73 - AL - MUZZAMMIL
KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
1. Ewe uliye jifunika!
2. Kesha usiku kucha, ila kidogo tu!
3. Nusu yake, au ipunguze kidogo.
4. Au izidishe - na soma Qur'ani kwa utaratibu na utungo.
5. Hakika Sisi tutakuteremshia kauli nzito.
6. Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo, na maneno yake
yanatua zaidi.
7. Kwani hakika mchana una shughuli nyingi.
8. Na lidhukuru jina la Mola wako Mlezi, na ujitolee kwake kwa
ukamilifu.
9. Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, hapana mungu isipo kuwa Yeye,
basi mfanye kuwa Mtegemewa wako.
10. Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kwa vizuri.
11. Na niache Mimi na hao wanao kanusha, walio neemeka; na wape
muhula kidogo!
12. Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unao waka kwa ukali
kabisa!
13. Na chakula kinacho kwama kooni, na adhabu inayo umiza.
14. Siku ambayo ardhi itatikiswa na milima pia, na milima itakuwa
15. Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu,
16. Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamshika mshiko wa
mateso.
17. Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku ambayo
itawafanya watoto wadogo waote mvi?
18. Hapo mbingu zitapasuka! Ahadi yake itakuwa imetekelezwa.
19. Kwa hakika hili ni kumbusho. Mwenye kutaka atashika njia ya
kwendea kwa Mola wake Mlezi.
20. Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe unakesha
karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya
watu walio pamoja nawe kadhaalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye ukadiria usiku
na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni. Basi someni
kilicho chepesi katika Qur'ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa,
na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na
wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho
chepesi humo, na mshike Sala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo
mwema. Na kheri yoyote mnayo itanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi
Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa