24 - AN - NUR
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. HII NI SURA Tuliyo iteremsha na
tukailazimisha; tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.
2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni
huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu,
ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu
3. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke
mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina.
Na hayo yameharimishwa kwa Waumini.
4. Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi
wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na
hao ndio wapotovu.
5. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani
bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
6. Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao,
basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi
Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
7. Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake
ikiwa ni miongoni mwa waongo.
8. Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo
cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo.
9. Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu
yake
10. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema
yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba....
11. Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri
ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo
yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao,
atapata adhabu kubwa.
12. Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake
Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
13. Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta
mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
14. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake
katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu
ya yale mliyo jiingiza.
15. Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo
yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa.
16. Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya.
Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!
17. Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya
kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!
18. Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye hikima.
19. Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini,
watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na
nyinyi hamjui.
20. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema
yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu....
21. Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata
nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila
ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu
kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
22. Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa
jamaa zao na masikini na walio
23. Hakika wanao wasingizia wanawake, wanao jihishimu, walio
ghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu
kubwa.
24. Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono
25. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki,
na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi.
26. Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa
wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa
wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na
riziki ya ukarimu.
27. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe
ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka.
28. Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na
mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu
anajua mnayo yatenda.
29. Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisio kaliwa ambazo ndani yake
yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yadhihirisha na mnayo
yaficha.
30. Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu
zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayo
yafanya.
31. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde
tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe
shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au
baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka
zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo
wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto
ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili
yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi
Waumini, ili mpate kufanikiwa.
32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na
wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.
33. Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka
Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru
katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama
mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala
msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la
maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi
Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
34. Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na mifano
kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu.
35. Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni
kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile
ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti
ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta
yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu
humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
36. Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na
humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni
37. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru
Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na
macho yatageuka.
38. Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo yatenda, na
awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya
hisabu.
39. Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani.
Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta
Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwepesi wa kuhisabu.
40. Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu
ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake
anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na
nuru.
41. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika
mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala
yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua
wayatendayo.
42. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa
Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya wote.
43. Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha
huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na
huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo
amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua
macho.
44. Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo
yapo mazingatio kwa wenye kuona.
45. Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine
katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na
wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu.
46. Kwa yakini tumeteremsha Ishara zinazo bainisha. Na Mwenyezi
Mungu hummwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
47. Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tumet'ii.
Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini.
48. Na wanapo itwa kumuendea Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili
ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa.
49. Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kut'ii.
50. Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au
wanaogopa ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu?
51. Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume
wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio
wenye kufanikiwa.
52. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa
Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.
53. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba
ukiwaamrisha kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
54. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka,
basi yaliyo juu yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa
nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe
wazi wazi.
55. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na
wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya
makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo
wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi,
wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio
wapotovu.
56. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate
kurehemewa.
57. Msiwadhanie walio kufuru kwamba watashinda katika nchi. Na
makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo yao.
58. Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu
ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya
alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha.
Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya
nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu
anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
59. Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake
ruhusa, kama walivyo taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo
kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye
hikima.
60. Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza
nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
61. Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya
kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba
zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu,
au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu,
au nyumba za dada wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu.
Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba,
toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka
na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate
kuelewa.
62. Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume
wake; na wanapo kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka
wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao,
mruhusu umtakaye miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu.
63. Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa
nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho.
Basi nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata
adhabu chungu.
64. Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na
ardhini. Hakika Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza
waliyo yafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.