Part 25
47. UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi
Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba,
wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi
washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu
anaye shuhudia hayo.
48. Na wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo kwanza, na wakawa
na yakini kuwa hawana pa kukimbilia.
49. Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata shari,
mara huvunjika moyo akakata tamaa.
50. Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa
dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama
kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema
yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na
kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
51. Na tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga upande, na
inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu.
52. Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi
ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani
wa mbali?
53. Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi
zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola
wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
54. Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi! Ama
hakika Yeye amekizunguka kila kitu.
42 - ASH-SHUURA
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a Mim
2. A'yn Sin Qaf
3. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hikima anavyo
kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako.
4. Ni vyake viliomo mbinguni, na viliomo katika ardhi. Na Yeye
ndiye Mtukufu, Mkuu.
5. Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa
Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
6. Na wale walio wafanya walinzi wengine badala yake Yeye, Mwenyezi
Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.
7. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu
wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano,
haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni.
8. Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma mmoja,
lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu hawana
mlinzi wala msaidizi.
9. Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu
ndiye Mlinzi khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa
kila kitu.
10. Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa
Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye mtegemea na
kwake Yeye narejea.
11. Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume
katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii.
Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
12. Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki
amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu.
13. Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia
wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala
msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu
humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye.
14. Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya
husuda iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa
Mola wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli
hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka
inayo wahangaisha.
15. Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa,
wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi Mungu
katika Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni
Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na
nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na
Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.
16. Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa, hoja
za hawa ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo ghadhabu, na
itakuwa kwao adhabu kali.
17. Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu kwa Haki, na Mizani.
Na nini kitakacho kujuulisha ya kwamba pengine Saa ya Kiyama ipo karibu?
18. Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini wanao amini
wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao wanao
bishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa.
19. Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku ampendaye. Naye
ni Mwenye nguvu, Mtukufu.
20. Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika mavuno yake,
na mwenye kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini katika Akhera
hana fungu.
21. Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini asiyo
itolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la kupambanua basi
wangeli katiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu
chungu.
22. Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa sababu ya
waliyo yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema watakuwamo
katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi. Hiyo
ndiyo fadhila kubwa.
23. Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walio amini
na wakatenda mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika
kujikurubisha. Na anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Msamehevu Mwenye shukrani.
24. Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu
akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta upotofu na
anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliomo vifuani.
25. Naye ndiye anaye pokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa,
na anayajua mnayo yatenda.
26. Na anawaitikia wanao amini na wakatenda mema, na anawazidishia
fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu chungu.
27. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki waja wake, basi
bila ya shaka wangeli panda kiburi katika dunia. Lakini anaiteremsha kwa kipimo
akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
28. Naye ndiye anaye iteremsha mvua baada ya wao kwisha kata tamaa,
na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi Mwenye kuhimidiwa.
29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama alio
waeneza. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.
30. Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono
yenu. Naye anasamehe mengi.
31. Na nyinyi hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala nyinyi hamna
mlinzi wala msaidizi badala ya Mwenyezi Mungu.
32. Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea
baharini kama vilima.
33. Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu
ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri
akashukuru.
34. Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyo yatenda hao
watu. Naye husamehe mengi.
35. Na ili wajue wanao jadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana
pahala pa kukimbilia.
36. Basi vyote mlivyo pewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini
kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili ya walio amini,
na wakawa wanamtegemea Mola wao Mlezi,
37. Na wanayo yaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapo
kasirika wao husamehe,
38. Na wanao mwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo
yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na kutokana na tulicho waruzuku wakawa
wanatoa,
39. Na ambao wanapo fanyiwa jeuri hujitetea.
40. Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe,
na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye
hawapendi wenye kudhulumu.
41. Na wanao jitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya
kuwalaumu.
42. Bali lawama ipo kwa wale wanao wadhulumu watu, na wanafanya
jeuri katika nchi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.
43. Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya
kuazimiwa.
44. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana mlinzi baada
yake. Na utawaona wenye kudhulumu watakapo iona adhabu wanasema: Je! Ipo njia
ya kurudi?
45. Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa
unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini watasema: Hakika
wapatao khasara ni hao walio khasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ama
hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya daima.
46. Wala hawatakuwa na walinzi wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote.
47. Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyo epukika
itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa pa kukimbilia wala hamtakuwa na
cha kukingia.
48. Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwangalizi wao.
Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi tukimwonjesha mtu rehema
kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyo yatanguliza
mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.
49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba
apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto
wa kiume,
50. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye
tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.
51. Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa
Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia
ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.
52. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui
Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo
tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye Njia
Iliyo Nyooka.
53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo mbinguni
na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.
43 - AZZUKHRUF
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a Mim
2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.
3. Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu.
4. Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu
na yenye hikima.
5. Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio
pita mipaka kwa ukafiri?
6. Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
7. Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
8. Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa
watu wa zamani umekwisha pita.
9. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka
watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi,
10. Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani
yake njia mpate kuongoka.
11. Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi,
na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo
tolewa.
12. Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na
akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda.
13. Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola
wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu
atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe.
14. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
15. Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni
mtovu wa fadhila aliye dhaahiri.
16. Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na
akakuteulieni nyinyi watoto wanaume?
17. Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano
Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira.
18. Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi
kusema kwa bayana...?
19. Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni
wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao
watahojiwa!
20. Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu
sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
21. Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao
wanakishikilia hicho?
22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini
makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao.
23. Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake
walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika
dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao.
24. Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora
kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo
tumwa.
25. Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio
kadhibisha!
26. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika
mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu,
27. Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa.
28. Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake
ili warejee.
29. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na
Mtume aliye bainisha.
30. Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika
tunaukataa.
31. Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa
katika miji miwili hii?
32. Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi
tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua
baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya
wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo
yakusanya.
33. Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia
wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia
wanazo pandia,
34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu
yake,
35. Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya
dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu.
36. Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa
ndiye rafiki yake.
37. Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa
wameongoka.
38. Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na
wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe!
39. Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi
mnashirikiana katika adhabu.
40. Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu
na waliomo katika upotofu ulio wazi?
41. Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao.
42. Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza
juu yao.
43. Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye
Njia Iliyo Nyooka.
44. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja
ulizwa.
45. Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya
miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani?
46. 46, Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni
na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa
walimwengu wote!
47. Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
48. Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi
kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.
49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile
ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
50. Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja
ahadi.
51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu!
Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je!
Hamwoni?
52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema
waziwazi?
53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika
pamoja naye wakamwandama?
54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao
walikuwa watu wapotovu.
55. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!
56. Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye.
57. Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga
ukelele.
58. Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia
mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!
59. Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya
ni mfano kwa Wana wa Israili.
60. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika
ardhi wakifuatana.
61. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie
shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
62. Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa
dhaahiri.
63. Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na
hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni
Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.
64. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu
Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
65. Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole
wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
66. Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao
hawatambui?
67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa
wachamngu.
68. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala
hamtahuzunika.
69. Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu.
70. Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo.
71. Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na
vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa
humo milele.
72. Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa
mkiyafanya.
73. Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala.
74. Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu.
75. Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
76. Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa
madhaalimu.
77. Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako
Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
78. Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi
mlikuwa mnaichukia Haki.
79. Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao
pitisha.
80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi!
Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
81. Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa
kwanza kumuabudu.
82. Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi,
na hayo wanayo msifia.
83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku
yao waliyo ahidiwa.
84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye
ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
85. Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani
yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa.
86. Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea
mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.
87. Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema:
Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?
88. Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni
watu wasio amini.
89. Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.
44 - ADDUKHAN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a Mim
2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,
3. Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni
Waonyaji.
4. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,
5. Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye
kusikia Mwenye kujua.
7. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi
mna yakini.
8. Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na
Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.
9. Lakini wao wanacheza katika shaka.
10. Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio
dhaahiri,
11. Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!
12. Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
13. Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye
kubainisha.
14. Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni
mwendawazimu.
15. Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini
mtarejea vile vile!
16. Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi
ni wenye kutesa.
17. Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na
aliwafikia Mtume Mtukufu.
18. Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni
Mtume Muaminifu.
19. Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni
uthibitisho ulio wazi.
20. Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi
pia, ili msinipige mawe.
21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
22. Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni
wakosefu.
23. Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa
yakini mtafuatwa.
24. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi
litakalo zamishwa.
25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!
26. Na mimea na vyeo vitukufu!
27. Na neema walizo kuwa wakijistareheshea!
28. Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe.
29. La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula.
30. Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya
kuwadhalilisha,
31. Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia
mipaka.
32. Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe.
33. Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
34. Hakika hawa wanasema:
35. Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi
hatufufuliwi.
36. Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
37. Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao?
Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.
38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa
mchezo.
39. Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.
40. Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.
41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala
hawatanusuriwa.
42. Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye
Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
43. Hakika Mti wa Zaqqum,
44. Ni chakula cha mwenye dhambi.
45. Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni
46. Kama kutokota kwa maji ya moto.
47. (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu!
48. Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo
chemka.
49. Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!
50. Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.
51. Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani,
52. Katika mabustani na chemchem,
53. Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana,
54. Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini.
55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.
56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi
Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu,
57. Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu
kukubwa.
58. Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate
kukumbuka.
59. Ngoja tu, na wao wangoje pia.
45 - AL - JAATHIYA
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a Mim
2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu,
Mwenye hikima.
3. Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini.
4. Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara
kwa watu wenye yakini.
5. Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi
Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na
mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili.
6. Hizi Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi
gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake?
7. Ole wake kila mzushi mwenye dhambi!
8. Anaye sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anashikilia
yale yale aliyo katazwa, na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie
adhabu chungu!
9. Na anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia mzaha.
Watu hao ndio watakao kuwa na adhabu ya kufedhehesha.
10. Na nyuma
11. Huu ni uwongofu. Na wale wale walio zikataa Ishara za Mola wao
Mlezi watapata adhabu inayo tokana na ghadhabu iliyo chungu.
12. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili humo
zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake, na mpate
kushukuru.
13. Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika
ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa watu wanao
fikiri.
14. Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za
Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
15. Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye
kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu Mlezi.
16. Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii,
na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu
wote.
17. Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila
baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa baina yao. Hakika Mola
wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa
wakikhitalifiana.
18. Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi ifuate,
wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu.
19. Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na
hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa
wamchao.
20. Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni uwongofu, na
rehema kwa watu wanao yakinisha.
21. Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama walio
amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya
wanayo ihukumu!
22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili
kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa.
23. Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake,
na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri
juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi
nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?
24. Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani - twafa na
twaishi, na hapana kinacho tuhiliki isipo kuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu
ya hayo, ila wao wanadhani tu.
25. Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema:
Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasemao kweli.
26. Sema: Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha anakufisheni, kisha
anakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui.
27. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na
siku itapo simama Saa ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye kushikamana na
upotovu.
28. Na utauona kila umma umepiga magoti, na kila umma utaitwa kwenda
soma kitabu chake: Leo mtalipwa mliyo kuwa mkiyatenda.
29. Hichi kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi
tulikuwa tukiyaandika mliyo kuwa mkiyatenda.
30. Ama walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawatia
katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi.
31. Na ama walio kufuru, wataambiwa: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya
zangu nanyi mkapanda kichwa, na mkawa watu wakosefu?
32. Na ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Saa
haina shaka, nyinyi mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana tu, wala
hatuna yakini.
33. Basi ubaya wa waliyo yatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka
waliyo yafanyia maskhara.
34. Na itasemwa: Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyo sahau mkutano
wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa kukunusuruni.
35. Hayo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu;
na maisha ya dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo wala hao
hawatakubaliwa udhuru wao.
36. Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mbingu,
na Mola Mlezi wa ardhi, na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
37. Na ukubwa ni wake Yeye tu, mbinguni na katika ardhi, naye ni
Mwenye nguvu, Mwenye hikima.