni
mwa walio hishimiwa.