62 - AL - JUMUA'
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi
Mungu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
2. Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma,
awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla
ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
3. Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye ndiye Mwenye
nguvu, Mwenye hikima.
4. Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayo mpa amtakaye. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
5. Mfano wa walio bebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa
punda anaye beba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu walio
kadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu.
6. Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa ni vipenzi
vya Mwenyezi Mungu pasipo kuwa watu wengine, basi yatamanini mauti, ikiwa
mnasema kweli.
7. Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyo kwisha
yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua walio dhulumu.
8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia, bila ya shaka yatakukuteni.
Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Hapo
atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi
kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau
kama mnajua.
10. Na itakapo kwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila
za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate
kufanikiwa.
11. Na wanapo iona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo na
wakakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao
na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki.