46 - AL - AH'QAAF
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. H'A MIM
2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
3. Hatukuziumba mbingu na ardhi wala
yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda maalumu. Na walio kufuru
wanayapuuza yale wanayo onywa.
4. Je! Mwawaona wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au hao wanayo shirika
katika mbingu? Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki, au alama
yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
5. Na nani mpotofu mkubwa kuliko hao wanao waomba, badala ya
Mwenyezi Mungu, ambao hawatawaitikia mpaka Siku ya Kiyama, na
wala hawatambui maombi
6. Na ambao watu watakapo kusanywa watakuwa maadui zao, na
wataikataa ibada
7. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, walio kufuru husema juu
ya haki inapo wajia: Huu ni uchawi dhaahiri.
8. Au wanasema: Ameizua mwenyewe! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi
nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye anajua zaidi hayo
mnayo ropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Na Yeye ndiye
Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
9. Sema: Mimi si kiroja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyo
fanywa wala nyinyi. Mimi nafuata niliyo funuliwa tu kwa Wahyi, wala mimi si
chochote ila ni mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.
10. Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu,
nanyi mmeyakataa, na akashuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya
mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu wenye kudhulumu.
11. Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Lau kuwa hii ni kheri,
wasingeli tutangulia. Na walipo kosa kuongoka wakasema: Huu ni uzushi wa
zamani.
12. Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa chenye uwongozi
na rehema. Na hichi ni Kitabu cha kusadikisha na kilicho kuja kwa lugha ya
Kiarabu, ili kiwaonye walio dhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
13. Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu; kisha
wakatengenea, hawatakuwa na khofu, wala hawatahuzunika.
14. Hao ndio watu wa Peponi, watadumu humo, kuwa ni malipo kwa
waliyo kuwa wakiyatenda.
15. Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama
yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba
kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima
wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe
nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema
unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na
mimi ni miongoni mwa Waislamu.
16. Hao ndio tunao wapokelea bora ya vitendo vyao walivyo vitenda,
na tunayasamehe makosa
17. Na ambaye amewafyonya wazazi wake na akawaambia: Ati ndio
mnanitisha kuwa nitafufuliwa, na hali vizazi vingi vimekwisha pita kabla yangu!
Na hao wazazi humwomba msaada Mwenyezi Mungu (na humwambia mtoto wao): Ole
wako! Amini! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na yeye husema: Hayakuwa
haya ila ni visa vya watu wa kale.
18. Hao ndio ambao imehakikikishwa hukumu juu
19. Na wote watakuwa na daraja zao mbali mbali kwa waliyo yatenda,
na ili awalipe kwa vitendo vyao, na wala hawatadhulumiwa.
20. Na siku watakapo letwa walio kufuru kwenye Moto wataambiwa:
Nyinyi mlitwaa vitu vyenu vizuri katika uhai wa duniani, na mkastareheshwa
navyo. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya fedheha kwa mlivyo kuwa mkitakabari katika
ardhi bila ya haki, na kwa sababu mlikuwa mkifanya upotovu.
21. Na mtaje ndugu wa kina A'di, alipo waonya watu wake kwenye
vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada
yake kuwaambia: Msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nakukhofieni
isikupateni adhabu ya siku iliyo kuu.
22. Wakasema: Je! Umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi
tuletee hayo unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
23. Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu. Mimi
nakufikishieni niliyo tumwa. Lakini nakuoneni kuwa nyinyi mnafanya ujinga.
*
24. Basi walipo liona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema:
Wingu hili la kutunyeshea mvua! Kumbe sivyo, haya ni hayo mliyo yahimiza, upepo
ambao ndani yake imo adhabu chungu!
25. Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake Mlezi. Wakawa
hawaonekani ila nyumba zao tu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wakosefu!
26. Na bila ya shaka tuliwaweka vizuri sio kama tulivyo kuwekeni
nyinyi; na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo. Na hayakuwafaa kitu masikio
yao, wala macho yao, wala nyoyo zao kwa lolote. Kwani hao walikuwa wakizikataa
Ishara za Mwenyezi Mungu, na yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara ndiyo
yakawazunguka.
27. Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tulizitumia
Ishara ili wapate kurejea.
28. Basi mbona wale walio washika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa ati
hao ndio wawakurubishe, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na huo ndio uwongo
walio kuwa wakiuzua.
29. Na wakati tulipo waleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza
Qur'ani. Basi walipo ihudhuria walisema: Sikilizeni! Na ilipo kwisha somwa,
walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.
30. Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho
teremshwa baada ya Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho
ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka.
31. Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na
muaminini, Mwenyezi Mungu atakusameheni, na atakukingeni na adhabu chungu.
32. Na wasio mwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hao
hawatashinda katika ardhi, wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo
katika upotovu ulio dhaahiri.
33. Je! Hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliye ziumba mbingu na
ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwani?
Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
34. Na siku watakapo letwa makafiri Motoni wakaambiwa: Je! Haya si
kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, ni kweli! Atasema: Basi
onjeni adhabu kwa sababu ya kule kukataa kwenu.
35. Basi subiri, kama walivyo subiri Mitume wenye stahmala kubwa,
wala usiwafanyie haraka. Siku watakayo yaona waliyo ahidiwa itakuwa kama kwamba
hawakukaa ulimwenguni ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani
huangamizwa wengine isipo kuwa walio waovu tu ?