Part 3
253. MITUME hao tumewatukuza baadhi
254. Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni kabla haijafika
Siku ambayo hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi. Na makafiri ndio
madhaalimu.
255. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo
yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo
mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini
yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote
katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda
mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye
juu, na ndiye Mkuu.
256. Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha
pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu
bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
257. Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na
kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni Mashet'ani. Huwatoa
kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo
watadumu.
258. Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola wake Mlezi
kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola wangu ni yule
ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibrahim
akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe
magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu.
259. Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu
tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi
Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza:
Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku.
Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji
vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara
kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha
nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye
uweza juu ya kila kitu.
260. Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo
fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili
moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke
juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika
Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
261. Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni
kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo
punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
wasaa na Mwenye kujua.
262. Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha
hawafuatishii masimbulizi wala udhia kwa walicho toa, wana ujira wao kwa Mola
wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
263. Kauli njema na usamehevu ni bora kuliko sadaka inayo fuatiliwa
na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha na Mpole.
264. Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na
maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi
Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu
yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi
hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
makafiri.
265. Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta radhi ya
Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali
pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama
haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo
yatenda.
266. Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na
mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee
ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga chenye moto,
kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara ili mpate
kufikiri.
267. Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na
katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo
vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na
jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.
268. Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na anakuamrisheni mambo
machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila zitokazo kwake. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
269. Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima bila ya shaka
amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.
270. Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo weka basi hakika
Mwenyezi Mungu anajua. Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
271. Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha mkawapa mafakiri
kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi ya maovu yenu. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
272. Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa
amtakaye. Na kheri yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu. Wala msitoe ila kwa
kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mtakayo toa mtalipwa kwa
ukamilifu, wala hamtadhulumiwa.
273. Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia za Mwenyezi Mungu,
wasio weza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye wajua hali zao
huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama
zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa, basi kwa
yakini Mwenyezi Mungu anaijua.
274. Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri,
wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala
hawatahuzunika.
275. Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na
Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini
Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa
na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo
kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao
ndio watu wa Motoni, humo watadumu.
276. Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na
Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi.
277. Hakika wale walio amini na wakatenda mema na wakashika Sala na
wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu
juu yao, wala hawatahuzunika.
278. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo
bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini.
279. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume
wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala
msidhulumiwe.
280. Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka afarijike.
Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
281. Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha
kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.
282. Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi
andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae
kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye deni juu yake
aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze
chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au
hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na
mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili,
basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi.
Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi
wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka
muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi
kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya
mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini
mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na
mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
283. Na mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, yatosha kukabidhiwa
rahani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe basi aliye aminiwa airudishe
amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala msifiche
ushahidi. Na atakaye ficha basi hakika moyo wake ni wenye kutenda dhambi. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
284. Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya Mwenyezi Mungu. Na
mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu
atakuhisabuni kwayo. Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
285. Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi
wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake,
na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume
wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet'ii. Tunakutaka maghfira Mola
Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.
286. Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya
iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu
yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola
wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu.
Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na
uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya
makafiri.
3 - AL I'MRAN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Alif Laam Miim.
2. Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye Aliye Hai, Msimamizi wa
yote milele.
3. Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinacho sadikisha yaliyo kuwa
kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili
4. Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha Furqani
(Upambanuo). Hakika walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu
kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa.
5. Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki chochote kwake, duniani wala
mbinguni.
6. Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna
apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
7. Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya
muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za
mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa
kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila
Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi
tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo
kuwa wenye akili.
8. (Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya
kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye Mpaji.
9. Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye Mkusanyaji wa watu kwa Siku isiyo na
shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.
10. Kwa hakika wale walio kufuru hazitowafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu
mali zao, wala watoto wao; nao hao ndio kuni za Motoni-
11. - Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio kuwa kabla
yao. Walikanusha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa madhambi yao;
na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
12. Waambie walio kufuru: Karibuni mtashindwa na mtakusanywa, mtiwe
kwenye Jahannam; nako huko ni makao mabaya kabisa.
13. Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi mawili yalipo
pambana. Jeshi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jingine kafiri
likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu
humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa
wenye macho.
14. Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na
mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni
starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo
mema.
15. Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wachamngu ziko
Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na wake walio
takaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona
waja wake,
16. Ambao husema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumeamini, basi
tufutie madhambi yetu, na tuepushe na adhabu ya Moto,
17. Wanao subiri, wanao sema kweli, na wat'iifu, na wanao toa
sadaka, na wanao omba maghafira kabla ya alfajiri.
18. Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa
hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu
ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.17
19. Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio
pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya
uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
20. Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu
kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie walio pewa
Kitabu na wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka. Na
wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwaona waja wake.
21. Hakika wanao zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawauwa
Manabii pasipo haki, na wakawauwa watu waamrishao Haki wabashirie adhabu
kali.
22. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika duniani na Akhera. Nao
hawatapata wa kuwanusuru.
23. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaitwa kukiendea
Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao; kisha baadhi yao wanageuka
wanakikataa.
24. Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa Moto isipo kuwa kwa
siku chache tu. Na yakawadanganya katika dini yao yale ambayo wenyewe waliyo
kuwa wakiyazua.
25. Basi itakuwaje tutakapo wakusanya Siku ambayo haina shaka kuja
kwake? Na kila nafsi italipwa kama ilivyo chuma, bila ya kudhulumiwa.
26. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe humpa
ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye, na
humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni Muweza wa
kila kitu.
27. Wewe huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika
usiku. Na humtoa hai kutokana na maiti, na humtoa maiti kutokana na aliye hai.
Na unamruzuku umtakaye bila ya hisabu.
28. Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala ya Waumini.
Na anaye fanya hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Ila ikiwa
kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye.
Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.
29. Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyafichua Mwenyezi
Mungu anayajua; na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo duniani. Na Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu.
30. Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya
yamehudhurishwa, na pia ubaya ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako
masafa marefu baina ya ubaya huo na yeye. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni
naye. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
31. Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi,
Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.
32. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka basi
Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.
33. Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo wa Ibrahim
na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.
34. Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na
Mwenye kujua.
35. Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri
kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye
kusikia na Mwenye kujua.
36. Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke -
na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa - Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na
mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na
Shet'ani aliye laaniwa.
37. Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza
makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya alipo
ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu!
Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na
Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
38. Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi, akasema: Mola
wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi.
39. Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika kamnadia: Hakika Mwenyezi
Mungu anakubashiria Yahya, ataye kuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa
Mwenyezi Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa watu wema.
40. Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata mwana na hali
ukongwe umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi
Mungu hufanya apendavyo.
41. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema: Alama yako ni
kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu. Na mdhukuru
Mola Mlezi wako kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi.
42. Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Kwa hakika
Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake
wote.
43. Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname
pamoja na wainamao.
44. Hizi ni khabari za ghaibu tunazo kufunulia; nawe hukuwa nao
walipo kuwa wakitupa kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa nao walipo
kuwa wakishindana.
45. Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu
anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa
Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio
karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).
46. Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima
wake, na atakuwa katika watu wema.
47. Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali
hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi
Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa.
48. Na atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na Injili.
49. Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na
Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura
ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na
ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa
idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba
katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye
kuamini.
50. Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili
nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara
kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini
mimi.
51. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi.
Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
52. Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani
wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi
wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika
ni Waislamu.
53. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyo yateremsha, na tumemfuata
huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.
54. Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu akapanga
mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.
55. Pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na
nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na nitawaweka wale
walio kufuata juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo
yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa mkikhitalifiana.
56. Ama wale walio kufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na
Akhera, wala hawatapata wa kuwanusuru.
57. Na ama wale walio amini na wakatenda mema basi Mwenyezi Mungu
atawalipa ujira wao kaamili. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu.
58. Haya tunayo kusomea ni katika Aya na Ukumbusho wenye
hikima.
59. Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam;
alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa.
60. Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni
mwa wanao fanya shaka.
61. Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii
waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu,
na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya
Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.
62. Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila Mwenyezi
Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
63. Na
64. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina
yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala
tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi
badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi
ni Waislamu.
65. Enyi Watu wa Kitabu! Mbona mnabishana juu ya Ibrahim, na hali
Taurati na Injili hazikuteremshwa ila baada yake? Basi hamzingatii?
66. Angalieni! Nyinyi mlibishana katika yale mliyo yajua. Mbona sasa
mnabishana katika yale msiyo yajua? Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye, na nyinyi
hamjui.
67. Ibrahim hakuwa Yahudi wala Mkristo, lakini alikuwa mwongofu
Muislamu, wala hakuwa katika washirikina.
68. Watu wanao mkaribia zaidi Ibrahim ni wale walio mfuata yeye na
Nabii huyu na walio amini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa Waumini.
69. Kipo kikundi katika Watu wa Kitabu wanao penda kukupotezeni;
lakini hawapotezi ila nafsi zao, nao wenyewe hawatambui.
70. Enyi Watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa Ishara za Mwenyezi Mungu
ilhali nyinyi mnashuhudia?
71. Enyi Watu wa Kitabu! Mbona kweli mnaivisha uwongo, na kweli
mnaificha na hali mnajua?
72. Na kikundi katika Watu wa Kitabu walisema: Yaaminini yale waliyo
teremshiwa wenye kuamini mwanzo wa mchana, na yakataeni mwisho wake; huenda
wakarejea.
73. Wala msimuamini ila anaye fuata dini yenu. Sema: Hakika uwongofu
ni uwongofu wa Mwenyezi Mungu, kuwa apewe mtu mfano wa mlio pewa nyinyi au
wakuhojini mbele ya Mola wenu Mlezi. Sema: Hakika fadhila zimo mikononi mwa
Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na
Mjuzi.
74. Yeye humchagua kumpa rehema zake amtakaye; na Mwenyezi Mungu
ndiye Mwenye fadhila kubwa.
75. Na miongoni mwa Watu wa Kitabu yupo ambaye ukimpa amana ya
mrundi wa mali atakurudishia, na miongoni mwao yupo ambaye ukimpa amana ya
dinari moja hakurudishii isipo kuwa ukimsimamia kumdai. Haya ni kwa kuwa
wakisema: Hatuna lawama kwa ajili ya hawa wasio jua kusoma. Na wanamzulia
uwongo Mwenyezi Mungu, hali nao wanajua.
76. Sivyo hivyo, bali anaye timiza ahadi yake na akamchamngu basi
Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu.
77. Hakika wanao uza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao thamani
ndogo, hao hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala Mwenyezi
Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao
watapata adhabu chungu.
78. Na wapo baadhi yao wanao pindua ndimi zao katika kusoma Kitabu
ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema:
Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na
wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na wao wanajua.
79. Haiwezi kuwa mtu aliye pewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima
na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi
Mungu.
80. Wala hatakuamrisheni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa ni miungu.
Je, atakuamrisheni ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?
81. Na pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa Manabii: Nikisha
kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha mliyo nayo,
ni juu yenu mumuamini na mumsaidie. Akasema: Je, mmekiri na mmekubali kushika
agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi shuhudieni, na
Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia.
82. Watakao geuka baada ya haya basi hao ndio wapotovu.
83. Je, wanataka dini isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu, na hali kila
kilichomo mbinguni na katika ardhi kimesilimu kwa kumt'ii Yeye kikipenda
kisipende, na kwake Yeye watarejeshwa?
84. Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyo teremshiwa sisi, na aliyo
teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na wajukuu zao, na aliyo
pewa Musa na Isa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi. Hatubagui baina
yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake.
85. Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake.
Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.
86. Mwenyezi Mungu atawaongoaje watu walio kufuru baada ya kuamini
kwao, na wakashuhudia ya kuwa Mtume huyu ni wa haki, na zikawafikia hoja zilizo
wazi? Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
87. Hao malipo
88. Humo watadumu. Hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa
nafasi.
89. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
90. Hakika wale walio kufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi
kukufuru, toba yao haitakubaliwa, na hao ndio walio potea.
91. Hakika wale walio kufuru, na wakafa hali ni makafiri
haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau
wangeli itoa. Hao watapata adhabu chungu, wala hawatakuwa na wa
kuwanusuru.
92. KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na
kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.