Part 5
24. NA WANAWAKE wenye waume, isipo kuwa walio milikiwa na mikono
yenu ya kulia. Ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na mmehalilishiwa wasio
kuwa hao, mtafute kwa
25. Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa
kiungwana Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu ya
kulia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa
wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama ada,
wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapo olewa kisha wakafanya
uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyo wekewa waungwana. Hayo
ni kwa yule miongoni mwenu anaye ogopa kuingia katika zina. Na mkisubiri ndio
bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
26. Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za
walio kuwa kabla yenu, na akurejezeni kwenye ut'iifu wake. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi, Mwenye hikima.
27. Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na
wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.
28. Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na mwanaadamu
ameumbwa dhaifu.
29. Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe
biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwarehemuni.
30. Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhaalimu, basi huyo
tutamwingiza Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
31. Mkiyaepuka makubwa mnayo katazwa, tutakufutieni makosa yenu
madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu.
32. Wala msitamani alicho wafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu
kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake wana fungu
katika walio vichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
33. Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyo yaacha wazazi
wawili na jamaa. Na mlio fungamana nao ahadi wapeni fungu lao. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
34. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi
Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa. Basi wanawake
wema ni wale wenye kut'ii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi
Mungu ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu
wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia
ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu.
35. Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi
pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za
mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye khabari.
36. Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na
wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa
karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio
milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi
wanao jifakhiri,
37. Ambao wanafanya ubakhili na wanaamrisha watu ubakhili, na
wanaficha fadhila alizo wapa Mwenyezi Mungu. Na tumewaandalia makafiri adhabu
ya fedheha,
38. Na ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu, wala hawamuamini
Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho; na yule ambaye Shet'ani amekuwa ndiye
rafiki yake, basi ana rafiki mbaya mno.
39. Na ingeli wadhuru nini wao lau wangeli muamini Mwenyezi Mungu na
Siku ya Mwisho, na wakatoa katika aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuwajua vyema.
40. Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu hata uzito wa chembe moja. Na
ikiwa ni jambo jema basi Yeye hulizidisha na hutoa kutoka kwake malipo
makubwa.
41. Basi itakuwaje pindi tukiwaletea kutoka kila umma shahidi, na
tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa?
42. Siku hiyo walio kufuru na wakamuasi Mtume watatamani ardhi
isawazishwe juu yao. Wala hawataweza kumficha Mwenyezi Mungu neno lolote.
43. Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue
mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini - mpaka mkoge. Na
mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa
wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu na
mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kughufiria.
44. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu wananunua upotovu na
wanakutakeni nanyi mpotee njia?
45. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema maadui zenu. Na Mwenyezi Mungu
anatosha kuwa ni Mlinzi, na anatosha kuwa ni Mwenye kukunusuruni.
46. Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa
mahala pake, na husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya kusikilizwa. Na
husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao ili kuitukana Dini. Na
lau kama wangeli sema: Tumesikia na tumet'ii, na usikie na "Undhurna"
(Utuangalie), ingeli kuwa ni kheri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu
amewalaani kwa kufuru yao; basi hawaamini ila wachache tu.
47. Enyi mlio pewa Kitabu! Aminini tuliyo yateremsha yenye
kusadikisha yale mliyo nayo, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni,
au tukawalaani
48. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo
duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika
amezua dhambi kubwa.
49. Jee huwaoni wale wanao dai kuwa ati wametakasika? Bali Mwenyezi
Mungu humtakasa amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kadiri ya kijiuzi kilichomo
ndani ya uwazi wa kokwa ya tende.
50. Tazama vipi wanavyo mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na haya
yatosha kuwa dhambi iliyo dhaahiri.
51. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini masanamu na
Shet'ani! Na wanawasema walio kufuru, kuwa hao wameongoka zaidi katika njia
kuliko Walio amini.
52. Hao ndio Mwenyezi Mungu amewalaani. Na ambaye Mwenyezi Mungu
amemlaani basi hutamwona kuwa na mwenye kumnusuru.
53. Au wanayo sehemu ya utawala? Basi hapo wasingewapa watu hata
tundu ya kokwa ya tende.
54. Au wanawahusudu watu kwa yale aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa
fadhila yake? Basi tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hikima na tukawapa
utawala mkubwa.
55. Basi wapo miongoni mwao waliyo yaamini, na wapo walio yakataa.
Na Jahannamu yatosha kuwa ni moto wa kuwateketeza.
56. Hakika wale walio zikataa Ishara zetu tutawaingiza Motoni. Kila
zitapo wiva ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyengine ili waionje hiyo adhabu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
57. Na wale walio amini na wakatenda mema tutawaingiza katika Pepo
zipitazo mito kati yake kwa kudumu humo milele. Huko watakuwa na wake walio
takasika, na tutawaingiza katika vivuli vizuri kweli.
58. Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa
wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo
kuwaidhini Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia,
Mwenye kuona.
59. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na
wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa
Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
60. Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa
kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya
upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea
mbali.
61. Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu, na njooni kwa Mtume; utawaona wanaafiki wanakukwepa kwa upinzani.
62. Basi inakuwaje unapo wasibu msiba kwa sababu ya yale iliyo
tanguliza mikono yao? Hapo tena hukujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu wakisema:
Hatukutaka ila wema na mapatano.
63. Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo ndani ya
nyoyo zao. Basi waachilie mbali, uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri
na kuingia katika nafsi zao.
64. Na hatukumtuma Mtume yeyote ila at'iiwe kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na lau pale walipo jidhulumu nafsi zao wangeli kujia, wakamwomba
Mwenyezi Mungu msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka wangeli mkuta
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
65. La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe
ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo
zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa.
66. Na lau kuwa tumewaamrisha: Jiueni, au tokeni majumbani kwenu,
wasingeli fanya hayo ila wachache tu miongoni mwao. Na lau kama wangeli fanya
walio waidhiwa ingeli kuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi.
67. Na hapo tunge wapa malipo makubwa kutoka kwetu.
68. Na tungeli waongoa Njia iliyo nyooka.
69. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale
alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na
Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!
70. Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi wa kutosha.
71. Enyi mlio amini! Chukueni hadhari yenu! Na mtoke kwa vikosi au
tokeni nyote pamoja!
72. Na yupo kati yenu anaye bakia nyuma; na ukikusibuni msiba
husema: Mwenyezi Mungu kanifanyia kheri sikuwa nao.
73. Na ikikufikieni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema - kama
kwamba hapakuwa mapenzi baina yenu naye: Laiti ningeli kuwa pamoja nao
nikafanikiwa mafanikio makubwa.
74. Basi nawapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanao
uza uhai wa dunia kwa Akhera. Na anaye pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu
kisha akauliwa au akashinda basi tutakuja mpa ujira mkubwa.
75. Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao
onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe
katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye
toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako.
76. Walio amini wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio
kufuru wanapiana katika njia ya upotofu. Basi piganeni na marafiki wa Shet'ani.
Hakika hila za Shet'ani ni dhaifu.
77. Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu, na mshike
Sala na mtoe Zaka. Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati yao
liliwaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi. Na
wakasema: Mola Mlezi wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge
tuakhirishia kiasi ya muda kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na
Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa
kokwa ya tende.
78. Popote mlipo mauti yatakufikieni, na hata mkiwa katika ngome
zilizo na nguvu. Na likiwafikilia jema wanasema: Hili limetoka kwa Mwenyezi
Mungu. Na likiwafikilia ovu wanasema: Hili limetoka kwako wewe. Sema: Yote
yanatokana na Mwenyezi Mungu. Basi wana nini watu hawa hata hawakaribii
kufahamu maneno?
79. Jema lilio kufikia limetokana na Mwenyezi Mungu. Na ovu lilio
kusibu linatokana na nafsi yako. Nasi tumekutuma kwa watu uwe ni Mtume. Na
Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kutosha.
80. Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi Mungu. Na anaye
kengeuka, basi Sisi hatukukutuma wewe uwe ni mlinzi wao.
81. Na wanasema: Tunat'ii. Lakini wanapo toka kwako kundi moja
miongoni mwao hupanga njama usiku kinyume na unayo yasema. Na Mwenyezi Mungu
anayaandika yote hayo wanayo yapangia njama za usiku. Basi waachilie mbali, na
umtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.
82. Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye
kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu
nyingi.
83. Na linapo wafikia jambo lolote lilio khusu amani au la kitisho
wao hulitangaza. Na lau kuwa wangeli lipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka
kati yao, wale wanao chunguza wangeli lijua. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi
Mungu juu yenu na rehema yake mngeli mfuata Shet'ani ila wachache wenu tu.
84. Basi pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Hukalifishwi ila
nafsi yako tu. Na wahimize Waumini. Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulio
ya walio kufuru. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mkali zaidi wa kushambulia na Mkali
zaidi wa kuadhibu.
85. Mwenye kusaidia msaada mwema ana fungu lake katika hayo, na
mwenye kusaidia msaada mwovu naye ana sehemu yake katika hayo. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza na ujuzi juu ya kila kitu.
86. Na mnapo amkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa
yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuhisabu kila kitu.
87. Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Kwa yakini
atakukusanyeni Siku ya Kiyama. Halina shaka hilo. Na ni nani msema kweli kuliko
Mwenyezi Mungu?
88. Mmekuwaje kuwa makundi mawili kwa khabari ya wanaafiki, na hali
Mwenyezi Mungu amewageuza kwa sababu ya yale waliyo yachuma? Je! Mnataka
kumwona mwongofu ambaye Mwenyezi Mungu amemhukumu kuwa kapotea? Na aliye
mhukumu Mwenyezi Mungu kuwa amekwisha potea wewe hutampatia njia.
89. Wanapenda lau kuwa nanyi mnge kufuru kama walivyo kufuru wao,
ili muwe sawa sawa. Basi msiwafanye marafiki miongoni mwao mpaka wahame kwa
ajili ya Dini ya Mwenyezi Mungu. Na wakikengeuka basi wakamateni na wauweni
popote mnapo wapata. Wala msimfanye rafiki katika wao wala msaidizi.
90. Isipokuwa wale walio fungamana na watu ambao mna ahadi baina
yenu na wao, au wanakujieni na vifua vyao vina dhiki kupigana nanyi, au
kupigana na watu wao. Na lau angeli penda Mwenyezi Mungu angeli wasaliti juu
yenu wakapigana nanyi. Basi wakijitenga nanyi, wasipigane nanyi, na
wakakuleteeni amani, basi Mwenyezi Mungu hakukupeni njia kupigana nao.
91. Mtawakuta wengine wanataka wapate salama kwenu na salama kwa
watu wao. Kila wakirudishwa kwenye fitna hudidimizwa humo. Ikiwa hawajitengi
nanyi, na wakakuleteeni salama, na wakazuia mikono yao, basi wakamateni na
wauweni popote mnapo wakuta. Na juu ya hao ndio tumekupeni hoja zilizo
wazi.
92. Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye
kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya
kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni
jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye
Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi
wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge
miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi na Mwenye hikima.
93. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni
Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na
amemuandalia adhabu kubwa.
94. Enyi mlio amini! Mnapo safiri katika Njia ya Mwenyezi Mungu basi
hakikisheni, wala msimwambie anaye kutoleeni salamu: Wewe si Muumini; kwa
kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi Mungu zipo
ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyo kuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi Mungu
akakuneemesheni. Basi chunguzeni sawa sawa. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari
za mnayo yatenda.
95. Hawawi sawa Waumini wanao kaa tu wala hawanadharura, na wale
wanao pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyezi
Mungu amewatukuza cheo wale wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao kuliko wale
wanao kaa tu. Ingawa Mwenyezi Mungu amewaahidi wote mashukio mema, lakini
Mwenyezi Mungu amewafadhili wanao pigana kwa ujira mkubwa kuliko wanao kaa
tu.
96. Ni vyeo hivyo vinavyo toka kwake, na maghfira na rehema. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye kurehemu.
97. Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha nao
wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa.
Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo?
Basi hao makaazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa.
98. Isipo kuwa wale walio kuwa wanyonge miongoni mwa wanaume na
wanawake na watoto wasio na uweza wa hila ya kuongoza njia ya kuhama.
99. Basi hao huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa maghfira.
100. Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu atapata pengi
duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anaye toka nyumbani kwake kuhama
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti njiani basi
umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
maghfira na Mwenye kurehemu.
101. Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha
Sala, iwapo mnachelea wasije wale walio kufuru wakakuleteeni maudhi. Hakika
makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.
102. Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi moja miongoni
mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida
zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali, lisali
pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru wanapenda
mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja.
Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa,
mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu
amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
103. Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa,
na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni Sala kama dasturi.
Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu.
104. Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui. Ikiwa
mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji kwa
Mwenyezi Mungu wasio yataraji wao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye
hikima.
105. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki ili upate
kuhukumu baina ya watu kwa alivyo kuonyesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe mtetezi
wa makhaaini.
106. Na muombe maghfira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
107. Wala usiwatetee wanao khini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu
hampendi aliye khaaini, mwenye dhambi.
108. Wanataka kujificha kwa watu, wala hawataki kujificha kwa
Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao pale wanapo panga njama usiku kwa maneno
asiyo yapenda. Na Mwenyezi Mungu anayajua vyema wanayo yatenda.
109. Hivyo nyinyi mmewatetea hawa katika uhai huu wa duniani. Basi
nani atakaye watetea kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama? Au ni nani atakuwa
wakili wao wa kumtegemea?
110. Na anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba
maghfira kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira,
Mwenye kurehemu.
111. Na anaye chuma dhambi, basi ameichumia nafsi yake mwenyewe. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.
112. Na atendaye kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye na kosa,
basi amejitwika dhulma na dhambi iliyo wazi.
113. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema
yake, kundi moja kati yao linge dhamiria kukupoteza. Wala hawapotezi ila nafsi
zao, wala hawawezi kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia
Kitabu na hikima na amekufundisha uliyo kuwa huyajui. Na fadhila za Mwenyezi
Mungu zilizo juu yako ni kubwa.
114. Hakuna kheri katika mengi ya wanayo shauriana kwa siri, isipo
kuwa kwa yule anaye amrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina
ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi
tutakuja mpa ujira mkubwa.
115. Na anaye mpinga Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu, na
akafuata njia isiyo kuwa ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na
tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu.
116. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na kitu. Lakini
Yeye husamehe yasiyo kuwa hayo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi
Mungu basi huyo amepotea upotovu wa mbali.
117. Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala hawamuombi
ila Shet'ani aliye asi.
118. Mwenyezi Mungu amemlaani. Naye Shet'ani alisema: Kwa yakini
nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako.
119. Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha,
basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyo umba
Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni mlinzi wake badala ya
Mwenyezi Mungu, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri.
120. Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shet'ani hawaahidi ila
udanganyifu.
121. Hao makao yao ni Jahannamu, na wala hawapati makimbilio kutoka
humo.
122. Na wale walio amini na wakatenda mema, tutawaingiza katika
Bustani zipitayo mito kati yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi
Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu.
123. Si kwa matamanio yenu, wala matamanio ya Watu wa Kitabu! Anaye
fanya ubaya atalipwa kwalo, wala hatajipatia mlinzi wala wa kumnusuru, isipo
kuwa Mwenyezi Mungu.
124. Na anaye fanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni
Muumini - basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu
ya kokwa ya tende.
125. Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliye usilimisha uso
wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa mwema, na anafuata mila ya Ibrahim
mwongofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwendani.
126. Ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo
duniani. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuvizunguka vitu vyote.
127. Wanakuuliza nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu ana
kutoleeni fatwa juu yao, na mnayo somewa humu Kitabuni kukhusu mayatima
wanawake ambao hamwapi walicho andikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu
wanyonge katika watoto, na kwamba mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na kheri
yoyote mnayo fanya Mwenyezi Mungu anaijua.
128. Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si
vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa
machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika
Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
129. Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia.
Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojapo) kama aliye tundikwa. Na
mkisikizana na mkamchamngu basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye
kurehemu.
130. Na wakitengana Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja katika
wao kwa ukunjufu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu Mwenye hikima.
131. Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote viliomo katik mbingu na
viliomo katika dunia. Na kwa hakika tuliwausia walio pewa Kitabu kabla yenu, na
nyinyi pia, kwamba mumche Mwenyezi Mungu. Na mkikataa, basi ni vya Mwenyezi
Mungu viliomo mbinguni na viliomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi,
anajitosha, na Msifiwa.
132. Na ni vya Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na viliomo katika
ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi.
133. Akitaka atakuondoeni, enyi watu! Na awalete wengineo. Na
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa hayo.
134. Anaye taka malipo ya dunia, basi kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo
ya dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
135. Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili
na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu anawastahikia zaidi.
Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkajitenga
nao basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayo yatenda.
136. Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na
Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha kabla
yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na
Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali.
137. Hakika walio amini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha
wakazidi ukafiri, Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaghufiria wala wa kuwaongoa
njia.
138. Wabashirie wanaafiki kwamba watapata adhabu chungu,
139. Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki badala ya
Waumini. Je! Wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa
Mwenyezi Mungu.
140. Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya kwamba mnapo
sikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli, basi msikae
pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa nanyi mfano
wao hao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanaafiki na makafiri wote pamoja
katika Jahannamu,
141. Wale ambao wanakungojeeni, mkipata ushindi unao toka kwa
Mwenyezi Mungu wao husema: Si tulikuwa pamoja nanyi vile? Na ikiwa ni sehemu ya
makafiri kushinda wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kukushindeni, nasi
tukakukingeni na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya
Kiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.
142. Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na hali ni Yeye
ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa unyong'onyo,
wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.
143. Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na huko
hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompatia
njia.
144. Enyi mlio amini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio marafiki badala
ya Waumini. Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyo wazi juu yenu?
145. Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini kabisa Motoni,
wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.
146. Isipo kuwa wale walio tubu, na wakatengeneza na wakashikamana na
Mwenyezi Mungu, na wakamtakasia Dini yao Mwenyezi Mungu. Basi hao ni pamoja na
Waumini. Na Mwenyezi Mungu atakuja wapa Waumini ujira mkubwa.
147. Mwenyezi Mungu hakuadhibuni mkimshukuru na mkamuamini. Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea shukrani na ndiye Mwenye kujua.