17 - AL ISRAAI (BANI ISRAIL)
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti
Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili
tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye
kuona.
2. Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa
Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi!
3. Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa
mja mwenye shukrani.
4. Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi
mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi
kikubwa.
5. Basi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni waja wetu
wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa ahadi iliyo
timizwa.
6. Kisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na tukakusaidieni
kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi.
7. Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya
ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso
zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila
walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa.
8. Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi
tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri.
9. Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na
inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo
makubwa.
10. Na yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia adhabu
chungu.
11. Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani
mwanaadamu ni mwenye pupa.
12. Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta
ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute
fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu.
Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.
13. Na kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake. Na Siku ya
Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa.
14. Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu.
15. Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye
potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa
mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume.
16. Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe
na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti
juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.
17. Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi
anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake.
18. Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa
hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo
hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa.
19. Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali zake, naye
ni Muumini, basi hao juhudi
20. Wote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika neema za Mola
wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki. *
21. Angalia vipi tulivyo wafadhili baadhi
22. Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukawa
wa kulaumiwa uliye tupika.
23. Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye
tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako,
au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa
msemo wa hishima.
24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na
useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.
25. Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa nyinyi
mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake.
26. Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala
usitumie ovyo kwa fujo.
27. Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye
kumkufuru Mola wake Mlezi.
28. Na ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta rehema ya Mola wako
Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini.
29. Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala
usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi.
30. Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye.
Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona.
31. Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku
wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa.
32. Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.
33. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa
haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini
asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa.
34. Wala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa kwa njia iliyo
bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi
itasailiwa.
35. Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa.
Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndio bora.
36. Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho,
na moyo - hivyo vyote vitasailiwa.
37. Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi
kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.
38. Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako
Mlezi.
39. Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala
usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika
Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa.
40. Je! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana, na Yeye akawafanya
Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi mkubwa.
41. Na tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii ili wapate kukumbuka.
Lakini haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo.
42. Sema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu mingine kama
wasemavyo, basi wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi.
43. Subhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka juu kabisa na hayo
wanayo yasema.
44. Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani
yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu
kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira.
45. Na unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako na wale wasio iamini
Akhera pazia linalo wafunika.
46. Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka
kwenye masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke
yake, basi wao hugeuka nyuma wakenda zao.
47. Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo
kusikiliza, na wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati
isipo kuwa mtu aliye rogwa.
48. Tazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea. Kwa hivyo
hawawezi kuipata njia.
49. Na walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika,
tutafufuliwa kwa umbo jipya?
50. Sema: Kuweni hata mawe na chuma.
51. Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua vyenu. Watasema:
Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza!
Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa
karibu!
52. Siku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia kwa kumshukuru, na
mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mdogo tu.
53. Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet'ani
huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa
mwanaadamu.
54. Mola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda atakurehemuni, na
akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao.
55. Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika
ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi
tulimpa Zaburi.
56. Sema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake Yeye. Hawawezi
kukuondoleeni madhara, wala kuyaweka pengine.
57. Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola
wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji rehema zake na
wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari
nayo.
58. Na hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza kabla ya Siku ya
Kiyama, au tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa katika Kitabu.
59. Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa
zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo
dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya
kuhadharisha.
60. Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka
hao watu. Na hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti
ulio laaniwa katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi
mkubwa.
61. Na pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam. Wakamsujudia
isipo kuwa Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba kwa udongo?
62. Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza juu yangu.
Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza dhuriya zake
wasipo kuwa wachache tu.
63. Akasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali! Atakaye kufuata katika
wao, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo ya kutimia.
64. Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie
jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika
mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.
65. Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi
anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
66. Mola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni marikebu katika bahari
ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kukurehemuni
nyinyi.
67. Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba
wanapotea, isipo kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka.
Ama mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha.
68. Je! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni upande wowote katika
nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto? Kisha msipate wa
kumtegemea.
69. Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na
kukupelekeeni kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha
msipate wa kukunusuruni nasi.
70. Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi
kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa
fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba.
71. Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa
wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao
watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.
72. Na aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na
atakuwa aliye ipotea zaidi Njia.
73. Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili
utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki.
74. Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia kuwaelekea
kidogo.
75. Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya
uhai, na adhabu mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu wa kukunusuru nasi.
76. Na walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na hapo wao wasingeli
bakia humo ila kwa muda mchache tu.
77. Huo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla yako. Wala hupati
mabadiliko katika mwendo wetu.
78. Shika Sala jua linapo pinduka mpaka giza la usiku, na Qur'ani ya
al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa daima.
79. Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe.
Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika.
80. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema, na unitoe
kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie.
81. Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo
lazima utoweke!
82. Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa
Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara.
83. Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga kando. Na
inapo mgusa shari hukata tamaa.
84. Sema: Kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu Mlezi
anajua aliye ongoka katika njia.
85. Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola
wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu.
86. Na tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia. Kisha
usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya.
87. Isipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika
fadhila yake kwako ni kubwa.
88. Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii
Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.
89. Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano.
Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu.
90. Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika
ardhi hii.
91. Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na utupitishie mito
kati yake ikimiminika.
92. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee
Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso.
93. Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala hatutaamini
kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi,
Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na
Mtume?
94. Na nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo wajia uwongofu isipo
kuwa walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu kuwa ni Mtume?
95. Sema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea kwa utulivu
wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni Mtume wao.
96. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na
nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
97. Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye hidika. Na
anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya Siku ya
Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na
makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake
kwa nguvu.
98. Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na
wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa
umbo jipya?
99. Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na
ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio na shaka
yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri.
100. Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola
wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na
mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo!
101. Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize Wana
wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi nakuona wewe Musa
umerogwa!
102. Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha
ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika
mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia.
103. Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo
tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote.
104. Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi.
Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja.
105. Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka. Na
hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji.
106. Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa
kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.
107. Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla
yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu.
108. Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu Mlezi!
Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe!
109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha
unyenyekevu.
110. Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni Rahman
(Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina mazuri
mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa sauti
ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo.
111. Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye
hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa kumsaidia kwa
sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa.