7 - AL - A'RAAF
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. ALIF LAM MYM 'SAAD
2. Kitabu kilicho teremshwa kwako - basi isiwe dhiki kifuani kwako kwa
ajili yake, upate kuonya kwacho, na kiwe ni ukumbusho kwa Waumini.
3. Fuateni mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala
msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake. Ni machache mnayo
yakumbuka.
4. Na miji mingapi tuliiangamiza, ikaifikia adhabu yetu usiku au
walipo kuwa wamelala adhuhuri.
5. Basi hakikuwa kilio chao ilipo wafikia adhabu yetu, isipo kuwa kusema:
Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu.
6. Na kwa yakini tutawauliza wale walio pelekewa Ujumbe, na pia
tutawauliza hao Wajumbe.
7. Tena tutawasimulia kwa ilimu; wala Sisi hatukuwa mbali.
8. Na Siku hiyo kipimo kitakuwa kwa Haki. Basi watakao kuwa na
uzani mzito, hao ndio watakao fanikiwa.
9. Na watakao kuwa na uzani khafifu, basi hao ndio walio zitia
khasarani nafsi zao kwa sababu ya kuzipinga Ishara zetu.
10. Na hakika tumekuwekeni katika ardhi, na tumekujaalieni humo njia
za kupatia maisha. Ni kuchache kushukuru kwenu.
11. Na hakika tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha
tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam. Basi wakasujudu isipo kuwa Iblisi, hakuwa
miongoni mwa walio sujudu.
12. Mwenyezi Mungu akasema: Nini kilicho kuzuia kumsujudia nilipo
kuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye
umemuumba kwa udongo.
13. Akasema: Basi teremka kutoka humo! Haikufalii kufanya kiburi
humo. Basi toka! Hakika wewe u miongoni mwa walio duni.
14. Akasema: Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa.
15. Akasema: Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula.
16. Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika
Njia yako Iliyo Nyooka.
17. Kisha nitawazukia mbele
18. Akasema: Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha fukuzwa.
Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi
nyote.
19. Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni
humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu.
20. Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo
fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa
Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele.
21. Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao
kunasihini.
22. Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao
zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita:
Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa
dhaahiri?
23. Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama
hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.
24. Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui. Na kwenye
ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.
25. Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo
mtatolewa.
26. Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na
nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi
Mungu mpate kukumbuka.
27. Eny wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama alivyo watoa
wazazi wenu Peponi, akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na
kabila yake wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya
Mashet'ani kuwa ni marafiki wa wasio amini.
28. Na wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu,
na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi
mambo machafu. Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua?
29. Sema: Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu, na mumuelekeze nyuso
zenu kila mnapo sujudu, na muombeni Yeye kwa kumsafia Dini. Kama alivyo
kuumbeni mwanzo ndivyo mtavyo rudi,
30. Hali ya kuwa kundi moja amelihidi, na kundi jengine
limethibitikiwa na upotofu. Kwa hakika hao waliwafanya mashet'ani kuwa ndio
marafiki walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, na wanadhani kuwa wao
wameongoka.
31. Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa
ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye
hapendi wanao fanya israfu.
32. Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo
watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio
amini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna
hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua.
33. Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na
ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na
asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua.
34. Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi
hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia.
35. Enyi wanaadamu! Watakapo kufikieni Mitume miongoni mwenu
wakakuelezeni Ishara zangu, basi watakao mchamngu na wakatengenea haitakuwa
khofu kwao, wala hawatahuzunika.
36. Na wale watakao kanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao
ni watu wa Motoni; humo watadumu.
37. Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu
uwongo, au anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia sehemu yao waliyo
andikiwa, mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi
mlio kuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na
watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri.
38. Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo
pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake.
Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola
wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu.
Atasema: Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
39. Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi nyinyi pia
hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyo kuwa
mkiyachuma.
40. Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi
hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia
katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu.
41. Jahannamu itakuwa kitanda chao na juu yao nguo za moto za
kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
42. Na wale wanao amini na wakatenda mema - hatumkalifishi mtu
yoyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa Peponi. Wao watadumu humo.
43. Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe inapita mito.
Na watasema: Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye
tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi
Mungu hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Na watanadiwa
kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa
mkiyafanya.
44. Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta
aliyo tuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo
kuahidini Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji
atawatangazia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu,
45. Wale ambao walikuwa wakizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na
wakataka kuipotosha, nao wanaikanusha Akhera.
46. Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na juu ya
Mnyanyuko patakuwa watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao watawaita watu
wa Peponi: Assalamu Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado hawajaingia humo, lakini
wanatumai.
47. Na yanapo geuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni, watasema:
Mola Mlezi wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu walio dhulumu.
48. Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa alama
zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho mlicho kuwa
mnafanyia kiburi.
49. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi Mungu
hatawafikishia rehema. Ingieni Peponi, hapana khofu kwenu, wala
hamtahuzunika!
50. Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumimieni maji, au chochote
alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika Mwenyezi Mungu
ameviharimisha hivyo kwa makafiri,
51. Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo, na maisha ya
dunia yakawadanganya. Basi leo Sisi tunawasahau kama walivyo usahau mkutano wa
Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu.
52. Na hakika tumewaletea Kitabu tulicho kipambanua kwa ilimu,
uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini.
53. Je, lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake? Siku yatapo
fika matokeo yake watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu
walileta Haki! Je, tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye
yasiyo kuwa yale tuliyo kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri nafsi
zao, na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua.
54. Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na
ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku
kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa
amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wa viumbe vyote.
55. Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika
Yeye hawapendi warukao mipaka.
56. Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha
tengenezwa. Na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi
Mungu iko karibu na wanao fanya mema.
57. Na Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara
kabla ya kufika rehema yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito
tunayachunga mpaka kwenye nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio
kama hivyo tukatolesha kila aina ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo
wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.
58. Na ardhi njema, yenye udongo wa rutba, hutoa mimea yenye kukua
vizuri yenye uhai, kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Na ardhi mbaya haitoi ila
mimea michache, isiyo na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo tunavyo
zipambanua Ishara (Aya) kwa watu wanao shukuru.
59. Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi kaumu yangu!
Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi
ninakukhofieni adhabu ya Siku iliyo kuu.
60. Wale watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika sisi tunakuona
wewe umo katika upotofu ulio dhaahiri.
61. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu, lakini mimi
ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
62. Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninakunasihini; na
ninayajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
63. Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi
wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na ili
mumchemngu, na ili mpate kurehemewa?
64. Basi walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja
naye katika jahazi. Na tukawazamisha wale walio kanusha Ishara zetu. Hakika hao
walikuwa watu vipofu.
65. Na kwa A'adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema: Enyi watu
wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je,
hamumchi?
66. Wakasema watukufu wa wale walio kufuru katika kaumu yake: Sisi tunakuona
umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe ni katika
waongo.
67. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni
Mtume niliye toka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
68. Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni
mwenye kukunasihini, muaminifu.
69. Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu
Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo
kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi
zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
70. Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake,
na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi,
ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
71. Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha
kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina
tu mliyo yaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha
uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja.
72. Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye kwa rehema zetu,
na tukakata mizizi ya wale walio zikanusha Ishara zetu, na hawakuwa wenye
kuamini.
73. Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu
wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha
kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike
wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya
Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu.
74. Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na
akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake,
na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala
msitende uovu katika nchi kwa ufisadi.
75. Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa
wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola
Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa.
76. Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo
yaamini.
77. Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na
wakasema: Ewe Saleh! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa
Mitume.
78. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa
majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa.
79. Basi Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu!
Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi
hamwapendi wenye nasaha.
80. Na tulimtuma Lut', alipo waambia watu wake: Je, mnafanya uchafu
ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote!
81. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkwawacha
wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji!
82. Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipo kuwa kuambizana:
Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanao jitakasa.
83. Basi tukamwokoa yeye na watu wake, isipo kuwa mkewe, alikuwa
miongoni mwa walio bakia nyuma.
84. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyo kuwa mwisho wa
wakosefu.
85. Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib. Akasema:
Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa
Yeye. Imekwisha kufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni
sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye
uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu
ikiwa nyinyi ni Waumini.
86. Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na kuwazuilia na
Njia ya Mwenyezi Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia ipotoke. Na
kumbukeni mlipo kuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na tazameni jinsi
ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi.
87. Na kama liko kundi miongoni mwenu lililo amini haya niliyo
tumwa, na kundi jengine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu
baina yetu. Naye ndiye Mbora wa wenye kuhukumu.
88. WAHESHIMIWA WALIO TAKABARI katika kaumu yake wakasema: Ewe
Shua'ib! Tutakutoa wewe pamoja na wale walio kuamini katika mji wetu, au mrejee
katika mila yetu. Akasema: Je, ingawa tunaichukia?
89. Bila ya shaka itakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukirudi
katika mila yenu baada ya kwisha tuokoa nayo Mwenyezi Mungu. Wala haiwi kwetu
sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu. Ujuzi wa
Mola Mlezi wetu umeenea katika kila kitu. Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Ewe
Mola Mlezi wetu! Tuhukumie baina yetu na kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye mbora
wa wanao hukumu.
90. Na waheshimiwa walio kufuru katika kaumu yake wakasema:
Mkimfuata Shua'ib, basi hakika hapo nyinyi mtakuwa mlio khasiri.
91. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na wakaamkia majumbani mwao
wamejifudikiza, wamekwisha kufa.
92. Wale walio mkanusha Shua'ib wakawa kama kwamba hawakuwako. Walio
mkanusha Shua'ib ndio walio kuwa wenye kukhasiri.
93. Basi akawaachilia mbali na akasema: Enyi kaumu yangu!
Nimekufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na nimekunasihini; basi vipi
niwahuzunikie watu makafiri?
94. Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji ila tuliwapatiliza wakaazi
wake kwa taabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.
95. Kisha Sisi hubadilisha mahala pa ubaya kwa wema, hata wakazidi,
na wakasema: Taabu na raha ziliwafikia baba zetu. Basi kwa ghafla tukawashika,
hali ya kuwa hawajatambua.
96. Na lau kuwa watu wa miji wangeli amini na wakamchamngu, kwa
yakini tungeli wafungulia baraka kutoka mbinguni na katika ardhi. Lakini
walikanusha basi tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyo kuwa
wakiyachuma.
97. Je, watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafika
usiku, nao wamelala?
98. Au watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafika
mchana, nao wanacheza?
99. Je, wamejiaminisha na mipango ya Mwenyezi Mungu? Kwani
hawajiaminishi na mipango ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye kukhasiri.
100. Je, hawahidiki hawa wanao rithi ardhi baada ya wale wenyewe
kwamba tukitaka tutawapatiliza kwa madhambi yao, na tutapiga muhuri juu ya
nyoyo zao, na kwa hivyo hawatasikia?
101. Miji hiyo, tunakusimulia baadhi ya khabari zake. Na hapana shaka
Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo waziwazi. Lakini hawakuwa wenye kuamini
waliyo yakanusha zamani. Namna hivi Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za
makafiri.
102. Wala hatukuwaona wengi wao kuwa wanatimiza ahadi; bali kwa
hakika tuliwakuta wengi wao ni wapotofu.
103. Kisha baada yao tukamtuma Musa na Ishara zetu kwa Firauni na
waheshimiwa wake. Nao wakazikataa. Basi tazama ulikuwaje mwisho wa
waharibifu.
104. Na Musa alisema: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa
Mola Mlezi wa viumbe vyote.
105. Inafaa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila lilio la Haki. Nami
hakika nimekujieni na dalili waziwazi kutokana na Mola Mlezi wenu. Basi waache
Wana wa Israili wende nami.
106. Akasema Firauni: Ikiwa umekuja na Ishara, basi ilete ukiwa ni
katika wasemao kweli.
107. Basi akaitupa fimbo yake, na mara ikawa nyoka dhaahiri.
108. Na akatoa mkono wake, mara ukawa mweupe kwa watazamao.
109. Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Hakika huyo ni mchawi
mjuzi.
110. Anataka kukutoeni katika nchi yenu. Basi mnatoa shauri
gani?
111. Wakasema: Mwache kidogo yeye na nduguye, na watume mijini
wakusanyao,
112. Wakuletee kila mchawi mjuzi.
113. Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: Hakika tutapata ujira
ikiwa tutashinda.
114. Akasema: Naam! Nanyi bila ya shaka mtakuwa katika wa karibu
nami.
115. Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe, au tutakuwa sisi tutao
tupa?
116. Akasema: Tupeni! Basi walipo tupa waliyazuga macho ya watu na
wakawatia khofu, na wakaleta uchawi mkubwa.
117. Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako. Mara
ikavimeza vyote vile walivyo vibuni.
118. Kweli ikathibiti na yakabat'ilika waliyo kuwa wakiyatenda.
119. Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo.
120. Na wachawi wakapoomoka wakisujudu.
121. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa viumbe vyote,
122. Mola Mlezi wa Musa na Haarun.
123. Akasema Firauni: Mmemuamini kabla sijakupeni idhini? Hizi ni
njama mlizo panga mjini mpate kuwatoa wenyewe. Lakini karibu mtajua!
124. Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali. Kisha
nitakutundikeni misalabani.
125. Wakasema: Sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
126. Nawe hukuudhika nasi ila kwa kuwa tumeziamini Ishara za Mola
Mlezi wetu zilipo tujia. Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie uvumilivu na utufishe
hali ni Waislamu.
127. Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Unamuacha Musa na watu
wake walete uharibifu katika nchi na wakuache wewe na miungu yako? Akasema:
Tutawauwa wavulana wao, na tutawaacha hai wanawake wao. Na bila ya shaka sisi
ni wenye nguvu juu yao.
128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu, na
subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Naye humrithisha amtakaye katika
waja wake. Na mwisho ni wa wachamngu.
129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia, na baada ya wewe
kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamhiliki adui wenu, na
akakufanyeni nyinyi ndio wa kufuatia kushika nchi, ili atazame mtavyo kuja
tenda nyinyi.
130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa miyaka (ya ukame) na
kwa upungufu wa mazao, ili wapate kukumbuka.
131. Likiwafika jema wakisema: Haya ni haki yetu. Na likiwafika ovu
husema: Musa na walio pamoja naye ni wakorofi. Hakika ukorofi wao huo unao
wafikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
132. Na wakisema: Hata ukituletea Ishara yoyote kutuzuga hatuto
kuamini.
133. Basi tukawapelekea tufani, na nzige, na chawa, na vyura, na
damu, kuwa ni Ishara mbali mbali. Nao wakapanda kiburi, na wakawa watu
wakosefu.
134. Na ilipo waangukia adhabu wakasema: Ewe Musa! Tuombee kwa Mola
wako Mlezi kwa aliyo kuahidi. Ukituondolea adhabu hii hapana shaka tutakuamini,
na tutawaachilia Wana wa Israili wende nawe.
135. Lakini tukiwaondolea adhabu mpaka muda fulani wao waufikie, mara
wakivunja ahadi yao.
136. Basi tuliwapatiliza, tuka- wazamisha baharini kwa sababu
walizikanusha Ishara zetu, na wakaghafilika nazo.
137. Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki na
magharibi ya ardhi tuliyo ibariki. Na likatimia neno jema la Mola Mlezi wako
juu ya Wana wa Israili, kwa vile walivyo subiri. Na tukayaangamiza aliyo kuwa
akiyafanya Firauni na kaumu yake, na waliyo kuwa wakiyajenga.
138. Na tukawavusha bahari Wana wa Israili, wakafika kwa watu wanao
abudu masanamu yao. Wakasema: Ewe Musa! Hebu tufanyie na sisi miungu kama hawa
walivyo kuwa na miungu. Musa akasema: Hakika nyinyi ni watu msio jua kitu.
139. Hakika haya waliyo nayo watu hawa yatakuja angamia, na hayo
waliyo kuwa wakiyafanya yamepotea bure.
140. Akasema: Je, nikutafutieni mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na
Yeye ndiye aliye kufadhilisheni juu ya viumbe vyote?
141. Na pale tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu
za mwisho wa uovu. Wakiwauwa wavulana wenu, na wakawaacha hai wanawake wenu. Na
katika hayo yalikuwa majaribio makubwa kutokana na Mola wenu Mlezi.
142. Tulimuahidi Musa masiku thalathini na tukayatimiza kwa kumi;
ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arubaini. Na Musa akamwambia nduguye
Haarun: Shika mahala pangu kwa watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya
waharibifu.
143. Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi
akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu
akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi
utaniona. Basi alipo jionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike,
na Musa akaanguka chini amezimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka,
Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.
144. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteuwa wende kwa
watu na Ujumbe wangu na maneno yangu. Basi chukua niliyo kupa na uwe katika
wanao shukuru.
145. Na tukamuandikia katika mbao kila kitu, mawaidha na maelezo ya
mambo yote. (Tukamwambia): Basi yashike kwa nguvu na uwaamrishe watu wako
wayashike kwa ubora wake. Nami nitakuonyesheni makaazi ya wapotofu.
146. Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi katika nchi
bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu
hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa
ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na wameghafilika
nazo.
147. Na walio zikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera a'mali zao
zimeharibika. Kwani watalipwa ila kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda?
148. Na baada yake walimfanya ndama kutokana na mapambo yao
(kumuabudu), kiwiliwili tu kilicho kuwa na sauti. Hivyo, hawakuona kuwa
hawasemezi wala hawaongoi njia? Wakamuabudu, na wakawa wenye kudhulumu.
149. Na walipo juta na wakaona ya kwamba wamekwisha potea, walisema:
Ikiwa Mola wetu Mlezi hakuturehemu na akatusamehe, bila ya shaka tutakuwa
miongoni mwa walio khasiri.
150. Na alipo rudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika na kuhuzunika,
alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya
Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na akamkamata kichwa ndugu yake
akimvutia kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu
wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu,
wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu.
151. (Musa) akasema: Mola Mlezi wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu,
na ututie katika rehema yako. Nawe ni Mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.
152. Hakika wale walio muabudu ndama, itawapata ghadhabu ya Mola wao
Mlezi na madhila katika maisha ya dunia. Na hivi ndivyo tunavyo walipa
wazushi.
153. Na walio tenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaamini,
hapana shaka kuwa Mola Mlezi wako baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu.
154. Na Musa ilipo mtulia ghadhabu aliziokota zile mbao. Na katika
maandiko yake mna uwongofu na rehema kwa wanao mwogopa Mola wao Mlezi.
155. Na Musa akawateuwa watu sabiini katika kaumu yake kwa miadi
yetu. Na ulipo fika mtetemeko mkubwa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ungeli taka
ungeli wahiliki wao na mimi zamani! Unatuhiliki kwa waliyo yafanya wajinga
katika sisi? Haya si chochote ila ni mtihani wako, umpoteze umtakaye na umhidi
umtakaye. Wewe ndiye Rafiki Mlinzi wetu. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe
ndiye mbora wa kughufiria.
156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika Akhera. Sisi
tumerejea kwako. (Mwenyezi Mungu) akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo
nimtakaye. Na rehema yangu imeenea kila kitu. Lakini nitawaandikia khasa wanao
mchamngu, na wanao toa Zaka, na wale ambao wanaziamini Ishara zetu,
157. Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala
kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha
mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu,
na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. Basi wale walio
muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo
teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.
158. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliye
tumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye
anaye huisha na anaye fisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake
asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake.
Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka.
159. Na katika kaumu ya Musa lipo kundi linao waongoa watu kwa haki
na kwa haki wanafanya uadilifu.
160. Na tuliwagawanya katika makabila kumi na mbili, mataifa mbali
mbali. Na tulimfunulia Musa walipo muomba maji watu wake kumwambia: Lipige hilo
jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatibuka humo chemchem kumi na mbili, na kila watu
wakajua mahali pao pa kunywea. Na tukawafunika kivuli kwa mawingu, na
tukawateremshia Manna na Salwa. Tukawaambia: Kuleni vizuri hivi tulivyo
kuruzukuni. Wala hawakutu- dhulumu Sisi, bali wamejidhulumu wenyewe.
161. Na pale walipo ambiwa: Kaeni katika mji huu, na mle humo
mpendapo, na semeni: Tufutie dhambi zetu. Na ingieni katika mlango wake kwa
unyenyekevu, tupate kukusameheni makosa yenu. Walio wema tutawazidishia.
162. Lakini walio dhulumu miongoni mwao walibadilisha kauli, sio ile
waliyo ambiwa. Basi tukawapelekea adhabu kutoka mbinguni kwa vile walivyo kuwa
wakidhulumu.
163. Na waulize khabari za mji ulio kuwa kando ya bahari, wakiivunja
Sabato (Jumaamosi ya mapumziko). Samaki walikuwa wakiwajia juu juu siku ya
mapumziko yao, na siku zisio kuwa za kupumzika hawakuwa wakiwajia. Kwa namna
hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya upotovu.
164. Na kikundi kati yao walisema: Kwa nini mnawawaidhi watu ambao
tangu hapo Mwenyezi Mungu atawateketeza au atawaadhibu adhabu kali? Wakasema:
Ili uwe ni udhuru kwa Mola Mlezi wenu, na huenda nao wakamchamngu.
165. Basi walipo yasahau waliyo kumbushwa, tuliwaokoa walio kuwa
wakikataza maovu, na tukawatesa walio dhulumu kwa adhabu mbaya kwa vile walivyo
kuwa wakifanya upotovu.
166. Walipo jifakharisha katika waliyo kanywa tuliwaambia: Kuweni
manyani wa kudharauliwa.
167. Na pale alipo tangaza Mola wako Mlezi kwamba hapana shaka
atawaletea watu ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya mpaka Siku ya Kiyama.
Hakika Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuadhibu, na bila ya shaka ni Mwenye
maghfira, na Mwenye kurehemu.
168. Na tuliwafarikisha katika ardhi makundi makundi. Wako kati yao
walio wema, na wengine kinyume cha hivyo. Na tukawajaribu kwa mema na mabaya
ili wapate kurejea.
169. Na wakafuatia baada yao kizazi kibaya walio rithi Kitabu.
Wakashika anasa za haya maisha duni, na wakasema: Tutasamehewa! Na ikiwajia
tena anasa kama hiyo wataishika pia. Je, hawakufanyiwa agano la Kitabu kuwa
wasiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila Haki tu? Nao wamekwisha soma yaliomo humo.
Na nyumba ya Akhera ni bora kwa wanao jikinga na maasi. Basi je, hamtii
akilini?
170. Na wale wanao kishikilia Kitabu, na wakashika Sala - hakika Sisi
hatupotezi ujira wa watendao mema.
171. Na pale tulipo unyanyua mlima juu yao ukawa kama kwamba ni
kiwingu kilicho wafunika, na wakadhani kuwa utawaangukia, (tukawaambia):
Kamateni kwa nguvu tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate
kumcha Mungu.
172. Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika wanaadamu kutoka
migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia:
Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku
ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.
173. Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu,
na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyo
yafanya wapotovu?
174. Ndio kama hivyo tunavyo zipambanua Ishara, kwa kutaraji kuwa
watarejea.
175. Na wasomee khabari za yule ambaye tulimpa Ishara zetu, naye
akajivua nazo. Na Shet'ani akamuandama, akawa miongoni walio potea.
176. Na tungelitaka tungeli mtukuza kwa hizo Ishara, lakini yeye
aliushikilia ulimwengu na akafuata pumbao lake. Basi mfano wake ni mfano wa
mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi na ukimwacha pia hupumua na kutoa
ulimi. Huo ni mfano wa kaumu wanao zikanusha Ishara zetu. Basi simulia hadithi,
huenda wakatafakari.
177. Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanao kanusha Ishara zetu na
wakajidhulumu nafsi zao.
178. Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemhidi basi huyo amehidika; na alio
waacha kupotea basi hao ndio walio khasirika.
179. Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini
hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini
hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio
walio ghafilika.
180. Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa
hayo. Na waacheni wale wanao haribu utakatifu wa majina yake. Hao watakuja
lipwa waliyo kuwa wakiyatenda.
181. Na katika tulio waumba wako watu wanao ongoza kwa Haki, na kwayo
wanafanya uadilifu.
182. Na wale walio kadhibisha Ishara zetu, tutawapururia pole pole
kwa namna ambayo wenyewe hawaijui.
183. Nami nitawapa muda. Hakika mpango wangu ni madhubuti.
184. Je, hawafikiri? Huyu mwenzao hana wazimu. Hakuwa yeye ila ni
mwonyaji aliye dhaahiri.
185. Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi, na vitu alivyo viumba
Mwenyezi Mungu, na pengine ajali yao imekwisha karibia? Basi maneno gani baada
ya haya watayaamini?
186. Aliye mwacha Mwenyezi Mungu kupotea hana wa kumwongoa. Atawaacha
hao wakitangatanga katika upotofu wao.
187. Wanakuuliza hiyo Saa (ya mwisho) itakuwa lini? Sema: Kuijua
kwake kuko kwa Mola Mlezi wangu. Haidhihirishi hiyo kwa wakati wake ila Yeye. Ni
nzito katika mbingu na ardhi. Haikujiini ila kwa ghafla tu. Wanakuuliza kama
kwamba wewe una pupa ya kuijua. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Lakini
aghlabu ya watu hawajui.
188. Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo
Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ninge jizidishia mema mengi,
wala ovu lisinge nigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mbashiri kwa watu
wanao amini.
189. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo
akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu. Na anapo muingilia hubeba
mzigo mwepesi, akitembea nao. Anapo kuwa mja mzito, wote wawili humwomba
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wao: Kama ukitupa mwana mwema tutakuwa katika wanao
shukuru.
190. Basi anapo wapa mwana mwema, wanamfanyia washirikina Mwenyezi
Mungu katika kile kile alicho wapa. Mwenyezi Mungu ametukuka na huko
kushirikisha kwao.
191. Ati wanawafanya viumbe kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, nao
hawaumbi, bali wao ndio wanaumbwa?
192. Wala hawana uwezo wa kuwanusuru wala wenyewe hawajinusuru.
193. Na mkiwaita kwenye uwongofu, hawakufuateni. Ni mamoja kwenu
ikiwa mtawaita au mkinyamaza.
194. Hakika hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu ni waja mfano
wenu nyinyi. Hebu waombeni, nao wakuitikieni, kama mnasema kweli.
195. Je, wao wanayo miguu ya kwendea? Au wanayo mikono ya kutetea? Au
wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikizia? Sema: Iiteni hio miungu
yenu ya ushirikina. Kisha nifanyieni mimi vitimbi, wala msinipe muhula.
196. Hakika Mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu aliye teremsha Kitabu.
Naye ndiye awalindae walio wema.
197. Na hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi hawawezi kukunusuruni,
wala hawajinusuru wenyewe.
198. Na mkiwaita kwenye uwongofu hawasikii. Na unawaona wanakutazama,
nao hawaoni.
199. Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na
majaahili.
200. Na uchochezi wa Shet'ani ukikuchochea basi omba ulinzi wa
Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Msikizi, Mjuzi.
201. Hakika wale wamchao Mungu, zinapo wagusa pepesi za Shet'ani,
mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki.
202. Na ndugu zao wanawavutia kwenye upotofu, kisha wao
hawaachi.
203. Na usipo waletea Ishara waitakayo husema: Kwa nini hukuibuni?
Sema: mimi ninafuata yanayo funuliwa kwangu kutokana na Mola Mlezi wangu. Hii
(Qur'ani) ni hoja zinazo toka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu na rehema kwa
watu wanao amini.
204. Na isomwapo Qur'ani isikilizeni na mnyamaze ili mpate
kurehemewa.
205. Na mkumbuke Mola Mlezi wako nafsini kwako kwa unyenyekevu na
khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni. Wala usiwe
miongoni wa walio ghafilika.
206. Hakika wale walioko kwa Mola wako Mlezi hawajivuni wakaacha
kumuabdu, na wanamtakasa na wanamsujudia