61 - ASS'AF
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye
nguvu, Mwenye hikima.
2. Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo
yatenda?
3. Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi
Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda.
4. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika Njia
yake kwa safu
5. Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini
mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye
tumwa kwenu? Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke. Na
Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
6. Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi
ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu
katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina
lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi
ulio dhaahiri!
7. Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye mzulia
Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi
watu madhaalimu.
8. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi
Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia.
9. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki
ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
10. Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayo kuokoeni na
adhabu iliyo chungu?
11. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni Jihadi
katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu,
ikiwa nyinyi mnajua.
12. Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika Mabustani
yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele.
Huko ndio kufuzu kukubwa.
13. Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Mwenyezi
Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!
14. Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyo
sema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa
Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi
taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi
tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.