26 - ASH-SHUA'RAA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. T'aa Siin Miim. (T'.S.M.) 

2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. 

3. Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini. 

4. Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao. 

5. Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao. 

6. Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. 

7. Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri? 

8. Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. 

9. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

10. Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu, 

11. Watu wa Firauni. Hawaogopi? 

12. Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe. 

13. Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun. 

14. Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa. 

15. Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza. 

16. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

17. Waachilie Wana wa Israili wende nasi. 

18. (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? 

19. Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani? 

20. (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea. 

21. Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume. 

22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili? 

23. Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote? 

24. Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini. 

25. (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi? 

26. (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza. 

27. (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu. 

28. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini. 

29. (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani. 

30. Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi? 

31. Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli. 

32. Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. 

33. Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao. 

34. (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu. 

35. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani? 

36. Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo. 

37. Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu. 

38. Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu. 

39. Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika? 

40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda. 

41. Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda? 

42. Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele. 

43. Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa. 

44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda. 

45. Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua. 

46. Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. 

47. Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

48. Mola Mlezi wa Musa na Harun. 

49. (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote. 

50. Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. 

51. Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini. 

52. Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa. 

53. Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo. 

54. (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo. 

55. Nao wanatuudhi. 

56. Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari. 

57. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, 

58. Na makhazina, na vyeo vya hishima, 

59. Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili. 

60. Basi wakawafuata lilipo chomoza jua. 

61. Na yalipo onana majeshi mawili haya, watuwa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! 

62. (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa! 

63. Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa. 

64. Na tukawajongeza hapo wale wengine. 

65. Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote. 

66. Kisha tukawazamisha hao wengine. 

67. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini. 

68. Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

69. Na wasomee khabari za Ibrahim. 

70. Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini? 

71. Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea. 

72. Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? 

73. Au yanakufaeni, au yanakudhuruni? 

74. Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo. 

75. Je! Mmewaona hawa mnao waabudu- 

76. Nyinyi na baba zenu wa zamani? 

77. Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

78. Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa, 

79. Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. 

80. Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha. 

81. Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha. 

82. Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo. 

83. 83, Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema. 

84. Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye. 

85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema. 

86. Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu. 

87. Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa. 

88. Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana. 

89. Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi. 

90. Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu. 

91. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu. 

92. Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu 

93. Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe? 

94. Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu, 

95. Na majeshi ya Ibilisi yote. 

96. Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo: 

97. Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri, 

98. Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

99. Na hawakutupoteza ila wale wakosefu. 

100. Basi hatuna waombezi. 

101. Wala rafiki wa dhati. 

102. Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini. 

103. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. 

104. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

105. Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume. 

106. Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu? 

107. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 

108. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 

109. Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

110. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 

111. Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini? 

112. Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya? 

113. Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua! 

114. Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini. 

115. Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri. 

116. Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe. 

117. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha. 

118. Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini. 

119. Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni. 

120. Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia. 

121. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini. 

122. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

123. Kina A'd waliwakanusha Mitume. 

124. Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu? 

125. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 

126. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 

127. Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

128. Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi? 

129. Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! 

130. Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. 

131. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. 

132. Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua. 

133. Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. 

134. Na mabustani na chemchem. 

135. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa. 

136. Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha. 

137. Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani. 

138. Wala sisi hatutaadhibiwa. 

139. Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 

140. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

141. Kina Thamud waliwakanusha Mitume. 

142. Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu? 

143. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 

144. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. 

145. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

146. Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa? 

147. Katika mabustani, na chemchem? 

148. Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva. 

149. Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi. 

150. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 

151. 151, Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka, 

152. Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi. 

153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa. 

154. Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. 

155. Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu. 

156. Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa. 

157. Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta. 

158. Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 

159. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

160. Watu wa Lut'i waliwakanusha Mitume. 

161. Alipo waambia ndugu yao, Lut'i: Je! Hamumchimngu? 

162. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu. 

163. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi. 

164. Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

165. Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume? 

166. Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka! 

167. Wakasema: Ewe Lut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji! 

168. Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu. 

169. Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo. 

170. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote, 

171. Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma. 

172. Kisha tukawaangamiza wale wengine. 

173. Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa. 

174. Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 

175. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. 

176. Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume. 

177. Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu? 

178. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. 

179. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. 

180. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

181. Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja. 

182. Na pimeni kwa haki iliyo nyooka; 

183. Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi. 

184. Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia. 

185. Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa. 

186. Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo. 

187. Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. 

188. Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda. 

189. Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa. 

190. Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. 

191. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

192. Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

193. Ameuteremsha Roho muaminifu, 

194. Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji, 

195. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi. 

196. Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale. 

197. Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili? 

198. Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu, 

199. Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini. 

200. Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu. 

201. Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. 

202. Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari. 

203. Na watasema: Je, tutapewa muhula? 

204. Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu? 

205. Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka, 

206. Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa, 

207. Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa? 

208. Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji - 

209. Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu. 

210. Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo, 

211. Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi. 

212. Hakika hao wametengwa na kusikia. 

213. Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa. 

214. Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe. 

215. Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini. 

216. Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda. 

217. Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

218. Ambaye anakuona unapo simama, 

219. Na mageuko yako kati ya wanao sujudu. 

220. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. 

221. Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani? 

222. Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi. 

223. Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo. 

224. Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata. 

225. Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde? 

226. Na kwamba wao husema wasiyo yatenda? 

227. Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.