60 - AL - MUMTAH'INAH
KWA JINA
LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Enyi mlio amini! Msiwafanye adui zangu na adui
zenu kuwa marafiki mkiwapa mapenzi, na hali wao wamekwisha ikataa haki iliyo
kujieni, wakamfukuza Mtume na nyinyi kwa sababu mnamuamini Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wenu. Mnapotoka kwa ajili ya Jihadi katika Njia
yangu na kutafuta radhi yangu, mnafanya urafiki nao kwa siri, na Mimi
nayajua mnayo yaficha na mnayo dhihirisha. Na mwenye kufanya
hayo kati yenu basi ameipotea njia ya sawa.
2. Wakikuwezeni wanakuwa maadui zenu, na
wanakukunjulieni mikono
3. Hawatakufaeni jamaa zenu, wala watoto wenu Siku ya Kiyama.
Mwenyezi Mungu atapambanua baina yenu, na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo
yatenda.
4. Hakika nyinyi mna mfano mzuri kwenu kwa Ibrahim na wale walio
kuwa pamoja naye, walipo waambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na
hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunakukataeni; na umekwisha
dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapo muamini Mwenyezi
Mungu peke yake. Isipo kuwa kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika
nitakuombea msamaha, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi
Mungu. Mola wetu Mlezi! Juu yako tumetegemea, na kwako tumeelekea, na kwako
ndio marejeo.
5. Mola wetu Mlezi! Usitufanyie mtihani kwa walio kufuru. Na
tusamehe, Mola wetu Mlezi. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
6. Kwa yakini umekuwa mfano mzuri kwenu katika mwendo wao, kwa
anaye mtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kugeuka basi hakika
Mwnyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
7. Asaa Mwenyezi Mungu akatia mapenzi baina yenu na hao maadui
zenu, na Mwenyezi Mungu ni Mweza, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye
kurehemu.
8. Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale
ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu
huwapenda wafanyao uadilifu.
9. Hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni kufanya urafiki na wale
walio kupigeni vita, na wakakutoeni makwenu, na wakasaidia katika kufukuzwa
kwenu. Na wanao wafanya hao marafiki basi hao ndio madhaalimu.
10. Enyi mlio amini! Wakikujilieni wanawake Waumini walio hama, basi
wafanyieni mtihani - Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua zaidi Imani yao. Mkiwa
mnawajua kuwa ni Waumini basi msiwarudishe kwa makafiri. Wanawake hao si halali
kwa hao makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake Waumini. Na wapeni
hao wanaume mahari walio toa. Wala hapana makosa kwenu kuwaoa mkiwapa mahari
yao. Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu. Na takeni
mlicho kitoa, na wao watake walicho kitoa. Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu
anayo kuhukumuni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
11. Na akitoroka yeyote katika wake zenu kwenda kwa makafiri, tena
ikatokea mkapata ngawira, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha
mahari waliyo yatoa. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
12. Ewe Nabii! Watakapo kujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba
hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini,
wala hawatawauwa watoto wao, wala hawataleta uzushi wanao uzua tu wenyewe baina
ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana nao
ahadi, na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi
maghfira, Mwenye kurehemu.
13. Enyi mlio amini! Msiwafanye rafiki zenu watu ambao Mwenyezi
Mungu amewakasirikia. Hao wamekwisha kata tamaa ya Akhera, kama makafiri
walivyo wakatia tamaa watu wa makaburini.