Part 8
111. NA LAU kuwa tungeli wateremshia Malaika, na maiti wakazungumza
nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, bado wasingeli amini, ila Mwenyezi
Mungu atake. Lakini wengi wao wamo ujingani.
112. Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashet'ani wa
kiwatu, na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba-pamba, kwa
udanganyifu. Na angeli penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya hayo. Basi waache
na wanayo yazua.
113. Na ili nyoyo za wasio amini Akhera zielekee hayo, nao wayaridhie
na wayachume wanayo yachuma.
114. Je, nimtafute hakimu ghairi ya Mwenyezi Mungu, naye ndiye aliye
kuteremshieni Kitabu kilicho elezwa waziwazi? Na hao tulio wapa Kitabu wanajua
ya kwamba kimeteremshwa na Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi usiwe katika wanao
tia shaka.
115. Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu.
Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na
Mwenye kujua.
116. Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia
ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema
uwongo tu.
117. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio
potea Njia yake, na ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio hidika.
118. Basi kuleni katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu, ikiwa
mnaziamini Aya zake.
119. Na kwa nini msile katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu,
naye amekwisha kubainishieni alivyo kuharimishieni, isipo kuwa vile mnavyo
lazimishwa? Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya kuwa na ilimu.
Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua wanao pindukia
mipaka.
120. Na acheni dhambi zilizo dhaahiri na zilizo fichikana. Hakika
wanao chuma dhambi watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
121. Wala msile katika wale wasio somewa jina la Mwenyezi Mungu.
Kwani huo ni upotofu. Na kwa yakini mashet'ani wanawafunza marafiki zao
kubishana nanyi. Na mkiwafuata basi hapana shaka nyinyi mtakuwa
washirikina.
122. Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru
inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani akawa hata
hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa
wakiyafanya.
123. Kadhaalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa wakosefu wao
wafanye vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa nafsi zao,
nao hawatambui.
124. Na inapo wajia Ishara, wao husema: Hatutoamini mpaka tupewe
mfano wa walio pewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko
wote kujua wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao walio kosa udhalili na
adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo kuwa
wakivifanya.
125. Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi humfungulia
kifua chake kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake kina dhiki,
kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia
uchafu juu ya wasio amini.
126. Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka.
Tumezipambanua Aya kwa watu wanao kumbuka.
127. Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye
Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda.
128. Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi makundi ya
majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na marafiki zao
katika wanaadamu waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Na
tumefikia ukomo wetu ulio tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto ndio
makaazi yenu, mtadumu humo, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako
Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua.
129. Ndio kama hivi tunawaelekeza madhaalimu wapendane wao kwa wao
kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma.
130. Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni Mitume
kutokana na nyinyi wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni mkutano
wa Siku yenu hii. Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na
yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa
makafiri.
131. Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa wa kuiangamiza
miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika.
132. Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale waliyo yatenda.
Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
133. Na Mola wako Mlezi ndiye Mkwasi, Mwenye rehema. Akipenda
atakuondoeni na awaweke wengine awapendao badala yenu, kama vile alivyo kutoeni
kutokana na uzazi wa watu wengine.
134. Bila ya shaka hayo mnayo ahidiwa yatafika tu, wala nyinyi
hamtaweza kuyaepuka.
135. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezayo, na hakika mimi nafanya.
Mtakuja jua nani atakuwa na makaazi mema mwishoni. Hakika madhaalimu
hawatafanikiwa.
136. Na wamemwekea sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea na wanyama alio
umba, nao husema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai
137. Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika
washirikina kuwauwa watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao. Na lau
kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo wanayo
yazua.
138. Nao husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko. Hawatokula ila
wale tuwapendao - kwa madai yao tu. Na wanyama hawa imeharimishwa migongo yao
kupandwa. Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao.
Wanamzulia uwongo tu Mwenyezi Mungu. Atawalipa kwa hayo wanayo mzulia.
139. Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya
wanaume wetu tu, na wameharimishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa nyamafu basi
wanashirikiana. Mwenyezi Mungu atawalipa kwa maelezo yao hayo. Hakika Yeye ni
Mwenye hikima, Mwenye kujua.
140. Hakika wamekhasirika wale ambao wamewauwa watoto wao kwa upumbavu
pasipo kujua, na wakaharimisha alivyo waruzuku Mwenyezi Mungu kwa kumzulia
Mwenyezi Mungu. Hakika wamepotea, wala hawakuwa wenye kuongoka.
141. Na Yeye ndiye aliye ziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja,
na zisio tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali, na mizaituni
na mikomamanga inayo fanana na isiyo fanana. Kuleni matunda yake inapo zaa, na
toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye
hawapendi watumiayo kwa fujo.
142. Na katika wanyama amekujaalieni wenye kubeba mizigo na kutoa
matandiko. Kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, wala msifuate nyayo
za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu dhaahiri.
143. Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika kondoo, na
wawili katika mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili,
au waliomo matumboni mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi
mnasema kweli.
144. Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je, ameharimisha
yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa yote majike? Au,
nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya? Basi ni nani dhaalimu
mkubwa kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa ajili ya kuwapoteza
watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi watu madhaalimu.
145. Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho
harimishwa kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika,
au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina
la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya
kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
146. Na wale walio fuata dini ya Kiyahudi tumewaharimishia kila
mwenye kucha. Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi tumewaharimishia shahamu
yao, isipo kuwa ile iliyo beba migongo yao au matumbo yao, au iliyo gandamana
na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na bila ya shaka Sisi ndio
wasema kweli.
147. Wakikukanusha basi wewe sema: Mola Mlezi wenu ni Mwenye rehema
iliyo enea. Wala haizuiliki adhabu yake kwa watu wakhalifu.
148. Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu ange taka
tusingeli shiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu chochote.
Vivi hivi walikanusha walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu yetu. Sema:
Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila
uwongo tu.
149. Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya kukata. Na kama
angeli penda angeli kuhidini nyote.
150. Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa Mwenyezi Mungu
ameharimisha hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja nao. Wala
usifuate matamanio ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini Akhera, na
ambao wanamlinganisha Mola Mlezi wao na wengine.
151. Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi.
Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema.
Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi
na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayo onekana, na yanayo fichikana.
Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa
haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini.
152. Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa,
mpaka afikilie utu-uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu. Sisi
hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo semeni kwa uadilifu
ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo amekuusieni ili mpate
kukumbuka.
153. Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni,
wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni ili
mpate kuchamngu.
154. Tena tulimpa Musa Kitabu kwa kumtimizia (neema) aliye fanya
wema, na kuwa ni maelezo ya kila kitu, na uwongofu na rehema, ili wapate
kuamini mkutano wao na Mola wao Mlezi.
155. Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa. Basi
kifuateni, na mchenimngu, ili mrehemewe.
156. Msije mkasema: Hakika mataifa mawili kabla yetu yameteremshiwa
Kitabu; na sisi tulikuwa hatuna khabari ya waliyo kuwa wakiyasoma.
157. Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungeli kuwa
waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu Mlezi,
na uwongofu, na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye
kanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wanao jitenga
na Ishara zetu adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga kwao.
158. Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au awafikie Mola wako
Mlezi, au zifike baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku zitakapo fika baadhi
ya Ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa
ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake. Sema: Ngojeni, nasi
pia tunangoja.
159. Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna
ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha
atawaambia yale waliyo kuwa wakiyatenda.
160. Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya
hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa.
161. Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia
Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye kuwa
mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
162. Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa
kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
163. Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa
kwanza wa Waislamu.
164. Sema: Je nitafute Mola Mlezi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na hali
Yeye ndiye Mola Mlezi wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na
habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu
Mlezi, naye atakuambieni mliyo kuwa mkikhitalifiana.
165. Naye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na amewanyanyua
baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa hayo aliyo
kupeni. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu
7 - AL - A'RAAF
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. ALIF LAM MYM 'SAAD
2. Kitabu kilicho teremshwa kwako - basi isiwe dhiki kifuani kwako
kwa ajili yake, upate kuonya kwacho, na kiwe ni ukumbusho kwa Waumini.
3. Fuateni mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala
msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake. Ni machache mnayo
yakumbuka.
4. Na miji mingapi tuliiangamiza, ikaifikia adhabu yetu usiku au
walipo kuwa wamelala adhuhuri.
5. Basi hakikuwa kilio chao ilipo wafikia adhabu yetu, isipo kuwa
kusema: Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu.
6. Na kwa yakini tutawauliza wale walio pelekewa Ujumbe, na pia
tutawauliza hao Wajumbe.
7. Tena tutawasimulia kwa ilimu; wala Sisi hatukuwa mbali.
8. Na Siku hiyo kipimo kitakuwa kwa Haki. Basi watakao kuwa na
uzani mzito, hao ndio watakao fanikiwa.
9. Na watakao kuwa na uzani khafifu, basi hao ndio walio zitia
khasarani nafsi zao kwa sababu ya kuzipinga Ishara zetu.
10. Na hakika tumekuwekeni katika ardhi, na tumekujaalieni humo njia
za kupatia maisha. Ni kuchache kushukuru kwenu.
11. Na hakika tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha
tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam. Basi wakasujudu isipo kuwa Iblisi, hakuwa
miongoni mwa walio sujudu.
12. Mwenyezi Mungu akasema: Nini kilicho kuzuia kumsujudia nilipo
kuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye
umemuumba kwa udongo.
13. Akasema: Basi teremka kutoka humo! Haikufalii kufanya kiburi humo.
Basi toka! Hakika wewe u miongoni mwa walio duni.
14. Akasema: Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa.
15. Akasema: Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula.
16. Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika
Njia yako Iliyo Nyooka.
17. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na
kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani.
18. Akasema: Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha fukuzwa.
Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi
nyote.
19. Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni
humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu.
20. Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo
fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa
Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele.
21. Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao
kunasihini.
22. Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao
zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi
akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui
yenu wa dhaahiri?
23. Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama
hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.
24. Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui. Na kwenye
ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.
25. Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo
mtatolewa.
26. Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na
nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi
Mungu mpate kukumbuka.
27. Eny wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama alivyo watoa wazazi
wenu Peponi, akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila yake
wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashet'ani kuwa ni
marafiki wa wasio amini.
28. Na wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu,
na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi
mambo machafu. Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua?
29. Sema: Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu, na mumuelekeze nyuso
zenu kila mnapo sujudu, na muombeni Yeye kwa kumsafia Dini. Kama alivyo
kuumbeni mwanzo ndivyo mtavyo rudi,
30. Hali ya kuwa kundi moja amelihidi, na kundi jengine
limethibitikiwa na upotofu. Kwa hakika hao waliwafanya mashet'ani kuwa ndio
marafiki walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka.
31. Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa
ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye
hapendi wanao fanya israfu.
32. Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo
watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio
amini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna
hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua.
33. Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na
ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na
asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua.
34. Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi
hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia.
35. Enyi wanaadamu! Watakapo kufikieni Mitume miongoni mwenu
wakakuelezeni Ishara zangu, basi watakao mchamngu na wakatengenea haitakuwa
khofu kwao, wala hawatahuzunika.
36. Na wale watakao kanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao
ni watu wa Motoni; humo watadumu.
37. Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi
Mungu uwongo, au anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia sehemu yao waliyo
andikiwa, mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi
mlio kuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na
watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri.
38. Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo
pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake.
Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao:
Mola wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu.
Atasema: Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
39. Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi nyinyi pia
hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyo kuwa
mkiyachuma.
40. Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi
hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia
katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu.
41. Jahannamu itakuwa kitanda chao na juu yao nguo za moto za
kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
42. Na wale wanao amini na wakatenda mema - hatumkalifishi mtu
yoyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa Peponi. Wao watadumu
humo.
43. Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele
44. Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta
aliyo tuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo
kuahidini Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji
atawatangazia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu,
45. Wale ambao walikuwa wakizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na
wakataka kuipotosha, nao wanaikanusha Akhera.
46. Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na juu ya
Mnyanyuko patakuwa watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao watawaita watu
wa Peponi: Assalamu Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado hawajaingia humo, lakini
wanatumai.
47. Na yanapo geuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni, watasema:
Mola Mlezi wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu walio dhulumu.
48. Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa alama
zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho mlicho kuwa
mnafanyia kiburi.
49. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi Mungu
hatawafikishia rehema. Ingieni Peponi, hapana khofu kwenu, wala
hamtahuzunika!
50. Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumimieni maji, au
chochote alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika Mwenyezi Mungu
ameviharimisha hivyo kwa makafiri,
51. Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo, na maisha ya
dunia yakawadanganya. Basi leo Sisi tunawasahau kama walivyo usahau mkutano wa
Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu.
52. Na hakika tumewaletea Kitabu tulicho kipambanua kwa ilimu,
uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini.
53. Je, lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake? Siku yatapo
fika matokeo yake watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu
walileta Haki! Je, tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye
yasiyo kuwa yale tuliyo kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri nafsi
zao, na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua.
54. Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na
ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku
kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa
amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wa viumbe vyote.
55. Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika
Yeye hawapendi warukao mipaka.
56. Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha
tengenezwa. Na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi
Mungu iko karibu na wanao fanya mema.
57. Na Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara
kabla ya kufika rehema yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito
tunayachunga mpaka kwenye nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio
kama hivyo tukatolesha kila aina ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo
wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.
58. Na ardhi njema, yenye udongo wa rutba, hutoa mimea yenye kukua
vizuri yenye uhai, kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Na ardhi mbaya haitoi ila
mimea michache, isiyo na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo tunavyo
zipambanua Ishara (Aya) kwa watu wanao shukuru.
59. Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi kaumu yangu!
Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi
ninakukhofieni adhabu ya Siku iliyo kuu.
60. Wale watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika sisi tunakuona
wewe umo katika upotofu ulio dhaahiri.
61. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu, lakini mimi
ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
62. Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninakunasihini; na
ninayajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
63. Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi
wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na ili
mumchemngu, na ili mpate kurehemewa?
64. Basi walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja
naye katika jahazi. Na tukawazamisha wale walio kanusha Ishara zetu. Hakika hao
walikuwa watu vipofu.
65. Na kwa A'adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema: Enyi watu
wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je,
hamumchi?
66. Wakasema watukufu wa wale walio kufuru katika kaumu yake: Sisi
tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe ni katika
waongo.
67. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni
Mtume niliye toka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
68. Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni
mwenye kukunasihini, muaminifu.
69. Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu
Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo kufanyeni
mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi zikumbukeni
neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
70. Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake,
na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi,
ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
71. Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha
kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina
tu mliyo yaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha
uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja.
72. Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye kwa rehema zetu,
na tukakata mizizi ya wale walio zikanusha Ishara zetu, na hawakuwa wenye
kuamini.
73. Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu
wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha
kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike
wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya
Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu.
74. Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na
akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake,
na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu
wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi.
75. Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa
wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola
Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa.
76. Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo
yaamini.
77. Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na
wakasema: Ewe Saleh! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa
Mitume.
78. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa
majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa.
79. Basi Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu!
Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi
hamwapendi wenye nasaha.
80. Na tulimtuma Lut', alipo waambia watu wake: Je, mnafanya uchafu
ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote!
81. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkwawacha
wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji!
82. Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipo kuwa kuambizana:
Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanao jitakasa.
83. Basi tukamwokoa yeye na watu wake, isipo kuwa mkewe, alikuwa
miongoni mwa walio bakia nyuma.
84. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyo kuwa mwisho wa
wakosefu.
85. Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu
86. Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na kuwazuilia na
Njia ya Mwenyezi Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia ipotoke. Na
kumbukeni mlipo kuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na tazameni jinsi
ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi.
87. Na kama liko kundi miongoni mwenu lililo amini haya niliyo
tumwa, na kundi jengine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu
baina yetu. Naye ndiye Mbora wa wenye kuhukumu.