27 - AN-NAML
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu kinacho
bainisha;
2. Uwongofu na bishara kwa Waumini,
3. Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini
nayo.
4. Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao,
kwa hivyo wanatangatanga ovyo.
5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika Akhera ndio
watapata khasara zaidi.
6. Na hakika wewe unafundishwa Qur'ani inayo tokana kwake Mwenye
hikima Mwenye kujua.
7. (Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona moto,
nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili mpate
kuota moto.
8. Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu na
walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa
walimwengu wote.
9. Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye
hikima.
10. Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka
nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu
Mitume.
11. Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya ubaya,
basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
12. Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe bila ya
maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao
walikuwa watu waovu.
13. Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema:
Huu ni uchawi dhaahiri.
14. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao
zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!
15. Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu
Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye tufadhilisha kuliko wengi
katika waja wake Waumini.
16. Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa
usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo
dhaahiri.
17. Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na
ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu.
18. Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu
chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni
Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua.
19. Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema:
Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na
wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema yako katika
waja wako wema.
20. Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni
Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu?
21. Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au nitamchinja, au
aniletee hoja ya kutosha.
22. Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua usilo
gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za
yakini.
23. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila
kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.
24. Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi
Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo
hawakuongoka,
25. Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana
katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.
26. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi
tukufu..
27. Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni
mwa waongo.
28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame
watarejesha nini.
29. (Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa barua
tukufu.
30. Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi
wa rehema, Mwenye kurehemu.
31. Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye
kusalimu amri.
32. Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo langu
hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.
33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko
kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.
34. Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na
wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.
35. Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi
nayo wajumbe.
36. Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo
ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi
kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.
37. Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza
kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na
wanyonge.
38. Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea
kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.
39. Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka
pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu.
40. Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya
kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika
fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na
mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye
kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.
41. Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone ataongoka, au
atakuwa miongoni mwa wasio ongoka.
42. Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni
kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake wakasema):
Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu.
43. Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu
yalimzuilia. Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri.
44. Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo liona alidhani ni
maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman) akasema: Hakika
hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola wangu Mlezi!
Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja na Sulaiman kwa
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
45. Na kwa kina Thamud tulimtuma ndugu yao Saleh kuwaambia:
Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayo gombana.
46. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya
wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?
47. Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye
akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni watu
mnao jaribiwa.
48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala
hawafanyi la maslaha.
49. Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku
yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya
watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli.
50. Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu, na
wao hawatambui.
51. Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba
tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote.
52. Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu.
Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua.
53. Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa wanamchamngu.
54. Na Lut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya uchafu nanyi
mnaona?
55. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio badala ya
wanawake? Hakika nyinyi ni watu mnao fanya ujinga kabisa!
56. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Wafukuzeni
wafwasi wa Lut'i katika mji wenu. Hao ni watu wanao jitia usafi.
57. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe;
tukamkadiria katika walio baki nyuma.
58. Na tukawanyeshea mvua. Ni ovu kweli kweli hiyo mvua ya walio
kwisha onywa.
59. Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na
amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni bora, au wale
wanao washirikisha naye?
60. AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni
maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi
hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu?
Bali hao ni watu walio potoka.
61. Au nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na akajaalia
ndani yake mito, na akaweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili kiziwizi?
Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.
62. Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo mwomba, na
akaiondoa dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na
Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayo yazingatia.
63. Au nani yule anaye kuongoeni katika giza la bara na bahari, na
akazipeleka pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu pamoja na
Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya wanao washirikisha naye.
64. Au nani anaye uanzisha uumbaji, kisha akaurejesha? Na nani anaye
kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu? Sema: Leteni hoja zenu
65. Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipo kuwa
Mwenyezi Mungu. Wala wao hawajui lini watafufuliwa.
66. Kwani huo ujuzi wao umefikilia kuijua Akhera? Bali wao wamo
katika shaka nayo tu, bali wao ni vipofu nayo.
67. Na wakasema walio kufuru: Tutapo kuwa mchanga, sisi na baba
zetu, hivyo kweli tutakuja tolewa?
68. Haya haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya
ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale.
69. Sema: Nendeni katika ardhi, na tazameni ulikuwaje mwisho wa
wakosefu.
70. Wala usiwahuzunukie wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya hila
zao wanazo zifanya.
71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa mnasema kweli?
72. Sema: Asaa ni karibu kukufikieni sehemu ya yale mnayo
yahimiza.
73. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye fadhila kwa watu, lakini
wengi wao hawashukuru.
74. Na hakika Mola wako Mlezi anayajua yanayo ficha vifua vyao na
wanayo yatangaza.
75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu
kinacho bainisha.
76. Hakika Qur'ani hii inawasimulia Wana wa Israili mengi wanayo
khitalifiana nayo.
77. Nayo hakika ni Uwongofu na Rehema kwa Waumini.
78. Hakika Mola wako Mlezi atawahukumu kwa hukumu yake, naye ni
Mwenye nguvu Mjuzi.
79. Basi mtegemee Mweneyezi Mungu; hakika wewe uko juu ya Haki iliyo
wazi.
80. Kwa hakika wewe huwezi kuwafanya maiti wasikie, wala kuwafanya
viziwi wasikie wito, wanapo kwisha geuka kwenda zao.
81. Wala huwezi kuwaongoa vipofu waache upotovu wao. Huwezi
kuwafanya wasikie isipo kuwa wenye kuziamini Ishara zetu; na hao ndio
wat'iifu.
82. Na itapo waangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika
ardhi atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana na yakini na Ishara
zetu.
83. Na Siku tutapo kusanya kutoka kila umma kundi katika wanao
kadhibisha Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu.
84. Hata watakapo fika, atasema (Mwenyezi Mungu): Je! Nyinyi si
mlizikanusha Ishara zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya nini?
85. Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyo dhulumu. Basi hao
hawatasema lolote.
86. Je! Hawaoni kwamba sisi tumeufanya usiku ili watulie, na mchana
wa kuangaza. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
87. Na Siku litapo pulizwa baragumu, watahangaika waliomo mbinguni
na katika ardhi, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni
wanyonge.
88. Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama
mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo
kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo.
89. Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao
watasalimika na mahangaiko ya Siku hiyo.
90. Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso zao Motoni.
Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda?
91. Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu aliye
ufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe
miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea.
92. Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida
ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa
waonyaji.
93. Na sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.
Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako Mlezi si mwenye
kughafilika na myatendayo.