9 - AT-TAWBA
1. Huku ni kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume
wake kwenye jukumu la maagano na mlio ahidiana nao katika washirikina.
2. Basi tembeeni katika nchi miezi mine, na jueni kwamba nyinyi
hamwezi kumshinda Mwenyezi Mung, na kwamba Mwenyezi
Mungu ndiye anaye wahizi makafiri.
3. Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi
Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume
wake hawana jukumu lolote kwa washirikina. Basi mkitubu itakuwa kheri kwenu, na mkigeuka basi jueni kuwa nyinyi hamumshindi Mwenyezi
Mungu. Na wabashirie makafiri kuwa watapata adhabu chungu.
4. Isipo kuwa washirikina ambao mliahidiana nao kisha
wasikupunguzieni chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi hao
watimizieni ahadi
5. Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote
mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia. Lakini
wakitubu, wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi waachilieni. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
6. Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi
mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake
pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.
7. Itakuwaje iwepo ahadi na washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na
mbele ya Mtume wake, ila wale mlio ahidiana nao kwenye Msikiti Mtakatifu? Basi
maadamu wanakwenda nanyi sawa, nanyi pia nendeni sawa nao. Hakika Mwenyezi
Mungu huwapenda wachamngu
8. Itakuwaje! Nao wakikushindeni hawatazami kwenu udugu wala ahadi.
Wanakufurahisheni kwa midomo yao tu, na nyoyo zao zinakataa hayo. Na wengi wao
ni wapotovu.
9. Wamenunua thamani ndogo kwa Ishara za Mwenyezi Mungu, na
wakazuilia watu na Njia yake. Hakika hao ni maovu waliyo kuwa wakiyatenda.
10. Hawatazami kwa Muumini udugu wala ahadi; basi hao ndio warukao
mipaka.
11. Basi wakitubu na wakashika Sala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu
zenu katika Dini. Na tunazichambua Aya kwa watu wajuao.
12. Na wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao, na wakatukana
Dini yenu, basi piganeni na waongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo vya
kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha.
13. Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo vyao na wakawa na hamu
ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara ya kwanza? Je, mnawaogopa?
Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope, ikiwa nyinyi ni Waumini.
14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na
awahizi na akunusuruni muwashinde, na avipoze vifua vya kaumu ya Waumini,
15. Na aondoe hasira ya nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba
ya amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
16. Je, mlidhani kuwa mtaachwa tu, bila ya Mwenyezi Mungu
kuwajuulisha wale walio pigana Jihadi kati yenu, na wala hawakumfanya mwendani
wao isipo kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wenziwe? Na Mwenyezi
Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
17. Haiwi kuwa makafiri ndio waamirishe misikiti ya Mwenyezi Mungu,
hali wanajishuhudishia wenyewe ukafiri. Hao ndio ambao vitendo vyao
vimeharibika, na katika Moto watadumu.
18. Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao
muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka,
na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika
waongofu.
19. Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na kuamirisha Msikiti
Mtakatifu ni sawa na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na
akapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
20. Wale walio amini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia
ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele
ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu.
21. Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo kwake, na radhi, na
Bustani ambazo humo watapata neema za kudumu.
22. Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo
makubwa.
23. Enyi mlio amini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa vipenzi
vyenu ikiwa wanastahabu ukafiri kuliko Imani. Na katika nyinyi atakaye wafanya
hao ndio vipenzi vyake, basi hao ndio madhaalimu.
24. Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu,
na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba
mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na
Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na
Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
25. Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika mapigano mengi, na
siku ya Hunayni ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni
kitu. Na ardhi ikawa dhiki kwenu juu ya upana wake. Kisha mkageuka mkarudi
nyuma.
26. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na
juu ya Waumini. Na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu wale
walio kufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
27. Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu atawasamehe awatakao. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
28. Enyi mlio amini! Hakika washirikina ni najsi, kwa hivyo
wasiukaribie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka wao huu. Na ikiwa mnakhofia
umasikini, basi Mwenyezi Mungu atakutajirisheni kwa fadhila yake akipenda.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
29. Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho,
wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala hawashiki
Dini ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa khiari yao,
hali wamet'ii.
30. Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu. Na Wakristo
wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao.
Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize!
Wanageuzwa namna gani hawa!
31. Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala
ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipo kuwa
wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo
wanayo mshirikisha nayo.
32. Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na
Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru yake ijapo kuwa makafiri
watachukia.
33. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki
ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
34. Enyi mlio amini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki
wanakula mali za watu kwa baat'ili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Na
wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.
35. Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo
vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya
ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.
36. Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili
katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo
iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu
humo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wnavyo pigana nanyi nyote. Na
jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
37. Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi katika kukufuru; kwa
hayo hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka
mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi
Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa
ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
38. Enyi mlio amini! Mna nini mnapo ambiwa: Nendeni katika Njia ya
Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia
kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na ya Akhera
ni chache.
39. Kama hamwendi atakuadhibuni adhabu chungu, na atawaleta watu
wengine, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila
kitu.
40. Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha
mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa
katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu
yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono
kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno
la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye
hikima.
41. Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na piganeni Jihadi kwa
mali yenu na nafsi zenu katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Haya ni kheri kwenu
mkiwa mnajua.
42. Na lau ingeli kuwa ipo faida ya papo kwa papo, na safari yenyewe
ni fupi, wangeli kufuata. Lakini wameona ni mbali na kuna mashaka. Nao wataapa
kwa Mwenyezi Mungu: Tungeli weza bila ya shaka tungeli toka pamoja nanyi.
Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni
waongo.
43. Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa ruhusa kabla ya
kubainikia kwako wanao sema kweli, na ukawajua waongo?
44. Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuwajua wachamngu.
45. Wasio muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na nyoyo zao
zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa. Basi hao wanataradadi katika
shaka zao.
46. Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangeli
jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo
akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!
47. Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na
wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao
wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
48. Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na wakakupindulia mambo
juu chini, mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya Mwenyezi Mungu, na wao
wamechukia.
49. Na miongoni mwao wapo wanao sema: Niruhusu wala usinitie katika
fitina. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika
Jahannamu imewazunguka.
50. Ukikupata wema unawachukiza, na ukikusibu msiba, wao husema:
Sisi tuliangalia mambo yetu vizuri tangu kwanza. Na hugeuka kwenda zao nao
wamefurahi.
51. Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye
Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu!
52. Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipo kuwa moja katika
mema mawili? Na sisi tunakutazamieni kuwa Mwenyezi Mungu akufikishieni adhabu
itokayo kwake, au kutokana na mikono yetu. Basi ngojeni, nasi tunangoja pamoja
nanyi.
53. Sema: Toeni mkipenda msipende. Hakitopokelewa kitu kwenu, kwani
nyinyi ni watu wapotovu.
54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa kuwa walimkataa
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala ila kwa uvivu, wala
hawatoi michango ila nao wamechukia.
55. Yasikufurahishe mali yao wala wana wao. Hakika Mwenyezi Mungu
anataka kuwaadhibu kwayo hapa duniani, na zitoke roho zao na hali wao ni
makafiri.
56. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, wala
wao si katika nyinyi. Lakini ni watu wanao ogopa.
57. Lau kama wangeli pata pa kukimbilia au mapango au pahala pa
kuingia basi wangeli fyatuka mbio kuelekea huko.
58. Na miongoni mwao wapo wanao kusengenya katika kugawa sadaka.
Wanapo pewa wao huridhika. Na wakito pewa hukasirika.
59. Na laiti wao wangeli ridhia kile alicho wapa Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa
katika fadhila yake - na pia Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi
Mungu!
60. Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia,
na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
61. Na miongoni mwao wapo wanao muudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni
sikio tu. Sema: Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamuamini Mwenyezi Mungu, na ana
imani na Waumini, naye ni rehema kwa wanao amini miongoni mwenu. Na wanao
muudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu watapata adhabu chungu.
62. Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni nyinyi, hali ya
kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lau kama
wao ni Waumini.
63. Je, hawajui ya kwamba anaye shindana na Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, basi huyo atapata Moto wa Jahannamu adumu humo? Hiyo ndiyo hizaya
kubwa.
64. Wanaafiki wanaogopa isije teremshwa Sura itakayo watajia
yaliyomo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni mzaha! Hakika Mwenyezi Mungu atayatoa
nje hayo mnayo yaogopa.
65. Na ukiwauliza, wanasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na
kucheza tu. Sema: Mlikuwa mkimfanyia maskhara Mwenyezi Mungu na Ishara zake na
Mtume wake?
66. Msitoe udhuru; mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu!
Tukilisamehe kundi moja kati yenu, tutaliadhibu kundi jingine kwa kuwa wao ni
wakosefu.
67. Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali moja.
Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi
Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanaafiki ndio wapotofu.
68. Mwenyezi Mungu amewaahidi wanaafiki wanaume na wanaafiki
wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu kudumu humo. Hayo yanawatosha, na
Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu milele.
69. Ni kama wale walio kuwa kabla yenu. Walikuwa wana nguvu na mali
na watoto zaidi kuliko nyinyi. Basi walistarehea fungu lao, na nyinyi mnastarehea
fungu lenu, kama walivyo starehe kwa fungu lao wale walio kuwa kabla yenu. Na
nyinyi mkazama katika maovu kama wao walivyo zama. Hao ndio ambao vitendo vyao
vimeharibika katika dunia na Akhera; na hao ndio walio khasiri.
70. Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla yao - kaumu ya
Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na miji
iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi. Basi
Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini wao walikuwa wakijidhulumu
wenyewe.
71. Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki
walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na
humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
72. Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake
Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi mema katika Bustani za
kudumu, na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu
kukubwa.
73. Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na wakazanie. Na
makaazi yao ni Jahannamu, na huo ndio mwisho mbaya.
74. Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema
neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya
ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume
wake amewatajirisha kutokana na fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na
wakigeuka Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala
hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru.
75. Na miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema:
Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika
watendao mema.
76. Alipo wapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na
wakageuka, na huku wakipuuza.
77. Basi akawalipa unaafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo
kutana naye, kwa sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyo
muahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.
78. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong'ono
yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua sana ya ghaibu?
79. Wale wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka nyingi na wasio
nacho cha kutoa ila kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli. Mwenyezi Mungu
atawakejeli wao! Nao watapata adhabu chungu!
80. Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara
sabiini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotofu.
81. Walifurahi walio achwa nyuma kwa kule kubakia kwao nyuma na
kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walichukia kupigana Jihadi kwa mali zao na
nafsi zao, na wakasema: Msitoke nje katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una
joto zaidi, laiti wangeli fahamu!
82. Basi nawacheke kidogo; watalia sana. Hayo ni malipo ya yale
waliyo kuwa wakiyachuma.
83. Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni
mwao - na wakakutaka idhini ya kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami kabisa,
wala hamtapigana na adui pamoja nami. Nyinyi mliridhia kukaa nyuma mara ya
kwanza, basi kaeni pamoja na hao watakao bakia nyuma.
84. Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame
kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakafa
na hali ni wapotofu.
85. Wala zisikushitue mali zao na watoto wao. Mwenyezi Mungu anataka
kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke roho zao na hali wao ni
makafiri.
86. Na inapo teremshwa Sura isemayo: Muaminini Mwenyezi Mungu na
piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu miongoni mwao hukutaka
ruhusa na husema: Tuache tuwe pamoja na wanao kaa nyuma!
87. Wameridhia kuwa pamoja na wabakiao nyuma, na nyoyo zao zikapigwa
muhuri; kwa hivyo hawafahamu.
88. Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi
kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio
wenye kufanikiwa.
89. Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake,
wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
90. Na walikuja wenye kutoa udhuru katika Mabedui ili wapewe ruhusa,
na wakakaa wale walio mwambia Mwenyezi Mungu na Mtume wake uwongo. Itawafika
walio kufuru katika wao adhabu chungu.
91. Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio pata cha kutumia,
maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu
wanao fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
92. Wala wale walio kujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha
kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya
kukosa cha kutoa.
93. Ipo njia ya kuwalaumu wale wanao kuomba ruhusa wasende vitani na
hali wao ni matajiri. Wameridhia kuwa pamoja na wanao bakia nyuma. Na Mwenyezi
Mungu amewapiga muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawajui.
94. WATAKUTOLEENI UDHURU mtapo warudia. Sema: Msitoe udhuru;
hatukuaminini. Mwenyezi Mungu amekwisha tueleza khabari zenu. Na Mwenyezi Mungu
na Mtume wake wataviona vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa ya siri
na ya dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
95. Watakuapieni kwa Mwenyezi Mungu mtakapo rudi kwao ili
muwaachilie mbali. Basi waachilieni mbali. Hakika hao ni najsi, na makaazi yao
ni Jahannamu, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
96. Wanakuapieni ili muwe radhi nao. Basi hata mkiwa radhi nao
nyiye, Mwenyezi Mungu hawi radhi na watu wapotofu.
97. Mabedui wamezidi sana katika ukafiri na unaafiki, na wameelekea
zaidi kutojua mipaka ya aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
98. Na katika Mabedui hao wapo wanao fikiri kuwa wanayo yatoa ni
gharama ya bure, na wanakungojeleeni mambo yakugeukieni. Mageuko maovu yatakuwa
juu yao! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
99. Na katika Mabedui wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho, na wanaitakidi kuwa wanayo yatoa ndiyo ya kuwasogeza kwa Mwenyezi Mungu
na ya kuwapatia dua za Mtume. Naam! Hayo ni kweli mambo ya kuwasogeza. Mwenyezi
Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira
Mwenye kurehemu.
100. Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na
walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye;
na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko
kufuzu kukubwa.
101. Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika
wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi
tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu
kubwa.
102. Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na
vingine viovu. Asaa Mwenyezi Mungu akapokea toba zao. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
103. Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na
uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusikia Mwenye kujua.
104. Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake,
na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na
Mwenye kurehemu?
105. Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na
Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na
dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
106. Na wapo wengine wanangojea amri ya Mwenyezi Mungu - ama
atawaadhibu au atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye
hikima.
107. Na wapo walio jenga msikiti kwa ajili ya madhara na ukafiri na
kuwafarikisha Waumini, na pa kuvizia kwa walio mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume
wake hapo kabla. Na bila ya shaka wataapa kwamba: Hatukukusudia ila wema tu. Na
Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao ni waongo.
108. Usisimame kwenye msikiti huo kabisa. Msikiti ulio jengwa juu ya
msingi wa uchamngu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame ndani
yake. Humo wamo watu wanao penda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanao
jitakasa.
109. Je! Mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya kumcha Mwenyezi
Mungu na radhi zake ni bora au mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya ukingo
wa shimo linalo burugunyika, na likaburugunyika naye katika Moto wa Jahannamu?
Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
110. Na jengo lao hilo walilo lijenga litakuwa sababu ya kutia wasiwasi
nyoyoni mwao mpaka nyoyo zao hizo zikatike vipande vipande. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
111. Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao
kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu - wanauwa
na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyo jilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili
na Qur'ani. Na nani atimizae ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa
biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa,
112. (Kwa) wanao tubia, wanao abudu, wanao himidi, wanao kimbilia
kheri, wanao rukuu, wanao sujudu, wanao amrisha mema na wanao kataza maovu, na
wanao linda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na wabashirie Waumini.
113. Haimpasii Nabii na wale walio amini kuwatakia msamaha
washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu
wa Motoni.
114. Wala haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila kwa sababu
wa ahadi aliyo fanya naye. Lakini ilipo mbainikia kwamba yeye ni adui ya
Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa mwingi wa kuomba,
mnyenyekevu, mvumilivu.
115. Na haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwahisabu watu kuwa wamepotea baada
ya kwisha waongoza mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kujua kila kitu.
116. Hakika Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na ardhi; huhuisha
na hufisha. Nanyi hamna Mlinzi wala Msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
117. Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na
Ansari walio mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za
baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole
na ni Mwenye kuwarehemu.
118. Na pia wale watatu walio achwa nyuma hata dunia wakaiona dhiki
juu ya ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika kuwa hapana pa
kumkimbia Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwake Yeye. Kisha akawaelekea kwa rehema
yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea toba
na Mwenye kurehemu.
119. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli.
120. Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio jirani zao kubakia
nyuma wasitoke na Mtume, wala kujipendelea nafsi zao kuliko yeye. Hayo ni kwa
kuwa hakiwapati kiu, wala machofu, wala njaa, kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi
Mungu, wala hawendi mahali panapo waghadhibisha makafiri, wala hakiwapati
chochote kutokana na maadui, ila huandikiwa kuwa ni kitendo chema. Hakika
Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wanao fanya mema.
121. Wala hawatoi cha kutoa kidogo wala kikubwa, wala hawalivuki
bonde, ila huandikiwa, ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo kuwa wakiya-
tenda.
122. Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini kwa nini hawatoki
baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje
kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?
123. Enyi mlio amini! Piganeni na wale makafiri walio karibu yenu, na
wakute ugumu kwenu. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wacha-
Mngu.
124. Na inapo teremshwa Sura wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani
miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walio amini inawazidishia
Imani, nao wanafurahi.
125. Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi inawazidishia uovu
juu ya uovu wao; na wanakufa hali ni makafiri.
126. Je! Hawaoni ya kwamba wanatiwa mtihanini kila mwaka mara moja au
mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki.
127. Na ikiteremka Sura hutazamana wao kwa wao, (kama kwamba
wanasema:) Je! Yuko mtu anakuoneni? Kisha hugeukilia mbali. Mwenyezi amezigeuza
nyoyo zao kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu.
128. Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe;
yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole
na mwenye huruma.
129. Basi wakigeuka, wewe sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Hapana
mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi namtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola Mlezi wa Kiti
Kikuu cha Enzi.