5 - AL - MAIDA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Enyi mlio amini! Timizeni ahadi. Mmehalalishiwa wanyama wa mifugo, ila wale mnao tajiwa. Lakini msihalalishe kuwinda nanyi mmo katika Hija. Hakika Mwenyezi Mungu anahukumu apendavyo. 

2. Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa Makka kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. 

3. Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliye chinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongeka koo, na aliye kufa kwa kupigwa, na aliye kufa kwa kuanguka, na aliye kufa kwa kupigwa pembe, aliye liwa na mnyama, ila mkimdiriki kumchinja. Na pia ni haramu kula nyama aliye chinjiwa masanamu. Na ni haramu kupiga ramli. Hayo yote ni upotovu. Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Na mwenye kushurutishwa na njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu. 

4. Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na mlicho wafundisha wanyama kukiwinda. Mnawafundisha alivyo kufunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni walicho kukamatieni, na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. 

5. Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anaye kataa kuamini bila shaka a'mali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara. 

6. Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru. 

7. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, na ahadi yake aliyo fungamana nanyi mlipo sema: Tumesikia na tumet'ii. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyomo vifuani. 

8. Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. 

9. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio muamini na wakatenda mema kwamba watapata maghfira na malipo makubwa. 

10. Na wale walio kufuru na wakakanusha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni. 

11. Enyi mlio amini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, walipo taka watu kukunyooshieni mikono, naye akaizuilia mikono yao kukufikieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. 

12. Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa Israili. Na tukawateulia kutokana nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa yakini Mimi ni pamoja nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, hapana shaka nitakufutieni maovu yenu na nitakuingizeni katika mabustani yapitayo mito kati yake. Lakini atakaye kufuru miongoni mwenu baada ya hayo bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa. 

13. Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana nao, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.  

14. Na kutoka kwa wale walio sema: Sisi ni Manasara, tulichukua ahadi yao, lakini wakasahau sehemu ya waliyo kumbushwa. Kwa hivyo tukaweka kati yao uadui na chuki mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia waliyo kuwa wakiyafanya. 

15. Enyi Watu wa Kitabu! Amekwisha kujieni Mtume wetu anaye kufichulieni mengi mliyo kuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anaye samehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha. 

16. Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyo nyooka. 

17. Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu. Sema: Ni nani mwenye kumiliki cho chote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi? Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu. 

18. Na Mayahudi na Wakristo wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema: Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu tu kama wale wengine alio waumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye. 

19. Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni Mtume wetu akikubainishieni katika wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema: Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji. Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa kila kitu. 

20. Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu. 

21. Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika. 

22. Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari. Nasi hatutaingia huko mpaka wao watoke humo. Wakitoka humo hapo tutaingia. 

23. Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, walisema: Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini. 

24. Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo kamwe maadamu wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane. Sisi tutakaa hapa hapa. 

25. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu. 

26. (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe usiwasikitikie watu wapotovu. 

27. Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli. Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu. 

28. Ukininyooshea mkono wako kuniuwa, mimi sitakunyooshea mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote. 

29. Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako, kwani wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Na hayo ndiyo malipo ya wenye kudhulumu. 

30. Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika. 

31. Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anaye fukua katika ardhi ili amwonyeshe vipi kumsitiri nduguye. Akasema: Ole wangu! Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta. 

32. Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi. 

33. Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa. 

34. Isipo kuwa wale walio tubu kabla hamjawatia nguvuni. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. 

35. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na tafuteni njia ya kumfikilia. Na wanieni kwa juhudi kwa ajili yake ili mpate kuokoka. 

36. Hakika walio kufuru lau wange kuwa na yote yaliyomo duniani, na mengine kama hayo, ili watoe fidia ya kuepukana na adhabu ya Siku ya Kiyama, yasingeli pokelewa kwao; na watapata adhabu chungu. 

37. Watataka watoke Motoni, lakini hawatatoka humo, na watakuwa na adhabu inayo dumu. 

38. Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 

39. Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake, na akatengenea, basi Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. 

40. Hujui ya kwamba Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na ardhi? Humuadhibu amtakaye, na humsamehe amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. 

41. Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wa fanyao haraka kukufuru, miongoni mwa wanao sema kwa vinywa vyao: Tumeamini, na hali nyoyo zao hazikuamini, na miongoni mwa Mayahudi, wanao sikiliza kwa ajili ya uwongo, wanao sikiliza kwa ajili ya watu wengine wasio kufikia. Wao huyabadilisha maneno kutoka pahala pake. Wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo pewa haya tahadharini. Na mtu ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi kuwa na madaraka naye mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao. Watakuwa na hizaya duniani, na Akhera watakuwa na adhabu kubwa. 

42. Hao ni wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo, na ni walaji mno vya haramu! Basi wakikujia, wahukumu baina yao au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao, basi wao hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu. 

43. Na huwaje wakufanye wewe hakimu nao wanayo Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanageuka. Na hao si wenye kuamini. 

44. Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uwongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walio nyenyekea kiislamu, na wachamngu, na wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali niogopeni Mimi. Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache. Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri. 

45. Na humo tuliwaandikia ya kwamba roho kwa roho, na jicho kwa jicho, na pua kwa pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino, na kwa majaraha kisasi. Lakini atakaye samehe basi itakuwa ni kafara kwake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhaalimu. 

46. Na tukawafuatishia hao Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongofu, na nuru na inayo sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa wachamngu. 

47. Na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyo teremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu. 

48. Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni nyote umma mmoja, lakini ni kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyo kuwa mkikhitalifiana. 

49. Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije kukufitini ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi wa watu ni wapotofu. 

50. Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini? 

51. Enyi mlio amini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa ni marafiki. Wao ni marafiki wao kwa wao. Na miongoni mwenu mwenye kufanya urafiki nao, basi huyo ni katika wao. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu. 

52. Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema: Tunakhofu yasitusibu mabadiliko. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake wakawa wenye kujuta kwa waliyo yaficha katika nafsi zao. 

53. Na walio amini watasema: Hivyo hawa ndio wale walio apa ukomo wa viapo vyao kuwa wao wa pamoja nanyi? Vitendo vyao vitapotea bure, na wataamkia kuwa wenye kukhasirika. 

54. Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na Mwenye kujua. 

55. Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea. 

56. Na atakaye fanya urafiki na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kushinda. 

57. Enyi mlio amini! Msiwafanye marafiki wale walio ifanyia kejeli na mchezo Dini yenu miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, na makafiri wengine. Na mcheni Mwenyezi Mungu kama nyinyi ni wenye kuamini. 

58. Na mnapo adhinia Sala wao wanaichukulia maskhara na mchezo. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili. 

59. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hivyo mnatuchukia kwa kuwa tumemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo teremshiwa na yaliyo teremshwa kabla, na kwa kuwa wengi katika nyinyi ni wapotofu? 

60. Sema: Je! Nikwambieni yule ambaye ni mwenye malipo mabaya zaidi kuliko hayo mbele ya Mwenyezi Mungu? Ni yule ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani na amemkasirikia, na amewafanya miongoni mwao manyani na nguruwe, na wakamuabudu Shet'ani. Hao ndio wenye mahali pabaya na wamepotea zaidi njia iliyo sawa. 

61. Na wanapo kujieni husema: Tumeamini. Lakini hakika wao wameingia na ukafiri wao, na wametoka nao pia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kabisa wa yote wanayo yaficha. 

62. Na utawaona wengi katika wao wanakimbilia kwenye dhambi, na uadui, na ulaji wao vya haramu. Ni maovu mno hayo wayatendayo! 

63. Mbona hao wanazuoni na makohani wao hawawakatazi maneno yao ya dhambi, na ulaji wao vya haramu? Ni maovu mno hayo wayafanyayo! 

64. Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyo fumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyo yasema. Bali mikono yake iwazi. Hutoa apendavyo. Kwa yakini yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidisha wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama. Kila mara wanapo washa moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu. 

65. Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeli amini na wakachamngu hapana shaka tungeli wafutia makosa yao, na tungeli waingiza katika Bustani zenye neema. 

66. Na lau kuwa wangeli ishika Taurati na Injili na yote waliyo teremshiwa kutokana na Mola wao Mlezi, basi hapana shaka wangeli kula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. Wapo watu miongoni mwao walio sawa, lakini wengi wao wanayo yafanya ni mabaya mno. 

67. Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri. 

68. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hamna lenu jambo mpaka muishike Taurati na Injili na yote mlio teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi. Na hakika ulio teremshiwa wewe kutokana na Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na ukafiri. Basi usiwasikitikie watu makafiri. 

69. Hakika walio amini, na Mayahudi na Masabii na Wakristo, walio muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya mwisho, na wakatenda mema, basi hawatakuwa na khofu wala hawatahuzunika. 

70. Tulifanya agano na Wana wa Israili, na tukawatumia Mitume. Kila alipo wajia Mtume kwa wasio yapenda nafsi zao wengine waliwakanusha na wengine wakawauwa. 

71. Na wakadhani kuwa hapatakuwa majaribio; basi wakawa vipofu na viziwi. Kisha Mwenyezi Mungu akawapokelea toba zao. Kisha tena wengi katika wao wakawa vipofu na viziwi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona hayo wayatendayo. 

72. Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru. 

73. Kwa hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa Utatu. Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayo yasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale wanao kufuru. 

74. Je! Hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. 

75. Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyo wabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyo geuzwa. 

76. Sema: Je! Mnawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, wale ambao hawawezi kukudhuruni wala kukufaeni? Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua. 

77. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya watu walio kwisha potea tangu zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa. 

78. Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka. 

79. Walikuwa hawakatazani maovu waliyo kuwa wakiyafanya. Hakika ni maovu yalioje mambo waliyo kuwa wakiyafanya! 

80. Utawaona wengi wao wanafanya urafiki na walio kufuru. Hakika ni maovu yaliyo tangulizwa na nafsi zao hata Mwenyezi Mungu amewakasirikia, nao watadumu katika adhabu. 

81. Na lau wangeli kuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu, na huyu Nabii, na yaliyo teremshwa kwake, wasingeli wafanya hao marafiki. Lakini wengi katika wao ni wapotofu. 

82. Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa walio amini ni Mayahudi na washirikina. Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanao sema: Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi. 

83. NA WANAPO SIKIA yaliyo teremshwa kwa Mtume utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia. 

84. Na kwa nini tusimuamini Mwenyezi Mungu na Haki iliyo tujia, na hali tunatumai Mola wetu Mlezi atuingize pamoja na watu wema? 

85. Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyo yasema, Bustani zipitazo mito katika yake; humo watadumu. Na haya ndiyo malipo ya wafanyao wema. 

86. Na wale walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni. 

87. Enyi mlio amini! Msiharimishe vizuri alivyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msikiuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wakiukao mipaka. 

88. Na kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini. 

89. Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru. 

90. Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. 

91. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha? 

92. Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, na tahadharini. Na ikiwa mtageuka basi jueni ya kuwa juu ya Mtume wetu ni kufikisha ujumbe tu ulio wazi. 

93. Si dhambi juu ya walio amini na wakatenda mema kwa walivyo vila (zamani) maadamu wakichamngu na wakiamini na wakitenda mema, kisha wakachamngu, na wakaamini, kisha wakachamngu na wakafanya mazuri. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao mazuri. 

94. Enyi mlio amini! Mwenyezi Mungu atakujaribuni kidogo kwa wanyama wa kuwinda inayo wafikia mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi Mungu amjue nani anaye mkhofu kwa ghaibu. Basi atakaye ruka mipaka baada ya hayo atapata adhabu kali. 

95. Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake hili. Mwenyezi Mungu amekwisha yafuta yaliyo pita; lakini atakaye fanya tena Mwenyezi Mungu atampa adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu. 

96. Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini na kuvila, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa mawindo ya wanyama wa bara maadamu mmeharimia Hija. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mtakusanywa kwake. 

97. Mwenyezi Mungu ameifanya Al Kaaba, hii Nyumba Tukufu, ni simamio la watu, na kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa dhabihu, na vigwe. Hayo ili mjue ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. 

98. Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, na Mwenye kurehemu. 

99. Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnacho kidhihirisha na mnacho kificha. 

100. Sema: Haviwi sawa viovu na vyema ujapo kupendeza wingi wa viovu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, ili mpate kufanikiwa. 

101. Enyi mlio amini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatakuchukizeni. Na mkiyauliza inapo teremshwa Qur'ani mtabainishiwa. Mwenyezi Mungu amesamehe hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira Mpole. 

102. Waliyauliza hayo watu wa kabla yenu, kisha wakawa wenye kuyakataa. 

103. Mwenyezi Mungu hakujaalia uharamu wowote juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala "Wasila" wala "Hami". Lakini walio kufuru humzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na wengi wao hawatumii akili. 

104. Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, na kwa Mtume, husema: Yanatutosha tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawakuongoka? 

105. Enyi mlio amini! Kilicho lazima juu yenu ni nafsi zenu. Hawakudhuruni walio potoka ikiwa nyinyi mmeongoka. Ni kwa Mwenyezi Mungu ndio marudio yenu nyote; basi atakwambieni yale mliyo kuwa mkiyatenda. 

106. Enyi mlio amini! Yanapo mfikia mauti mmoja wenu na akataka kutoa wasia, basi wawepo mashahidi wawili miongoni mwenu ambao ni waadilifu. Na mnapo kuwa safarini, na msiba wa mauti ukakusibuni, basi washuhudie wengineo wawili wasio kuwa katika nyinyi. Mtawazuia wawili hao baada ya Sala na waape kwa Mwenyezi Mungu, mkitilia shaka, wakisema: Hatutopokea thamani yoyote kwa haya hata kwa ajili ya jamaa; na wala hatutaficha ushahidi wa Mwenyezi Mungu; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi. 

107. Ikigundulikana kuwa wawili hao wamestahiki dhambi, basi wawili wengineo kutokana na warithi wenye kudai haki washike makamo ya wa mwanzo. Nao waape kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hakika ushahidi wetu ni wa haki zaidi kuliko ushahidi wa wale. Na sisi hatujafanya dhambi; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa walio dhulumu. 

108. Hivi inaelekea zaidi ya kwamba watatoa ushahidi ulio sawa au wataogopa visije vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao. Na mcheni Mwenyezi Mungu na msikie. Na hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi wapotofu. 

109. Ile siku ambayo Mwenyezi Mungu atapo wakusanya Mitume awaambie: Mlijibiwa nini? Watasema: Hatuna ujuzi; hakika Wewe ndiye Mjuzi Mkubwa wa yote yaliyo fichikana. 

110. Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu! 

111. Na nilipo wafunulia Wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu. 

112. Wanafunzi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini. 

113. Wakasema: Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanao shuhudia. 

114. Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku. 

115. Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu. 

116. Na pale Mwenyezi Mungu atakapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu? (Na Isa) atasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyo fichikana. 

117. Sikuwaambia lolote ila uliyo niamrisha, nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipo kuwa nao. Na ulipo nifisha ukawa Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu. 

118. Ukiwaadhibu basi hao ni waja wako. Na ukiwasamehe basi Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 

119. Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa. 

120. Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Naye ni Muweza wa kila kitu.