30 - AR-RUM

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) 

2. Warumi wameshindwa, 

3. Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda 

4. Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi. 

5. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. 

6. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui. 

7. Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera. 

8. Je! Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi. 

9. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao. 

10. Kisha ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara. 

11. Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake. 

12. Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa. 

13. Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao. 

14. Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika. 

15. Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika Bustani. 

16. Na ama walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu. 

17. Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na asubuhi, 

18. Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na adhuhuri. 

19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa. 

20. Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote. 

21. Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. 

22. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi. 

23. Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao sikia. 

24. Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao zingatia. 

25. Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi. 

26. Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii Yeye. 

27. Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 

28. Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo ogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili. 

29. Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru. 

30. Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui. 

31. Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina. 

32. Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho. 

33. Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao wametubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao Mlezi, 

34. Kwa kuyakataa tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua! 

35. Au tumewateremshia hoja ambayo kwayo ndio wanafanya ushirikina? 

36. Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na ukiwasibu uovu kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa. 

37. Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini. 

38. Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa. 

39. Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa. 

40. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha akakuruzukuni, kisha anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote katika hao mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika, na ametukuka na hayo mnayo mshirikisha naye. 

41. Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu. 

42. Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa walio tangulia. Wengi wao walikuwa washirikina. 

43. Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana. 

44. Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao. 

45. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri. 

46. Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema, na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru. 

47. Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya ukosefu. Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini. 

48. Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika waja wake, mara hao huwa na furaha. 

49. Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa. 

50. Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyo ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya shaka Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. 

51. Na tunge utuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya hayo wange endelea kukufuru. 

52. Kwani wewe hakika huwafanyi maiti wakasikia, wala viziwi wakasikia wito wakisha geuka kukupa mgongo. 

53. Wala wewe huwaongoi vipofu na upotovu wao. Huwasikilizishi ila wanao ziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walio nyenyekea. 

54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza. 

55. Na siku itapo simama Saa wakosefu wataapa kwamba hawakukaa duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyo kuwa wakipotozwa. 

56. Na walio pewa ilimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamuijui. 

57. Basi Siku hiyo hautawafaa walio dhulumu udhuru wao, wala haitotakiwa toba yao. 

58. Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur'ani. Na ukiwaletea Ishara yoyote hapana shaka walio kufuru watasema: Nyinyi si chochote ila ni waongo. 

59. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga muhuri kwenye nyoyo za wasio jua. 

60. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala wasikupaparishe hao wasio kuwa na yakini.