Part 24
32. BASI NI NANI dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye msingizia uwongo
Mwenyezi Mungu na kuikanusha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makaazi ya hao makafiri?
33. Na aliye ileta Kweli na akaithibitisha
- hao ndio wachamngu.
34. Watapata watakacho taka kwa Mola wao
Mlezi. Hayo ndiyo malipo ya watendao mema.
35.
36. Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake? Na ati
wanakutishia kwa hao wenginewe wasio kuwa Yeye! Na aliye hukumiwa na Mwenyezi
Mungu kupotea hana wa kumwongoa.
37. Na ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa hana wa kumpotoa. Je!
Mwenyezi Mungu si Mwenye nguvu anaye weza kulipiza?
38. Na ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi. Bila ya
shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnao waomba badala ya
Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza
kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema
yake? Sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Kwake Yeye wategemee wanao
tegemea.
39. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni mwezavyo, mimi pia nafanya. Basi
mtakuja ona
40. Ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mshukia
adhabu ya daima.
41. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa
Haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila ya shaka
amepotoka kwa khasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao. *
42. MWENYEZI MUNGU huzipokea roho zinapo kufa. Na zile zisio kufa
wakati wa kulala kwake, huzishika zilizo hukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine
mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa
watu wanao fikiri.
43. Au ndio wanachukua waombezi badala ya Mwenyezi Mungu? Sema:
Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui lolote?
44. Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Ni wake Yeye tu
ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake.
45. Na anapo tajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyoyo za wasio iamini
Akhera huchafuka. Na wanapo tajwa wenginewe asiye kuwa Yeye basi wao
hufurahi.
46. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi! Mjuzi wa
yasiyo onekana na yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika
waliyo kuwa wakikhitalifiana.
47. Na lau kuwa walio dhulumu wangeli kuwa na vyote viliomo duniani
na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikomboa
katika adhabu mbaya hiyo Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu
wasiyo kuwa wakiyatarajia.
48. Na utawadhihirikia ubaya wa waliyo yachuma, yatawazunguka waliyo
kuwa wakiyafanyia mzaha.
49. Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa neema
zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo ni
mtihani! Lakini wengi wao hawajui!
50. Waliyasema haya waliyo kuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyo
kuwa wakiyachuma.
51. Basi ukawasibu uovu wa waliyo yachuma. Na wale walio dhulumu
miongoni mwa hawa utawasibu uovu wa waliyo yachuma vile vile. Nao si wenye
kushinda.
52. Kwani wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki
amtakaye na akamkadiria? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu
wanao amini.
53. Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa
na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika
Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
54. Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake, kabla ya
kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.
55. Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu
kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali
hamtambui.
56. Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyo poteza
upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya
maskhara!
57. Au ikasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka
ningeli kuwa miongoni mwa wenye kumchamngu.
58. Au ikasema inapo ona adhabu: Lau kuwa ningeli pata fursa
nyengine, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.
59. Wapi! Bila ya shaka zilikujia Ishara zangu, nawe
ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!
60. Na Siku ya Kiyama utawaona walio msingizia uwongo Mwenyezi Mungu
nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanao takabari?
61. Na Mwenyezi Mungu atawaokoa wenye kujikinga kwa ajili ya kufuzu
kwao. Hapana uovu utao wagusa, wala hawatahuzunika.
62. Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi
juu ya kila kitu.
63. Yeye anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale walio zikataa
Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye kukhasiri.
64. Sema: Je! Mnaniamrisha nimuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, enyi
majaahili?
65. Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa kabla yako:
Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu a'mali zako zitaanguka, na lazima
utakuwa miongoni mwa wenye kukhasiri.
66. Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye
kushukuru.
67. Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kadiri
yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa
katika mkono wake wa kuume. Subhanahu wa Taa'la Ametakasika na Ametukuka na
hayo wanayo mshirikisha nayo.
68. Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo
katika ardhi, isipo kuwa aliye mtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara
nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea.
69. Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na Kitabu
kitawekwa, na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa
haki, wala hawatadhulumiwa.
70. Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyo yafanya, na Yeye anayajua
sana wanayo yatenda.
71. Na walio kufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa makundi. Mpaka
watakapo ifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani
hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na
kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Kwani! Lakini limekwisha thibiti
neno la adhabu juu ya makafiri.
72. Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo. Basi nayo ni
ubaya ulioje wa makaazi ya wanao takabari!
73. Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa
makundi, mpaka watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi
wake watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mmet'ahirika. Basi
ingieni humu mkae milele.
74. Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za Mwenyezi
Mungu aliye tutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika
Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
75. Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Kiti cha enzi cha
Mwenyezi Mungu, wakimtakasa na kumsifu Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa baina
yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa
viumbe vyote!
40 - GHAAFIR (AU AL MUUMIN)
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a, Mim.
2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu,
Mwenye kujua.
3. Anaye samehe dhambi na anaye pokea toba, Mkali wa kuadhibu,
Mwenye ukarimu, hakuna mungu ila Yeye; marejeo ni kwake.
4. Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu ila walio kufuru; basi
kusikughuri wewe kutanga tanga kwao katika nchi.
5. Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na makundi mengine baada
yao. Na kila taifa lilikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate. Na walibishana
kwa upotovu ili kuipindua haki. Kwa hivyo niliwakamata. Basi ilikuwaje adhabu
yangu!
6. Namna hivi limewathibitikia makafiri neno la Mola wako Mlezi ya
kwamba wao ni watu wa Motoni.
7. Wale wanao beba A'rshi, na wanao izunguka, wanamsabihi na
kumhimidi Mola wao Mlezi, na wanamuamini, na wanawaombea msamaha walio amini
kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi
wasamehe walio tubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya
Jahannamu.
8. Mola wetu Mlezi! Na waingize katika Bustani za Milele ulizo
waahidi. Na uwape haya pia wale walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na wake
zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
9. Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye maovu siku hiyo, hakika
umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa.
10. Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya shaka
kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu,
mlipo kuwa mnaitwa kwenye Imani nanyi mkakataa.
11. Watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufisha mara mbili, na umetuhuisha
mara mbili! Basi tunakiri madhambi yetu. Basi je, ipo njia ya kutoka?
12. Hayo ni hivyo kwa sababu mlikuwa akiombwa Mwenyezi Mungu peke
yake mnakataa. Na akishirikishwa mnaamini. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu Mkuu.
13. Yeye ndiye anaye kuonyesheni Ishara zake, na anakuteremshieni
kutoka mbinguni riziki. Na hapana anaye kumbuka ila anaye rejea.
14. Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, na
wangachukia makafiri.
15. Yeye ndiye Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A'rshi. Hupeleka Roho kwa
amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa Siku ya Mkutano.
16. Siku watakayo dhihiri wao. Hapana kitacho fichikana chochote
chao kwa Mwenyezi Mungu. Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Mwenyezi Mungu Mmoja
Mtenda nguvu.
17. Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo chuma. Hapana dhulma leo.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
18. Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni,
nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa
kuitikiwa.
19. (Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo ficha
vifua.
20. Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao wanao waomba
badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia
Mwenye kuona.
21. Kwani hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho
wa walio kuwa kabla yao? Hao walikuwa wamewazidi hawa kwa nguvu na athari
katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwatia mkononi kwa sababu ya madhambi yao. Na
wala hapakuwa wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.
22. Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawajia Mitume wao kwa hoja zilizo
wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyezi Mungu akawakamata. Bila ya shaka Yeye
ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.
23. Na kwa yakini tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na
uthibitisho ulio wazi,
24. Kumwendea Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema: Huyu ni mchawi,
mwongo mkubwa.
25. Basi alipo waletea Haki inayo toka kwetu, walisema: Waueni
watoto wanaume wa wale walio muamini na wawacheni hai wanawake wao. Na haviwi
vitimbi vya makafiri ila katika upotovu.
26. Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola
wake Mlezi! Mimi nachelea asije kubadilishieni dini yenu, au akatangaza
uharibifu katika nchi.
27. Na Musa akasema: Mimi najikinga kwa Mola wangu Mlezi na Mola
wenu Mlezi anilinde na kila mwenye jeuri asiye iamini Siku ya Hisabu.
28. Na akasema mtu mmoja Muumini, aliye kuwa mmoja katika watu wa
Firauni aliye ficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu
Mlezi ni Mwenyezi Mungu? Na hali naye amekujieni na hoja zilizo wazi? Na akiwa
yeye mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, na akiwa mkweli
yatakufikieni baadhi ya hayo anayo kuahidini. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi
apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa.
29. Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni
nani atakaye nisaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia?
Firauni akasema: Sikupeni shauri ila ile niliyo iona, wala sikuongozeni ila
kwenye njia ya uwongofu.
30. Na akasema yule aliye amini: Enyi watu wangu! Hakika mimi
nakukhofieni mfano wa siku za makundi,
31. Mfano wa hali ya watu wa Nuhu na A'di na Thamudi na wale wa
baada yao. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja.
32. Na enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni Siku ya
mayowe.
33. Siku mtakapo geuka kurudi nyuma. Hamtakuwa na wa kukulindeni kwa
Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi huyo hana
wa kumwongoa.
34. Na alikwisha wajieni Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini
nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyo kuleteeni; mpaka alipo kufa
mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta kabisa Mtume baada yake. Kama hivyo Mwenyezi
Mungu humwacha kupotea anaye pindukia mipaka katika maasi anaye jitia
shaka.
35. Hao ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu pasipo
ushahidi wowote ulio wafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele
ya walio amini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo muhuri juu ya kila moyo wa
jeuri anaye jivuna.
36. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate
kuzifikia njia,
37. Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi
bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyo pambiwa
ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila
katika kuangamia tu.
38. Na yule aliye amini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni mimi,
nitakuongozeni njia ya uwongozi mwema.
39. Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni starehe ipitayo
tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.
40. Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na
anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao
wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu.
41. Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye uwokofu,
nanyi mnaniita kwenye Moto?
42. Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule
ambaye simjui, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu Mwenye kusamehe?
43. Bila ya shaka mnaye niitia kumuabudu hastahiki wito duniani wala
Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanao pindukia mipaka
ndio watu wa Motoni!
44. Basi mtayakumbuka ninayo kuambieni. Nami namkabidhi Mwenyezi
Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake.
45. Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizo zifanya.
Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni.
46. Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapo fika Saa ya Kiyama
patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!
47. Na watapo hojiana huko Motoni, wanyonge watawaambia walio
jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, hamtuondolei sehemu ya
huu Moto?
48. Watasema walio jitukuza: Hakika sote sisi tumo humo humo! Kwani
Mwenyezi Mungu kesha hukumu baina ya waja!
49. Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu: Mwombeni Mola
wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu.
50. Nao watasema: Je! Hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu kwa hoja
zilio wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya makafiri
hayawi ila ni kupotea bure.
51. Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini
katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi,
52. Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata
laana, na watapata makaazi mabaya kabisa.
53. Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na tukawarithisha Wana wa
Israili Kitabu,
54. Ambacho ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili.
55. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na omba
msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na
asubuhi.
56. Hakika hao wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya
uthibitisho wowote uliyo wajia, hawana vifuani mwao ila kutaka ukubwa tu, na
wala huo hawaufikilii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye
kusikia, Mwenye kuona.
57. Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko
kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui.
58. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani; na walio amini na
watendao mema hawalingani na muovu. Ni machache mnayo yakumbuka.
59. Hakika Saa (ya Kiyama) itafika, nayo haina shaka. Lakini watu
wengi hawaamini.
60. Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika
wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike.
61. Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni usiku ili mpate kutulia humo, na
mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila juu ya
watu, lakini watu wengi hawashukuru.
62. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa kila kitu.
Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi?
63. Namna hivi ndivyo walivyo geuzwa walio kuwa wakizikataa Ishara
za Mwenyezi Mungu.
64. Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni ardhi kuwa ni pahala pa
kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri sura zenu,
na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Basi
ametukuka Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.
65. Yeye ndiye aliye Hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi
muabuduni Yeye mkimsafishia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wa walimwengu wote.
66. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya
Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja zilizo dhaahiri kutokana na Mola wangu Mlezi.
Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote.
67. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii,
kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha
mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanao kufa
kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate kufahamu.
68. Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe,
basi huliambia: Kuwa! Likawa.
69. Je! Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu?
Wanageuziwa wapi?
70. Ambao wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma Mitume wetu. Basi
watakuja jua.
71. Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku
wanabururwa
72. Katika maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni,
73. Tena wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwashirikisha
74. Badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani
hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia makafiri
wapotelee mbali.
75. Haya ni kwa sababu mlikuwa mkijitapa katika ardhi pasipo haki,
na kwa sababu mlikuwa mkijishaua.
76. Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo milele. Basi ni
maovu yaliyoje makaazi ya wanao takabari!
77. Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama
tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini wao
watarudishwa kwetu tu.
78. Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika
hao tumekusimulia khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete
Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija amri ya Mwenyezi
Mungu huhukumiwa kwa Haki, na hapo wapotofu watakhasiri.
79. Mwenyezi Mungu aliye kujaalieni nyama hoa, mifugo, ili muwapande
baadhi yao, na muwale baadhi yao.
80. Na katika hao mnayo manufaa kadhaa wa kadhaa, na mnapata kwao
haja ziliomo vifuani mwenu; na mnachukuliwa juu yao, na juu ya marikebu.
81. Naye anakuonyesheni Ishara zake. Basi Ishara gani za Mwenyezi
Mungu mnazo zikataa?
82. Kwani hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa walio
kuwa kabla yao? Wao walikuwa wengi kuliko hawa, na wamewashinda kwa nguvu na
athari katika nchi. Wala hayakuwafaa hayo waliyo kuwa wakiyachuma.
83. Walipo wajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi walijitapa kwa
ilimu waliyo kuwa nayo. Basi yakawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia
maskhara.
84. Walipo iona adhabu yetu walisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu
kuwa ni wa pekee, na tunaikataa miungu tuliyo kuwa tukiishirikisha naye.
85. Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa kitu wakati ambao
wamekwisha iona adhabu yetu. Huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kuwa kwa
waja wake. Na hapo walio kufuru walikhasiri.
41 - FUSS'ILAT (AU H'A MIM
SAJDAH)
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a Mim
2. Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye
kurehemu.
3. Hichi ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu
kwa watu wanao jua.
4. Kitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini wengi katika
wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii.
5. Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo
tuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe
tenda, nasi tunatenda.
6. Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya
kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na
mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha,
7. Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera.
8. Hakika wanao amini na wakatenda mema watakuwa na ujira usio na
ukomo.
9. Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika siku mbili,
na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote.
10. Na akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo na
akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao
uliza.
11. Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na
ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni
wat'iifu.
12. Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akazipangia kila
mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na kwa ulinzi. Hichi
ndicho kipimo cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua.
13. Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa
adhabu ya A'di na Thamudi,
14. Walipo wajia Mitume mbele
15. Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema:
Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi
Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa
Ishara zetu!
16. Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za ukorofi, ili
tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu
ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
17. Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu kuliko
uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale
waliyo kuwa wakiyachuma.
18. Na tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu.
19. Na siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto,
nao wakikgawanywa kwa makundi.
20. Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho
yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
21. Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo
zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye
ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.
22. Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na
ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi
katika mliyo kuwa mkiyatenda.
23. Basi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi.
Imekuangamizeni; na mmekuwa miongoni mwa walio khasiri.
24. Basi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba radhi
hawakubaliwi.
25. Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na
nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo pita kabla
yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye
kukhasirika.
26. Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii, na timueni
zogo, huenda mkashinda.
27. Basi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru adhabu kali, na
hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
28. Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo
watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa
Ishara zetu.
29. Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio
tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate
kuwa miongoni wa walio chini kabisa.
30. Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha
wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala
msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa.
31. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera,
na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo
vitaka.
32. Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
33. Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na
akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?
34. Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo
yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea
uchungu.
35. Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye
bahati kubwa.
36. Na Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi wewe jikinge kwa Mwenyezi
Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
37. Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi
msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa
nyinyi mnamuabudu Yeye tu.
38. Na ikiwa watajivuna, basi hao walioko kwa Mola wako Mlezi
wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.
39. Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapo
iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye
ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila
kitu.
40. Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu
hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani
Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.
41. Kwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo wajia
(wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
42. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa
na Mwenye hikima, Msifiwa.
43. Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla yako.
Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye adhabu
chungu.
44. Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema:
Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu?
Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo
uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako
pahala mbali.
45. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati
yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa.
Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
46. Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye
kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si
mwenye kuwadhulumu waja.