29 - AL - A'NKABUT

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) 

2. Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? 

3. Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo. 

4. Au wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya hiyo wanayo hukumu. 

5. Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. 

6. Na anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu. 

7. Na walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda. 

8. Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda. 

9. Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawatia miongoni mwa watu wema. 

10. Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu? 

11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio amini, na atawatambulisha wanaafiki. 

12. Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo. 

13. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua. 

14. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhaalimu. 

15. Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote. 

16. Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua. 

17. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa. 

18. Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha kadhibisha. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi. 

19. Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji, na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. 

20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu. 

21. Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa. 

22. Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. 

23. Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu chungu. 

24. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini. 

25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni. 

26. Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 

27. Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuriya zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema. 

28. Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo. 

29. Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli. 

30. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa! 

31. Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu. 

32. Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye miongoni mwa watao kaa nyuma. 

33. Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao, na moyo uliona dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa watao kaa nyuma. 

34. Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanao ufanya. 

35. Na tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao tumia akili zao. 

36. Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi mkifisidi. 

37. Lakini walimkanusha basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi, wakapambazukiwa ndani ya nyumba zao nao wamefudikia. 

38. Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona. 

39. Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia kwa Ishara waziwazi, lakini walijivuna katika nchi, wala hawakuweza kushinda. 

40. Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tulio wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio nyakuliwa na ukelele; na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tulio wazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao. 

41. Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua. 

42. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanacho kiomba badala yake Yeye. Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima. 

43. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila wenye ilimu. 

44. Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa hakika katika hayo ipo Ishara kwa Waumini. 

45. SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda. 

46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake. 

47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri. 

48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wavunjifu. 

49. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu. 

50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu. 

51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao amini. 

52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri. 

53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa ghafla, na hali wao hawana khabari. 

54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa hakika imewazunguka makafiri! 

55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda! 

56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu. 

57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu. 

58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao, 

59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. 

60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. 

61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa? 

62. Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. 

63. Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu. 

64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua! 

65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha. 

66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua! 

67. Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za Mwenyezi Mungu wanazikataa? 

68. Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri? 

69. Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.