28 - AL-QAS'AS'
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. T'A SIN MIM, (T'.S.M.)
2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho
bainisha.
3. Tunakusomea khabari za Musa na Firauni
kwa Haki kwa ajili ya watu wanao amini.
4. Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na
akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni
mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha
watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.
5. Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi.
6. Na kuwapa nguvu katika nchi, na
kutokana na wao kuwaonyesha kina Firauni na Hamana na majeshi
7. Tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia: Mnyonyeshe. Na
utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi
tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume.
8. Basi wakamwokota watu wa Firauni, aje kuwa adui kwao na huzuni.
Hakika Firauni na Hamana na majeshi
9. Na mkewe Firauni alisema: Atakuwa kiburudisho cha macho kwangu
na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mwenetu. Wala wao
hawakutambua.
10. Na moyo wa mama yake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kumdhihirisha,
ingeli kuwa hatukumtia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini.
11. Naye akamwambia dada yake Musa: Mfuatie. Basi naye akawa
anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua.
12. Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu mwanzo, mpaka
dada yake akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea kwa ajili
yenu, nao pia watakuwa wema kwake?
13. Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala
asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi
wao hawajui.
14. Na Musa alipo fika utu-uzima baraabara, tulimpa akili na ilimu.
Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema.
15. Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji wake, na akakuta
humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na mwengine katika
maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake. Musa akampiga
ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet'ani; hakika yeye ni adui,
mpotezaji dhaahiri.
16. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu;
basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
17. Akasema: Mola wangu Mlezi! Kwa ulivyo nineemesha, basi mimi
sitakuwa kabisa msaidizi wa wakosefu.
18. Akapambazukiwa mjini asubuhi naye ana khofu, akiangalia huku na
huku. Mara yule yule aliye mtaka msaada jana akawa anampigia kelele amsaidie.
Musa akamwambia: Hakika wewe ni mgomvi kweli kweli.
19. Basi alipo taka kumshika kwa nguvu yule aliye adui wao wote
wawili, akasema: Ewe Musa! Unataka kuniuwa
20. Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akipiga mbio, akasema: Ewe
Musa! Wakubwa wanashauriana kukuuwa. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanao
kupa nasaha.
21. Basi akatoka, naye ana khofu, akiangalia huku na huku. Akasema:
Mola wangu Mlezi! Niokoe na watu madhaalimu.
22. Na alipo elekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu Mlezi
akaniongoa njia iliyo sawa.
23. Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu
wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu
24. Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema:
Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayo niteremshia.
25. Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona
haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo
mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwisha okoka kwenye watu
madhaalimu.
26. Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu.
Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.
27. Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa
wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako; lakini mimi
sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema.
28. Musa akasema: Hayo yamekwisha kuwa baina yangu na wewe. Muda
mmojapo nikiumaliza sitiwi ubayani. Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu ya haya
tunayo yasema.
29. Basi alipo timiza muda wake na akasafiri na ahali zake, aliona
moto upande wa Mlima T'uri. Akawaambia ahali zake: Ngojeni! Mimi nimeona moto,
labda nitakuleteeni kutoka huko khabari au kijinga cha moto ili mpate kuota
moto.
30. Basi alipo ufikia aliitwa kutoka ng'ambo ya bonde la kuliani
katika eneo lilio barikiwa kutoka kwenye mti: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi
Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
31. Na tupa chini fimbo yako. Basi alipo iona ikitikisika kama
nyoka, akarudi nyuma wala hakutazama. (Akaambiwa): Ewe Musa! Njoo mbele wala
usiogope. Hakika wewe ni miongoni mwa walio salimika.
32. Ingiza mkono wako kwenye mfuko wako, utatoka mweupe pasipo na
ubaya. Na jiambatishe mkono wako ukihisi khofu. Basi hizi ni dalili mbili
zitokazo kwa Mola wako Mlezi kumpelekea Firauni na wakuu wa umma wake. Hakika
hao walikuwa watu mafaasiki.
33. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nilimuuwa mtu katika wao,
kwa hivyo naogopa wataniuwa.
34. Na ndugu yangu Harun ni fasihi zaidi ulimi wake kuliko mimi.
Basi mtume ende nami kunisaidia, ili anisadikishe. Hakika mimi nina khofu
watanikadhibisha.
35. (Mwenyezi Mungu) akasema: Tutautia nguvu mkono wako kwa nduguyo,
na tutakupeni madaraka, hata wasikufikilieni. Kwa sababu ya Ishara zetu nyinyi
na watakao kufuateni mtashinda.
36. Basi alipo wafikia Musa na Ishara zetu, walisema: Haya si
chochote ila ni uchawi ulio zuliwa. Na hatukuyasikia haya kwa baba zetu wa
zamani.
37. Na Musa akasema: Mola wangu Mlezi ni Mwenye kujua kabisa nani
anaye kuja na uwongofu unao toka kwake, na nani atakaye kuwa na mwisho mwema wa
makaazi. Hakika wenye kudhulumu hawatafanikiwa.
38. Na Firauni akasema: Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye mungu
asiye kuwa mimi. Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo, unijengee mnara
nipate kumchungulia mungu wa Musa. Na hakika mimi namwona yeye ni katika
waongo.
39. Na alipanda kiburi yeye na majeshi yake katika nchi bila ya
haki, na wakadhania kuwa hawatarudishwa kwetu.
40. Basi tukamshika yeye na majeshi yake, na tukawatupa baharini.
Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kudhulumu?
41. Na tuliwafanya ni waongozi waitao kwenye Moto. Na Siku ya Kiyama
hawatanusuriwa.
42. Na tukawafuatishia laana katika dunia hii, na Siku ya Kiyama
watakuwa miongoni mwa wanao chusha.
43. Na hakika bila ya shaka tulimpa Musa Kitabu baada ya kwisha
ziangamiza kaumu za mwanzo, ili kiwafumbue macho watu, na kiwe uwongofu, na
rehema, ili wapate kukumbuka.
44. Wala wewe hukuwa upande wa magharibi tulipo mpa Musa amri, wala
hukuwa katika walio hudhuria.
45. Lakini Sisi tuliziumba kaumu, na ukawa mrefu umri juu yao. Wala
hukuwa mkaazi na watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu. Lakini ni Sisi tulio kuwa
tukiwatuma Mitume.
46. Wala hukuwa kando ya mlima tulipo nadi. Lakini ni rehema itokayo
kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio pata kufikiwa na mwonyaji kabla
yako, huenda wakakumbuka.
47. Na usije kuwasibu msiba kwa iliyo yatanguliza mikono yao, wakasema:
Ewe Mola wetu Mlezi! Mbona hukututumia Mtume nasi, tukafuata Ishara zako, na
tukawa miongoni mwa Waumini?
48. Ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema: Mbona hakupewa kama
aliyo pewa Musa? Je! Kwani wao hawakuyakataa aliyo pewa Musa zamani? Walisema:
Ni wachawi wawili wanasaidiana. Na wakasema: Hakika sisi tunawakataa wote.
49. Sema: Basi leteni Kitabu kinacho toka kwa Mwenyezi Mungu chenye
kuongoka zaidi kuliko hivi viwili tukifuate, kama nyinyi mnasema kweli.
50. Na ikiwa hawakuitikii, basi jua kuwa wanafuata pumbao lao tu. Na
nani aliye potea zaidi kumshinda anaye fuata pumbao lake bila ya uwongofu
utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye
kudhulumu.
51. Na sasa kwa yakini tumewafikishia Neno ili wapate
kukumbuka.
52. Wale tulio wapa Kitabu kabla yake wanakiamini hiki.
53. Na wanapo somewa wanasema: Tunaiamini. Hakika hii ni Haki inayo
toka kwa Mola wetu Mlezi. Hakika sisi kabla yake tulikuwa ni Waislamu, tulio
nyenyekea.
54. Basi hao watapewa ujira wao mara mbili kwa walivyo vumilia, na
wakaondoa ubaya kwa wema, na wakatoa katika tuliyo waruzuku.
55. Na wanapo sikia upuuzi hujitenga nao na husema: Sisi tuna
vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu. Salamun Alaikum, Amani juu yenu!
Sisi hatutaki kujibizana na wajinga.
56. Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu
humwongoa amtakaye. Na Yeye ndiye anawajua zaidi waongokao.
57. Na wakasema: Tukiufuata uwongofu huu pamoja nawe tutanyakuliwa
kutoka nchi yetu. Je! Kwani Sisi hatukuwaweka imara katika pahala patakatifu,
penye amani, ambapo huletewa matunda ya kila aina kuwa ni riziki itokayo kwetu?
Lakini wengi wao hawajui.
58. Na miji mingapi iliyo jifakharisha tumeiangamiza! Na hayo
maskani yao hayakukaliwa tena baada yao, ila kwa uchache tu. Na Sisi ndio
tumekuwa warithi wao.
59. Na Mola wako Mlezi haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika
miji yake mikuu awasomee Ishara zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake
wawe madhaalimu.
60. Na chochote mlicho pewa ni matumizi ya maisha ya dunia na pambo
lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayo baki zaidi. Basi je,
hamfahamu?
61. Je! Yule tuliye muahidi ahadi nzuri, tena naye akayapata, ni
kama tuliye mstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani, na kisha Siku ya
Kiyama akawa miongoni mwa wanao hudhurishwa?
62. Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi mlio kuwa mkidai
kuwa ni washirika wangu?
63. Watasema wale iliyo thibiti juu yao kauli: Mola wetu Mlezi! Hawa
ndio tulio wapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyo potea sisi. Tunajitenga nao
mbele yako. Hawakuwa wakituabudu sisi.
64. Na itasemwa: Waiteni hao miungu wa kishirikina wenu! Basi
watawaita, lakini hawatawaitikia, na wataiona adhabu; laiti wangeli kuwa
wameongoka!
65. Na siku atapo waita na akasema: Mliwajibu nini Mitume?
66. Basi zitawapotea khabari siku hiyo, nao hawataulizana.
67. Ama mwenye kutubu na akaamini na akatenda mema, huyo atakuwa
miongoni mwa wenye kufanikiwa.
68. Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe hawana
khiari. Mwenyezi Mungu ametukuka na ametakasika na hao wanao washirikisha
naye.
69. Na Mola wako Mlezi anayajua yaliyo ficha vifua vyao, na wanayo
yatangaza.
70. Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye. Sifa
zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake Yeye. Na kwake
Yeye mtarejeshwa.
71. 71 Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni
moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu
atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii?
72. Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni
moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye
kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?
73. Na ni katika rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate
kupumzika humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
74. Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi hao mlio kuwa mkidai
kuwa ni washirika wangu?
75. Na tutatoa shahidi katika kila umma, na tutasema: Leteni hoja
zenu! Hapo watajua kwamba hakika kweli ni ya Mwenyezi Mungu, na yatawapotea
yale waliyo kuwa wakiyazua.
76. Hakika Qaruni alikuwa katika watu wa Musa, lakini aliwafanyia
dhulma. Na tulimpa khazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu wenye nguvu
kuzichukua. Walipo mwambia watu wake: Usijigambe! Hakika Mwenyezi Mungu
hawapendi wanao jigamba.
77. Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera.
Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo
kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika
Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.
78. Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu niliyo
nayo. Je! Hakujua kwamba Mwenyezi Mungu kesha waangamiza, katika vizazi vya
walio kabla yake, watu walio kuwa wenye ngubvu zaidi kuliko yeye, na wenye
makundi makubwa zaidi kuliko yake. Na wakosefu hawataulizwa khabari ya dhambi
zao.
79. Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema wale walio
kuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungeli kuwa tunayo kama aliyo pewa
Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.
80. Na wakasema wale walio pewa ilimu: Ole wenu! Malipo ya Mwenyezi
Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Wala hawatapewa hayo isipo
kuwa wenye subira.
81. Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake katika ardhi; wala
halikuwepo kundi lolote la kumnusuru kwa Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni
mwa wanao jitetea.
82. Na wale walio tamani kuwa pahala pake jana, wakawa wanasema:
Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na
humdhikisha amtakaye. Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutufanyia hisani angeli
tudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi!
83. Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasio taka
kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu.
84. Atakaye tenda wema atapata malipo bora kuliko huo wema alio
utenda. Na atakaye tenda uovu, hawalipwi watendao uovu ila waliyo kuwa
wakiyatenda.
85. Hakika aliye kulazimisha kuifuata Qur'ani hapana shaka
atakurudisha pahala pa marejeo. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye mjua zaidi
mwenye kuja na uwongofu, na nani aliyomo katika upotofu ulio dhaahiri.
86. Nawe hukuwa unataraji kuletewa Kitabu; lakini ni rehema tu ya
Mola wako Mlezi. Basi usiwe msaidizi wa makafiri.
87. Wala wasikuzuie kuzifuata Aya za Mwenyezi Mungu baada ya
kuteremshiwa wewe. Na lingania kwa Mola wako Mlezi, wala usiwe miongoni mwa
washirikina.
88. Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwenginewe. Hapana
mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipo kuwa Yeye. Hukumu iko kwake, na
kwake mtarejezwa.