Part 17

 

21 - AL - ANBIYAA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza. 

2. Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo. 

3. Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona? 

4. Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. 

5. Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyo tumwa wale wa mwanzo. 

6. Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je, wataamini hawa? 

7. Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui. 

8. Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele. 

9. Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka. 

10. Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii? 

11. Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine. 

12. Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia. 

13. Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa! 

14. Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu. 

15. Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio fyekwa, wamezimika. 

16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa mchezo. 

17. Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo. 

18. Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua. 

19. Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki. 

20. Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei. 

21. Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua? 

22. Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua. 

23. Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo. 

24. Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza. 

25. Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu. 

26. Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa. 

27. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake. 

28. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea. 

29. Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu. 

30. Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini? 

31. Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka. 

32. Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake. 

33. Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea. 

34. Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele? 

35. Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa. 

36. Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema! 

37. Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize. 

38. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli? 

39. Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa! 

40. Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula! 

41. Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka. 

42. Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi. 

43. Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi! 

44. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda? 

45. Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa. 

46. Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu. 

47. Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu. 

48. Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu, 

49. Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama. 

50. Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi je! Mnayakataa? 

51. Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua. 

52. Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu? 

53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu. 

54. Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhaahiri. 

55. Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu? 

56. Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo. 

57. Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkisha geuka kwenda zenu. 

58. Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie. 

59. Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu. 

60. Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim. 

61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia! 

62. Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim? 

63. Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka. 

64. Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu! 

65. Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi. 

66. Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni? 

67. Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini? 

68. Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo! 

69. Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim! 

70. Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri. 

71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote. 

72. Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawajaalia wawe watu wema. 

73. Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu. 

74. Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu. 

75. Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema. 

76. Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa. 

77. Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote. 

78. Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo. 

79. Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo. 

80. Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru? 

81. Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu. 

82. Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao. 

83. Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu. 

84. Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada. 

85. Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri. 

86. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema. 

87. Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu. 

88. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini. 

89. Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi. 

90. Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea. 

91. Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu. 

92. Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi. 

93. Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu. 

94. Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia. 

95. Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea, 

96. Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima; 

97. Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu. 

98. Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu. 

99. Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo. 

100. Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo). 

101. Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo. 

102. Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo yatamani nafsi zao. 

103. Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa! 

104. Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao. 

105. Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema. 

106. Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada. 

107. Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote. 

108. Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu? 

109. Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa. 

110. Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo. 

111. Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo. 

112. Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua. 

 

22 - AL -HAJJ

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 

 

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko la Saa (ya Kiyama) ni jambo kuu. 

2. Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali. 

3. Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet'ani aliye asi. 

4. Ameandikiwa kwamba anaye mfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali. 

5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri. 

6. Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu. 

7. Na kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini. 

8. Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru. 

9. Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua. 

10. (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja. 

11. Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi. 

12. Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho mdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotolea mbali! 

13. Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu. 

14. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo. 

15. Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na Akhera na afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila yake itaondoa hayo yaliyo mkasirisha? 

16. Na namna hivi tumeiteremsha (Qur'ani) kuwa ni Aya zilizo wazi, na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. 

17. Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu. 

18. Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo. 

19. Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi walio kufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayo chemka. 

20. Kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao pia. 

21. Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma. 

22. Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuungua! 

23. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri. 

24. Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa kwenye Njia ya Msifiwa. 

25. Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu. 

26. Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu, na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanao sujudu. 

27. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali. 

28. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri. 

29. Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao, na waizunguke Nyumba ya Kale. 

30. Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya Mwenyezi Mungu basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na mmehalalishiwa nyama hoa ila wale mlio somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni na usemi wa uwongo. 

31. Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali. 

32. Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo. 

33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha pahala pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale. 

34. Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu, 

35. Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanao vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa katika tulivyo waruzuku. 

36. Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru. 

37. Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema. 

38. Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila khaini mwingi wa kukanya mema. 

39. Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia - 

40. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. 

41. Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote. 

42. Na wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao watu wa Nuhu, na kina A'ad na kina Thamud, 

43. Na watu wa Ibrahim na watu wa Lut'i 

44. Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa. Nikawapa muda makafiri, kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu! 

45. Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu, ikawa imebaki magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti? 

46. Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani. 

47. Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi. 

48. Na miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, na kisha nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndio marudio yote. 

49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu niliye dhaahiri. 

50. Basi walio amini na wakatenda mema watapata maghfira na riziki za ukarimu. 

51. Na wanao jitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa Motoni. 

52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anapo soma, Shet'ani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayo yatia Shet'ani; kisha Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. 

53. Hayo ni ili alifanye lile analo litia Shet'ani liwe ni fitna kwa wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni ngumu. Na hakika madhaalimu wamo katika mfarakano wa mbali. 

54. Na ili walio pewa ilimu wajue kuwa hayo ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi na waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye waongoa wenye kuamini kwenye Njia Iliyo Nyooka. 

55. Na walio kufuru hawatoacha kuwa katika wasiwasi kwa hilo mpaka Saa iwafikie ghafla, au iwafikie adhabu ya Siku Tasa. 

56. Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi walio amini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani zenye neema. 

57. Na walio kufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha. 

58. Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao ruzuku. 

59. BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapo paridhia. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole. 

60. Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo adhibiwa, kisha akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye maghfira. 

61. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. 

62. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale wanao waomba badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye Juu na ndiye Mkubwa. 

63. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni, na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole na Mwenye kujua. 

64. Ni vyake viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Mwenye kusifiwa. 

65. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu. 

66. Na Yeye ndiye aliye kuhuisheni kisha akakufisheni, na kisha atakufufueni. Hakika mwanaadamu hana fadhila. 

67. Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika. Basi wasizozane nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi. Hakika wewe uko kwenye Uwongofu Ulio Nyooka. 

68. Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayo yatenda. 

69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama katika hayo mnayo khitalifiana. 

70. Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. 

71. Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhaalimu hawatakuwa na wa kuwasaidia. 

72. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso za walio kufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya zetu. Sema: Je! Nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio kufuru, na ni marudio mabaya hayo. 

73. Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa. 

74. Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kuadhimishwa. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda. 

75. Mwenyezi Mungu huteuwa Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. 

76. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Na kwa Mwenyezi Mungu yatarejeshwa mambo yote. 

77. Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe. 

78. Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo stahiki jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume shahidi juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora kabisa, na Msaidizi bora kabisa.