44 - ADDUKHAN
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'a Mim
2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,
3. Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni
Waonyaji.
4. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,
5. Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye
kusikia Mwenye kujua.
7. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi
mna yakini.
8. Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na
Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.
9. Lakini wao wanacheza katika shaka.
10. Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio
dhaahiri,
11. Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!
12. Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
13. Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye
kubainisha.
14. Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni
mwendawazimu.
15. Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini
mtarejea vile vile!
16. Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi
ni wenye kutesa.
17. Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na
aliwafikia Mtume Mtukufu.
18. Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni
Mtume Muaminifu.
19. Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni
uthibitisho ulio wazi.
20. Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi
pia, ili msinipige mawe.
21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
22. Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni
wakosefu.
23. Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa
yakini mtafuatwa.
24. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi
litakalo zamishwa.
25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!
26. Na mimea na vyeo vitukufu!
27. Na neema walizo kuwa wakijistareheshea!
28. Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe.
29. La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula.
30. Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya
kuwadhalilisha,
31. Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia
mipaka.
32. Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe.
33. Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
34. Hakika hawa wanasema:
35. Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi
hatufufuliwi.
36. Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
37. Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla
38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa
mchezo.
39. Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.
40. Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.
41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala
hawatanusuriwa.
42. Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye
Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
43. Hakika Mti wa Zaqqum,
44. Ni chakula cha mwenye dhambi.
45. Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni
46. Kama kutokota kwa maji ya moto.
47. (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu!
48. Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo
chemka.
49. Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!
50. Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.
51. Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani,
52. Katika mabustani na chemchem,
53. Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana,
54. Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini.
55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.
56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi
Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu,
57. Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu
kukubwa.
58. Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate
kukumbuka.
59. Ngoja tu, na wao wangoje pia.