67 - AL - MULK
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni
Mwenye uweza juu ya kila kitu.
2. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni
mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye
msamaha.
3. Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika
uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote?
4. Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea
mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka.
5. Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na
tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa
nguvu.
6. Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na
ni marejeo maovu yalioje hayo!
7. Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku
inafoka.
8. Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo
walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji?
9. Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na
tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika
upotovu mkubwa!
10. Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili,
tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!
11. Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni!
12. Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata
maghfira na ujira mkubwa.
13. Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa
yaliyomo vifuani.
14. Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari?
15. Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni
katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio
kufufuliwa.
16. Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye
ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika!
17. Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni
kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu?
18. Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi
kulikuwaje kukasirika kwangu?
19. Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa
zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye
kuona kila kitu.
20. Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa
Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu.
21. Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki
yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki.
22. Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi,
au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka?
23. Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni
masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu.
24. Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake
mtakusanywa.
25. Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?
26. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi
ni mwonyaji tu mwenye kubainisha.
27. Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru
zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba.
28. Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja
nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu?
29. Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake
tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri.
30. Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani
atakueleteeni maji yanayo miminika?