25 - AL - FURQAN
KWA JINA
LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji
kwa walimwengu wote.
2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana,
wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa
kipimo.
3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali
hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki
mauti, wala uhai, wala kufufuka.
4. Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio
uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na
uwongo.
5. Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha,
anavyo somewa asubuhi na jioni.
6. Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi.
Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea
masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?
8. Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika
hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa.
9. Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala
hawataiweza Njia.
10. Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo,
nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari.
11.
12. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake
na mngurumo wake.
13. Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba
wafe.
14. Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!
15. Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa
wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?
16. Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya
Mola wako Mlezi, inayo ombwa.
17. Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema:
Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea
njia?
18. Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi
kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao
hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia.
19. Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi
kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha
adhabu kubwa.
20. Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na
yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi
yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye
kuona.
21. NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi
hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona
bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno!
22. Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu.
Na watasema: Mungu apishe mbali!
23. Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao,
tuvifanye
24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali
penye starehe nzuri.
25. Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe
Malaika kwa wingi,
26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema,
na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
27. Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku
anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume!
28. Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!
29. Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli
Shet'ani ni khaini kwa mwanaadamu.
30. Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu
wameifanya hii Qur'ani ni kihame.
31. Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu,
na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.
32. Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani kwa
jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa
mafungu.
33. Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea
(jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora.
34. Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye
Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia.
35. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye,
Harun, kuwa waziri.
36. Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi
tukawateketeza kabisa.
37. Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na
tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu
chungu.
38. Na tuliwaangamiza kina A'di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi
vingi vilivyo kuwa kati yao.
39. Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa
kabisa.
40. Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua
mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.
41. Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema):
Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume?
42. Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli
kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona
adhabu, ni nani aliye potea njia.
43. Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake?
Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?
44. Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao
hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.
45. Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na
angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi
wake.
46. Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.
47. Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa
mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka.
48. Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema
yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi.
49. Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na
watu wengi tulio waumba.
50. Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu
wengi wanakataa ila kukufuru.
51. Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji.
52. Basi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa.
53. Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya
chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.
54. Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia
kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza.
55. Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo
wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi.
56. Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji.
57. Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia
iendayo kwa Mola wake Mlezi.
58. Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake.
Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.
59. Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku
sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari
zake kwa wamjuaye.
60. Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani
Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki.
61. Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa
na mwezi unao ng'ara.
62. Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya
anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru.
63. Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni
kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
64. Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na
kusimama.
65. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya
Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi.
66. Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya.
67. Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi
ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.
68. Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu,
wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala
hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara,
69. Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa
kufedheheka.
70. Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema.
Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
71. Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli
kweli kwa Mwenyezi Mungu.
72. Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo
penye upuuzi, hupita kwa hishima yao.
73. Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi
hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu.
74. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na
wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.
75. Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na
watakuta humo maamkio na salamu.
76. Wadumu humo - kituo na makao mazuri kabisa.
77. Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu.
Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.