36 - YA-SIN
KWA JINA
LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Ya-Sin (Y.S.).
2. Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima!
3. Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,
4. Juu ya Njia Iliyo Nyooka.
5. Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa ,
basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
7. Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.
8. Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo
vichwa vyao viko juu tu.
9. Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho
10. Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
11. Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha
Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira
mwema.
12. Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza,
na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye
kubainisha.
13. Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio
tumwa.
14. Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu
kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
15. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu
16. Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa
kwenu.
17. Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.
18. Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha
basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.
19. Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa?
Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.
20. Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema:
Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.
21. Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe
wameongoka.
22. NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake
mtarejeshwa?
23. Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa
Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala
hawataniokoa.
24. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio
dhaahiri.
25. Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!
26. Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli
jua
27. Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni
mwa walio hishimiwa.
28. Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka
mbinguni, wala si wenye kuteremsha.
29. Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!
30. Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.
31. Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla
32. Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.
33. Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na
tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!
34. Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na
tukatimbua chemchem ndani yake,
35. Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono
36. Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika
vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.
37. Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa
gizani.
38. Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye
nguvu, Mwenye kujua.
39. Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.
40. Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote
vinaogelea katika njia zao.
41. Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika
jahazi ilio sheheni.
42. Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.
43. Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala
hawaokolewi,
44. Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.
45. Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko
nyuma yenu, ili mpate kurehemewa...
46. Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila
wao huwa ni wenye kuipuuza.
47. Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu,
walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu
angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio
dhaahiri.
48. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni
wakweli?
49. Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo
kuzozana.
50. Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.
51. Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia
kwa Mola wao Mlezi.
52. Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya
ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
53. Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele
yetu.
54. Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila
yale mliyo kuwa mkiyatenda.
55. Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.
56. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya
fakhari.
57. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho
kitaka.
58. "Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi
Mwenye kurehemu.
59. Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!
60. Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani?
Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.
61. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
62. Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni
mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?
63. Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.
64. Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.
65. Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe
ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
66. Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa
wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?
67. Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi
wasinge weza kwenda wala kurudi.
68. Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je!
hawazingatii?
69. Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani
kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha.
70. Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.
71. Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono
yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
72. Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda,
na baadhi yao wanawala.
73. Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je,
hawashukuru?
74. Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati
wapate kusaidiwa!
75. Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao
hudhurishwa.
76. Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo
yaweka siri na wanayo yatangaza.
77. Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana
na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!
78. Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani
huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?
79. Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na
Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.
80. Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi
mkawa kwa huo mnawasha.
81. Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao?
Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.
82. Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na
kikawa.
83. Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila
kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.