Part 4

 

93. Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israili isipo kuwa alicho jizuilia Israili mwenyewe kabla haijateremshwa Taurati. Sema: Leteni Taurati muisome ikiwa nyinyi ni wasema kweli. 

94. Na wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo, basi hao ndio madhaalimu. 

95. Sema: Mwenyezi Mungu amesema kweli. Basi fuateni mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina. 

96. Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote. 

97. Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu. 

98. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha ishara za Mwenyezi Mungu, na ilhali kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi kwa yote mnayo yatenda? 

99. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia aliye amini Njia ya Mwenyezi Mungu mkiitafutia kosa, na hali nyinyi mnashuhudia? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda. 

100. Enyi mlio amini! Mkiwat'ii baadhi ya walio pewa Kitabu watakurudisheni kuwa makafiri baada ya Imani yenu. 

101. Na vipi mkufuru hali nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume yuko kati yenu? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi huyo ameongozwa kwenye Njia Iliyo Nyooka. 

102. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu. 

103. Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka. 

104. Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa. 

105. Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa. 

106. Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zitasawijika. Ama hao ambao nyuso zao zitasawijika wataambiwa: Je! Mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mnakufuru. 

107. Ama wale ambao nyuso zao zitanawiri watakuwa katika rehema ya Mwenyezi Mungu. Wao humo watadumu. 

108. Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu walimwengu. 

109. Na kila kilichomo mbinguni na kilichomo ardhini ni cha Mwenyezi Mungu; na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu. 

110. Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu. 

111. Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na wakipigana nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa. 

112. Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu. Na wakastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na wamepigwa na unyonge. Hayo ni kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasina haki; hayo ni kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka. 

113. Wote hao si sawa sawa. Miongoni mwa Watu wa Kitabu wamo watu walio simama baraabara, wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za usiku, na pia wanasujudu. 

114. Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanakimbilia katika mambo ya kheri. Na hao ndio miongoni mwa watenda mema. 

115. Na kheri yoyote wanayo ifanya hawatanyimwa malipwa yake. Na Mwenyezi Mungu anawajua wachamngu. 

116. Hakika wale walio kufuru hazitawafaa kitu mali zao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio watu wa Motoni - humo watadumu. 

117. Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la watu walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao. 

118. Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo kudhuruni. Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia akilini. 

119. Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala wao hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani. 

120. Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo. 

121. Na pale ulipo toka asubuhi, ukaacha ahali zako uwapange Waumini kwenye vituo kwa ajili ya vita - na Mwenyezi Mungu anasikia na anajua. 

122. Makundi mawili miongoni mwenu yakaingiwa na woga kuwa watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao; na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. 

123. Na Mwenyezi Mungu alikwisha kunusuruni katika Badri nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru. 

124. Ulipo waambia Waumini: Je, haitakutosheni ikiwa Mola wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tatu walio teremshwa? 

125. Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu. 

126. Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 

127. Haya ni kwa ajili awakate sehemu katika walio kufuru, au awahizi wapate kurejea nyuma nao wamepwelewa. 

128. Wewe huna lako jambo katika haya - ama atawahurumia au atawaadhibu, kwani wao ni madhaalimu. 

129. Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye kurehemu. 

130. Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa. 

131. Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya makafiri. 

132. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa. 

133. Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu, 

134. Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema; 

135. Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua. 

136. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao. 

137. Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanao kanusha. 

138. Hii ni bayana kwa watu wote, na ni uwongofu, na mawaidha kwa wachamngu. 

139. Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini. 

140. Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu; 

141. Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri. 

142. Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri? 

143. Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama. 

144. Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao mshukuru. 

145. Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye kushukuru. 

146. Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri. 

147. Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri. 

148. Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema. 

149. Enyi mlio amini! Ikiwa mtawat'ii walio kufuru watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri. 

150. Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye bora wa wasaidizi. 

151. Tutazitia khofu nyoyo za walio kufuru kwa vile walivyo mshirikisha Mwenyezi Mungu na washirika ambao hakuwateremshia hoja yoyote. Na makaazi yao ni Motoni; na maovu yaliyoje maskani ya wenye kudhulumu! 

152. Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile mlivyo kuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipo legea na mkazozana juu ya amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu wanao taka dunia, na wapo miongoni mwenu wanao taka Akhera. Kisha akakutengeni nao (maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwisha kusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya Waumini. 

153. Pale mlipo kuwa mkikimbia mbio wala hamumsikilizi yeyote, na Mtume anakuiteni, yuko nyuma yenu. Mwenyezi Mungu akakupeni dhiki juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yaliyo kukoseeni wala kwa yaliyo kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda. 

154. Kisha baada ya dhiki alikuteremshieni utulivu - usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jengine nafsi zao ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyo kuwa ya haki, dhana ya kijinga. Wakisema: Hivyo tuna lolote sisi katika jambo hili? Sema: Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyo kubainishia. Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusinge uliwa hapa. Sema: Hata mngeli kuwa majumbani mwenu, basi wangeli toka walio andikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe.(Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani. 

155. Hakika wale walio rudi nyuma miongoni mwenu siku yalipo pambana majeshi mawili, Shet'ani ndiye aliye watelezesha kwa sababu ya baadhi ya makosa waliyo yafanya; na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole. 

156. Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio kufuru na wakawasema ndugu zao walipo safiri katika nchi au walipo kuwa vitani: Wangeli kuwa kwetu wasingeli kufa na wasingeli uwawa. Ili Mwenyezi Mungu afanye hayo kuwa ni majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo. 

157. Na pindi mkiuliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au mkifa, hakika maghfira na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yote wanayo yakusanya. 

158. Na mkifa au mkiuliwa ni kwa Mwenyezi Mungu ndio mtakusanywa. 

159. Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea. 

160. Akikunusuruni Mwenyezi Mungu hapana wa kukushindeni, na akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye ataye kunusuruni? Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. 

161. Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa. 

162. Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea. 

163. Hao wana vyeo mbali mbali kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote wayatendayo. 

164. Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi. 

165. Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi mmekwisha watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka kwenu wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. 

166. Na yaliyo kusibuni siku yalipo pambana majeshi mawili yalikuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ili awajue Waumini. 

167. Na ili awapambanue walio kuwa wanaafiki, wakaambiwa: Njooni mpigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu au lindeni. Wakasema: Tungeli jua kuna kupigana bila ya shaka tungeli kufuateni. Wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anajua kabisa wanayo yaficha. 

168. Hao ndio walio waambia ndugu zao na wao wenyewe wakakaa kitako: Lau wengeli tut'ii wasingeli uliwa. Sema: Ziondoleeni nafsi zenu mauti kama mnasema kweli. 

169. Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi. 

170. Wanafurahia aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. 

171. Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa Waumini, 

172. Walio mwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya kwisha patwa na majaraha - kwa walio fanya wema miongoni mwao na wakamchamngu utakuwa ujira mkubwa - 

173. Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. 

174. Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya lilio wagusa, na wakafuata yanayo mridhi Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu. 

175. Hakika huyo ni Shet'ani anawatia khofu marafiki zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini. 

176. Wala wasikuhuzunishe wale wanao kimbilia ukafirini. Hakika hao hawamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee sehemu yoyote katika Akhera, na yao wao adhabu kubwa. 

177. Hakika wale walio nunua ukafiri kwa Imani hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na yao wao ni adhabu chungu. 

178. Wala wasidhani wale wanao kufuru kwamba huu muhula tunao wapa ni kheri yao. Hakika tunawapa muhula wazidi madhambi. Na yao wao ni adhabu ya kuwadhalilisha. 

179. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka apambanue wabaya na wema. Wala haiwi kwa Mwenyezi Mungu kukujuulisheni mambo ya ghaibu. Lakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume wake amtakaye. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake. Na mkiamini na mkamchamngu mtakuwa na ujira mkubwa. 

180. Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili Siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote myatendayo. 

181. Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya walio sema: Mwenyezi Mungu ni masikini, na sisi ni matajiri. Tumeyaandika waliyo yasema, na pia kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya kuungua. 

182. Haya ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yenu, na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja, 

183. Walio sema: Mwenyezi Mungu ametuahidi tusimuamini Mtume yeyote mpaka atuletee kafara inayo teketezwa na moto. Waambie: Walikujieni Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa hayo mnayo sema, basi kwa nini mkawauwa ikiwa mlikuwa wakweli? 

184. Na wakikukanusha basi walikanushwa Mitume wengine kabla yako walio kuja na hoja waziwazi na Vitabu vyenye hikima, na Kitabu chenye nuru. 

185. Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu. 

186. Hapana shaka yoyote mtapata misukosuko katika mali zenu na nafsi zenu, na bila ya shaka yoyote mtasikia udhia mwingi kutokana na walio pewa Kitabu kabla yenu na wale walio shiriki. Na ikiwa mtasubiri na mkamchamngu basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia. 

187. Na pale Mwenyezi Mungu alipo fungamana na walio pewa Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho walicho nunua. 

188. Usiwadhanie kabisa wale wanao furahia waliyo yafanya, na wakapenda kusifiwa kwa wasiyo yatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika na adhabu. Yao wao ni adhabu chungu. 

189. Na Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. 

190. Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili, 

191. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto. 

192. Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na walio dhulumu hawana wasaidizi. 

193. Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema. 

194. Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi. 

195. Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa. 

196. Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa walio kufuru katika nchi. 

197. Hiyo ni starehe ndogo. Kisha makaazi yao yatakuwa Jahannamu. Na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia. 

198. Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata Mabustani yanayo pita mito kati yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na vilioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema. 

199. Hakika miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na yaliyo teremshwa kwenu na yaliyo teremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawabadili Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani duni. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. 

200. Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa

 

4 - AN-NISAAI

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni. 

2. Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa. 

3. Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana. 

4. Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha. 

5. Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno mazuri. 

6. Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu. 

7. Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa. 

8. Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini, wapeni katika hayo mali ya urithi, na semeni nao maneno mema. 

9. Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao watoto wanyonge wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa. 

10. Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni. 

11. Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima. 

12. Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole. 

13. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa. 

14. Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha. 

15. Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wane katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine. 

16. Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na wakitubia wakatengenea basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu. 

17. Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima. 

18. Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale wanao kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu. 

19. Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake. 

20. Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi? 

21. Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti? 

22. Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo kwisha pita. Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya. 

23. Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.